FLAVIAN J. LUTAKANGWA
Law Mambo ya Walawi
Kol Wakolosai
Lk Luka
MSK. Mkusanyiko wa Sheria za Kanisa
Mt Mathayo
Ybs Hekima ya Yoshua Bin Sira
Zab Zaburi
§ Ibara
& Na
/ Au
Mkristo maana yake ni mfuasi wa Yesu
Kristo. Kumbe wale walio wafuasi wa Kristo ndiyo hao wanaitwa Wakristo. Mtu
anaitwa Mkristo mara baada ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Ubatizo ni nini? Ubatizo haupingani na
imani bali huandamana nayo (Gal 3:26-27; Efe 4:5; Ebr 10:22). Ubatizo ni alama
wazi na nguvu ya mambo yanayotendeka ndani ya mtu. Paulo anahesabu imani na
ubatizo kuwa na mapato yaleyale (Gal 2:16-20; Rum 6:3-9). Watu wa zamani hubatizwa
kwa kutoswa majini, na maana ya neno la ubatizo kwa kiyunani ni kutosa majini.
Tendo hili la kutoswa na kutoka majini latumika na Paulo kama mfano: kutoswa
majini maana yake mkosefu azikwa pamoja na Kristo (Kol 2:12), kutoka majini
maana yake mkosefu afufuka pamoja na Kristo (Kol 8:11) ili awe kiumbe kipya
(2Kor 5:7) au mtu mpya (Efe 2:15), au viungo vya mwili mmoja vihuishwavyo na
Roho mmmoja (1Kor 12:13). Ufufuko huo utakuja kukamilika mwisho wa dunia (1Ko
15:12).
Hivyo kulingana na Sheria za Kanisa la
Kirumi, Mkristo anaanza kubanwa na sheria yule tu mwenye uelewa wa kutosha na
mwenye kuanzia umri wa miaka saba. Baada ya Ubatizo mwaliko kwetu sote ni
kulitangaza Neno la Mungu kwa watu wote.
Kwa hiyo, lengo la mwandishi wa kitabu
hiki anataka kutuonyesha maisha yampasayo kuishi kama muumini Mkristo tena
Mkatoliki. Ni kutokana na nia hiyo, mwandishi anakuwa na mtazamo juu ya kuwa na
imani nawe msomaji wa kitabu hiki; kuwa kile utakachotoka nacho kama fundisho
basi ukakigawe na kwa wengine. Kama Askofu Mkuu Furton Sheen alivyoongezea
katika swali mahususi la kwanini Mungu alituumba. Yeye alisema ya kuwa Mungu
ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na kabla ya kwenda kwake mbinguni
basi tugawiane na kupeana yale tuliyojifunza (tuwafundishe na watu wengine, na
siyo kubaki nayo sisi wenyewe; huo utakuwa uchoyo na tutaonyesha wazi kwamba
wengine hatutaki waweze kufika kwa Baba muumba wetu).
Mpangilio
wa Kitabu
Kitabu hiki kina jumla ya sehemu nane.
Sehemu ya kwanza inahusu Maneno. Sehemu ya pili inahusu utumishi kwa wote.
Sehemu ya tatu inaongelea juu ya Matendo Sehemu ya nne inahusu Imani. Sehemu ya
tano inazungumzia juu ya Sakramenti. Sehemu ya sita inahusu ukipenda dunia
zaidi, kumpenda Mungu hakuko ndani yako. Na sehemu ya saba inaongelea juu ya
Mpinga Kristo. Na sehemu ya mwisho inahusu juu ya wapi tumaini lako lilipo? Na
mwisho mwishoni ni juu ya Hitimisho na Rejea.
Kuna methali isemayo “Mkono mtupu haulambwi” ukisema uishi kwa
kufuata maneno tu ya watu, kwa hakika utapotoshwa. Unachopaswa kuangalia na kujiuliza
ni je! maneno hayo yanatoka moyoni au mdomoni tu? Ukishatambua basi unakuwa
katika hali iliyo njema. Na kitu cha pekee kitakachokufanya uone ya kuwa mtu
huyu anachoniambia kitakuwa kina ukweli au kinatoka moyoni ni pale tu mhusika
atakapo jieleza akiwa huru au akiwa amejiachia. Lakini tambua kuwa ni vigumu
sana mtu afikie hatua hiyo, maana mwanadamu mara zote anakuwa ni mtu wa hofu
sana. Inaweza ikawa hofu ya mamlaka, hofu ya uthubutu au hofu ya kitu chochote
kile ambacho kwayo anafikiria juu ya matokeo yake itakuwaje.
Maneno huonyesha mtu, “kutikisa
chekecheke, itabaki wishwa; vilevile ila za mtu katika kujadili. Tanuu hujaribu
vyombo vya mfinyanzi; vilevile jaribio la mtu ni kujadili. Matunda ya mti
huonyesha ulimaji wake; vilevile kujadili mawazo ya moyoni. Usimsifu mtu
usijemsikia anajadili; hakika hilo ni jaribio la wanadamu.” Aya hizi zinatuonyesha wazi kuwa
ukitaka kumjua mtu na kwa namna ya pekee kupitia nafasi, embu jaribu umpe
nafasi ya kuongea au kujadili naye. Kupitia maongezi au kujadili nae utagundua
kile akisemacho kinatoka moyoni au mdomoni. Pia wakati wa majadiliano hayo
jitahidi umpe uhuru, hiyo ndiyo nafasi pekee itakayompatia mwanya wa kufunguka
kweli kweli.
Mfano huu wa kumpatia mtu uhuru ili
aweze kuongea pasipo wasiwasi na bila kujibakiza, naufananisha na mfano wa
mtoto mdogo. Mtoto mdogo anaweza akawa ametenda kosa fulani. Na kwa sababu
mtoto mara zote ukimbananisha vizuri basi huwa anasema ukweli. Sasa ikatokea
mtoto huyu kakosea au kuna kitu nyumbani hakiko sawa na pengine mtoto huyu
alishiriki moja kwa moja au alishuhudia. Utakapo muuliza akwambie ilikuwaje na
ukamhakikishia kuwa hutomfanya kitu chochote hata kama ni yeye aliyeharibu kitu
hicho, basi atakwambia chanzo cha mkasa na namna ilivyotukioa mpaka mwisho. Kwa
nini anafanya hivyo? Anaongea yote kwa kuwa umeshamtengenezea mazingira ya yeye
kusema kile kilichotendeka kwa uwazi kabisa na ndicho hicho kitokacho moyoni.
Katika fundisho hilo hilo, tuchukulie
mfano wa mtu mzima. Mtu mzima anatambua kilicho chema na kibaya pia. Kumbe
anaweza akawa hajapendezwa na kitu fulani na akaogopa kumfuata mhusika, na badala
yake kama ni mtu wa kutumia kamvinyo au kilevi basi anapotumia ni hali ya
kawaida kuwa anarudi katika asili. Yaani
anakuwa huru na anatenda kama mtoto mdogo. Hivyo anaweza kuanza kuwaeleza
rafiki zake alionao pale juu ya mtu Yule ambaye pengine anamkwaza katika
maisha. Na hapo kile atakacho kuwa anakitoa kwa hakika chatoka moyoni. Au
mwingine anachukizwa na mtu, ila hana au hawezi kumfuata na kumweleza. Badala
yake anasema na kupanga pia kunuwia kwenda kumnywea pombe. Akijisemea leo
atanitambua, na kweli anapokunywa na kukutana naye anamweleza kila kitu kutoka
moyoni kabisa; maana anakuwa amerudi katika asili yake na hivyo kutomwonea aibu
kwa kuwa anakuwa yuko huru. Ndiyo maana muda mwingine watu wanasema pombe
inatabia ya kukata mshipa wa aibu. Ina maana sawa na mfano huo, kwa kuwa
akishalewa basi hawezi kutunza siri na akianza kuongea karibu kila kitu
anachokichukia au kukipenda katika maisha ataweza kukwambia.
Kwa hiyo, tunatahadhalishwa sana kuwa
na umakini katika maneno yetu. Lakini pia tuwe watu wa kuchuja maneno yetu
kabla ya kusema. “Usijadiliane na mtu mwenye maneno mengi, ukaomekeza kuni juu
ya moto wake.” “Usipepete kwa kila upepo, wala
usiipitie kila njia. Uwe mtu thabiti wa akili, na liwe moja neno lako. Uwe
mwepesi wa kusikia, na mzito wa kutoa jibu.”
“Heri walio maskini wa roho, maana
ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika. Heri
wenye upole, maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana
hao watashibishwa. Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema. Heri wenye
moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana
wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni
wao.” Katika fikara za Yesu hao maskini ni watu
wanyenyekevu kadiri ya (Sef 2:3). Maneno “wa roho” yanakosekana katika (Lk 6:20). Lakini hao
maskini ni watu wasio na mali nyingi na watu wa kuonewa. Hali hiyoo yao
huwaweka tayari kupokea ufalme wa mbinguni kwa urahisi bila pingamizi kubwa. Na
hilo ndilo neno kuu katika hotuba hii juu ya heri (Lk 4:18; 7:22; Mt 11:5; Lk
14:13; Yak 2:5). Hali hii ya unyenyekevu ni sawa na utoto wa kiroho ambayo
yahitajika sana katika kuingia ufalme wa mbingu (Mk 9:33 nk; Lk 9:46; Mt 19:13
nk). Ufalme wa mbingu ni siri waliyofumbuliwa wadogo (Lk 12: 32; 1Kor 1: 26 n.k).
Maskini ni sawa na watu wanyonge watajwao katika Lk 1:48, 52; 14:11; 18:14; ni
watu wa “mwisho” duniani hapa watakaokuwa watu wa “kwanza” katika ufalme wa
mbingu (Mk 9:33); ni watu wadogo kwa kweli walio watu wakubwa (Lk 9:48; Mt
19:30; 20:26).
Ni kweli kwamba Kristo awadai tajiri na
fukara umaskini wa roho. Lakini amesifu mara nyingi umaskini katika matendo. Na
hasa huwadai wanafunzi ufukara katika matendo na si katika nia (maneno) tu (Mdo
2: 44; 4: 32; Mt 6: 9; 10: 9-10). Yeye
mwenyewe amekwisha tuonyesha mfano wa kuishi kifukara si kwa maneno bali
matendo (Lk 2: 7; Mdo 8: 20) na kiunyenyekevu (Mt 11:29; Yn 13: 12 nk; Flp
2:7). Na akajifanya sawa na wadogo na watu duni (Mt 25: 45; 18:5).
Yesu kuhani mkuu. “Tena wale walifanywa
makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na mauti wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa
milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa
kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana
ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii: aliye mtakatifu, asiyekuwa na
uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko
mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine,
kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kasha kwa ajili ya
dhambi za hao watu, maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.”
Atakaye
kuwa mkubwa na awe mdogo.[9] Katika utumishi wetu tunapaswa
kuongozwa na unyenyekevu. Tunapoamua kujitoa kwa ajili ya wengine ili
kuwatumikia, hatuna budi kujishusha ili tuweze kuendana na hadhira.
Kuhani
ni nani?
Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa
katika wandamu amewekwa kwa ajili ya wandamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili
atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao
wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katik ahali ya udhaifu; na
kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya
nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu
ajiywaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni.
Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakinii
yeye aliyemwambia, ndiwe mwanangu, mimi
leo nimekuzaa.”
Tunaambiwa Yesu ameanza kuhubiri au
kufundisha yapata miaka kama thelathini.
Nawe je umeanza kufundisha au kumtangaza Kristo katika maisha yako ukiwa
na umri gani? Tafakari sasa, ni mara ngapi umeshindwa kutekeleza wajibu wako
kama Mkristo? Mara ngapi kama Mkristu umeshindwa kuwasikiliza wale wanaokuja
kuomba msaada? Ni mara ngapi umetupilia mbali ombi au misaada ya wanaokulilia
uwasaidie?
Hakika utumishi tunaoongelea hapa ni
ule wa kutenda na kufanya vitu kwa Upendo kama Kristu alivyotutendea nasi
tuliokuwa hatusitahili; ila akatusitahilisha. Kuna mtu mwingine anaweza akawa
na vitu fulani vilivyo ndani ya uwezo wake. Lakini ule mguso wa utumishi kwa
wote akakosa. Ndipo hapo kwa mfano mtu anakuja kuomba umsaidie hata chakula, na
kwa kuwa anajua una chakula tena cha kutosha. Unaishia tu kumpa pole, pale
anapokwambia umsaidie kwani amelala njaa. Tusiwe watu wa kuchukulia mambo juu
juu tu (sympath); bali watu wa kuvaa shida za wengine na kuziona kama ni zetu
yaani zituguse (empanth). Na huu ndiyo utumishi wenyewe, wa kuwa tayari na
kuwajibika kwa ajili ya wengine.
Matendo yanaongea au yanasema zaidi
kuliko maneno. Haya ni maneno ambayo
tumeyazoweya kuyasikia mara nyingi. Nitoe mfano mmoja ambao utatupa tafakari
nzuri ya kutambua matendo haya ni nini maana yake katika maisha. Walitokea watu
wawili walioishi kwa kupendana na kujaliana. Mmoja aliitwa FRIDA na mwingine
aliitwa MAUA, yaani walikuwa wameivana sana. Sasa kama tujuavyo hakuna masika
isiyo kuwa na ncha, yaani hatuwezi kukaa na kutegemea kuwa mara zote maisha
yataenda vile tutakavyo. Sasa ikatokea MAUA akaugua ghafla. FRIDA akapata
taarifa kuwa rafiki yake MAUA alikuwa ni mgonjwa basi akaenda kumwona na uzuri
alikuwa jirani yake tu hatua kadhaa mpaka kufika kwake. Sasa FRIDA akamshauri
MAUA aende kufanya vipimo hospitalini. Kweli akajitahidi kwenda zahanati
akapimwa, ila akaambiwa hawajaona ugonjwa wowote ule. Basi akarudi kwanza
nyumbani na kuanza kujiapanga ili aweze kwenda kituo cha afya pia kwa vipimo
zaidi.
Siku ya siku ameshajiandaa akaenda, pia
majibu yakatoka ya kuwa hawaoni tatizo lolote. MAUA akawaza moyoni tatizo ni
lipi sasa? Mbona hali inazidi kudhoofika zaidi? Akajisemea moyoni kwa kuwa bado
nina kitu mfukoni ya kuniwezesha, ngoja niende hospitali ya Wilaya.
Akaunganisha na kufika kule, majibu yakawa yale yale kuwa hawaoni ugonjwa. Basi
akaamua kurudi nyumbani na kusema basi bora nikae nymbani tu ili nifie hapa
hapa kwa watoto wangu na mume wangu. Sasa baada ya FRIDA kusikia kuwa shahiba
wake amerudi kutoka hospitali, basi akasema ngoja akamwone. Kumbuka tuko katika
ulimwengu wa utandawazi sasa, cha ajabu na cha kutisha walipenda kuwasiliana sana
na wakati mwingine kwa njia ya simu. Hallo... shogaa yangu naomba leo saa kumi
kamili unisindikize kusuka saloon. Na hivyo walishirikiana vema, ila maajabu
wakati wote yuko huko hospitali hakuthubutu kumtafuta na kumwuliza juu ya
maendeleo yake.
Kwa hiyo FRIDA aliposikia amerudi
kutoka hospitali alikwenda kumwona MAUA. Alipofika na kumwona alivyokuwa
amekonda loo….. hata neno la faraja ya kuwa pole sana shogaa yangu
halikutolewa. Mwisho wa siku akaangua kilio na hatimaye wote wawili wakawa watu
wa kutoa machozi tu. Basi baadae FRIDA aliinuka na kurudi nyumbani. Hata
hakupata tena hamu ya kwenda kumwona rafiki yake………… Ndugu
msomaji wa kitabu hiki, mwandishi anataka kukupa somo hili
“Akufaaye
kwa dhiki ndiye rafiki.” Na Yoshua bin sira anasema, “Wala usisahau kwenda
kumtazama mgonjwa, mradi ukifanya hivi utapata kupendwa na watu.” Kwahiyo, unapomtembelea mgonjwa unabainisha
ukweli huu: rafiki katika shida ni rafiki wa kweli. Unapomtembelea mgonjwa mpe
matumaini, usimkatishe tamaa wala usimwongezee uchungu, maumivu na huzuni.
Mwambie pole na kumpa matumaini ya kuwa utapona.
Ndiyo maana wanasema ‘moyo wenye
furaha, una mwili unaohangaika au kuteseka.’ Na hivyo inakamilishwa na methali isemayo
ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Kumbe tutambue kuwa matendo yetu yanasema zaidi
kuliko kingine chote. Kwa mfano; Wewe huwezi kusema unawapenda watu waote,
wakati hapohapo tunaona kuna watu unawanyanyasa sana kwa namna mbalimbali. Hii
inatendeka zaidi pale unapokuwa umegubikwa na kutawaliwa na majivuno pia kiburi
na kujiona wewe ndiye hakuna mwingine. Ndiyo maana Maandiko yanatuambia ya kuwa
hatuwezi kujigamba ya kuwa tuna imani, wakati matendo yetu hayaonekani na hivyo
yamekufa.
Mtume Petro mwenyewe wakati wa
kukamatwa kwa Yesu alimkana Yesu, kama alivyokuwa amekwisha kumwambia kuwa
kabla jogoo hajawika mara tatu utakuwa umenikana kama zisemavyo Injili nne (Mt
26:69-75; Mk 14:66-72; Lk 22:54-62; Yn 18:25-27).
Ø Namna ya uongeaji (Mt 26:73).
Ø Namna ya kutembea kwake (Mt 26:71).
Ø Namna ya mwonekano wake wa ukaaji (Mt
26:69).
Kupitia Mtume Petro anachotufundisha ni
kwamba kama msemo mmoja usemavyo kuwa ‘hujafa hujaumbika.’ Na hivyo tunaaswa
tuepukane na kujiamini kipumbavu. Lakini
pale matendo yetu yanapoonyesha Ukristo wetu kwa wengine, basi tuwe tayari
kuendelea kuwadhihirishia watu hawa kuwa ndivyo tulivyo kama Wakristo. Na pia
pale tunaposhindwa kuwa waaminifu katika kuuonyesha Ukristo wetu basi tuwe tayari
kutafuta upatanisho kama alivyoanza kulia Mtume Petro. Kwa maana ya kawaida tu
kama wanadamu tu dhaifu na hivyo tunapaswa kulipokea hilo na kulifanyia kazi
pale tunapoona kweli hatujaenenda vile ipasavyo. “Tukisema kwamba hatuna dhambi,
twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye
ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu
wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno
lake halimo mwetu.”
Mwenyezi Mungu ni mwaminifu katika
ahadi zake hata ikipita miaka elfu na maelfu, anabaki mtekelezaji mwaminifu. “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu
hayatapita kamwe. Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata
malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. Angalieni, kesheni, (ombeni), kwa
kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.”
Ahadi ni kipimo cha kutosha juu ya
uaminifu kwa mhusika. Ni kwa mantiki hiyo inapofikia hatua ya utekelezaji tu,
hapo mtu anaonekana na kuonyesh ule uaminifu wake kwa kutekeleza ahadi au kile
alichoahidi. Lakini sasa bila kubagua, Wakristo walio wengi siku hizi wamekuwa
kama wanasiasa ambao ni wepesi wa kusema tu ila utekelezaji unakuwa zero.
Sasa kama Wakristo Wakatoliki tunaweka
ahadi zetu kwa Mungu juu ya kumkataa shetani na kuungama imani yetu. Licha ya
hulka yetu kama binadamu, kuna wakati tunavunja ahadi hizo ama kwa kutokujua
kweli au kwa kujua (tukiwa na uelewa wa kutosha juu ya kile tuanyacho kuwa
siyo). Na hii kwa watoto watoto wachanga, wazazi na wasimamizi ndiyo wenye
jukumu hili la kusema ahadi hizo kwa mgongo au niaba ya watoto hao. Ila kwa
wakatekumeni basi kwa kuwa wanakuwa ni watu wazima, hivyo wanakuwa na uelewa
wanajibu pia wao. Au kwa Waamini wote hujikumbushia ahadi hizi siku ile ya
mkesha wa Pasaka. Na katika kujibu inakuwa katika nafsi ya kwanza umoja (yaani
unajibu wewe kama wewe au kama vile ulikuwa unaulizwa peke yako).
Padre anawashauri wazazi na
wasimamizi kwa maneno yafuatayo:
Ndugu zangu, wazazi na wasimamizi,
watoto mliowaleta karibu watapata uzima mpya utokao katika mapendo ya Mungu,
kwa maji na Roho Mtakatifu, kwa Sakramenti ya Ubatizo. Basi, ninyi jitahidini
kuwalea katika imani, kusudi uzima ule wa Mungu usichafuke, bali uweze kukua
ndani yao, siku kwa siku.
Basi, iwapo kwa imani yenu mko tayari
kupokea wajibu huo, mkikumbuka na Ubatizo wenu ninyi wenyewe, kataeni dhambi na
kuungama imani katika Yesu Kristu, hiyo ndiyo imani ya Kanisa wanamobatizwa
watoto.
Mwamkataa
shetani?
Wazazi na Wasimamizi Namkataa.
Na
mambo yake yote?
Wazazi na Wasimamizi Nayakataa.
Na
fahari zake zote?
Wazazi na Wasimamizi Nazikataa.
Mwasadiki
kwa Mungu Baba mwenyezi, mwumba mbingu na dunia?
Wazazi na Wasimamizi Nasadiki.
Mwasadiki
kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa na Bikira Maria,
akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka katik wafu, amekaa kuume kwa Baba?
Wazazi na Wasimamizi Nasadiki.
Mwasadiki
kwa Roho Mtakatifu, Kanisaa Tkatifu Katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo
ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele?
Wazazi na Wasimamizi Nasadiki.
Hiyo
ndiyo imani yetu. Hiyo ndiyo imani ya Kanisa, tunayoona fahari kuiungama katika
Yesu Kristu Bwana wetu. Wote Amina.
Kwa
hiyo, kama Wakristo Wakatoliki tuna deni la kutekeleza kwa kuishi ahadi zetu za
Ubatizo. Ndiyo maana nimekuja na msemo huo kuwa ahadi ni deni.
Mpendwa msomaji wa kitabu hiki, tambua
ya kuwa mpaka sasa wewe ni mtoto wa Mungu. Kwani kwa Ubatizo, Mungu ametupokea
kama wana wake katika Kristu. Ndiyo maana tunaaambiwa kuwa “Bali
ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya
Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa
la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”
Ingawa kwa Kiswahili neno imani
lina maana mbalimbali. Ila zaidi inahusiana na kitenzi kuamini, kinachofanana na kusadiki.
Hapo ni kukubali ukweli wa jambo
lisiloweza kuthibitishwa. Katika dini msingi wake ni mamlaka ya Mungu aliyeshirikishwa
ukweli huo kwa njia ya ufunuo maalumu ili
kumsaidia binadamu amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani na ya baadaye. Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza
kushikilia jambo bila ya uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo unatia maanani pia akili katika ujuzi wa ukweli. Kadiri ya Mtume
Paulo imani ikifuatana
na tumaini na upendo ni adili kuu mojawapo, msingi, mzizi na chanzo cha wokovu. Na hivyo kwa husrikiana na makala tunaweza kujifunza kwa mapana juu ya imani kama
Wakristo.
Kila mara mtu anafuata ama umbile, asipopita fikra za kibinadamu tu (Imani), anapolenga mbinguni kwa njia ya utakatifu. Roho hizo zinazotuongoza maishani ni namna maalumu za
kupima, kuona, kuhisi, kupenda, kushabikia, kutaka na kutenda. Basi, roho ya
imani ni kupima yote kwa mtazamo wa juu ambao unapita maumbile na kutegemea mamlaka ya Mungu katika kujifunua,
na ukweli wake katika kutushirikisha utukufu. Tunaelewa zaidi roho ya imani tukiangalia iliyo kinyume
chake, yaani upofu wa roho unaozuia mtu asione mambo ya Mungu isipokuwa kidunia na
kutoka nje. Ndiyo maana Israeli haikuelewa uteuzi wake kadiri ya ukweli wa Mungu ulio wa juu kuliko ukabila au ubaguzi wowote.
Imani ina mitazamo mipana kuliko hiyo ya Waisraeli, kutokana na usahili wake unaoshiriki hekima ya Mungu. Kumbe “Basi
imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo
yasiyoonekana.” Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa
ndani yake, naye ndani yetu: kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Imani ni nje ya milango mitano ya fahamu
kwa maneno mengine. Juu sana kuliko mifuatano ya mawazo, ni tendo sahili ambalo
tunamsadiki Mungu anayefunua na papo hapo anajifunua. Kwa tendo hilo lipitalo
maumbile tunaambatana naye pasipo udanganyifu na hivyo katika giza tunalenga kutazama mambo ya Mungu, juu kuliko hakika zote za kibinadamu. Hakika inayotokana na imani
tuliyomiminiwa na Mungu, inapita hata hakika ya akili tunayoweza kujipatia kwa kuzingatia miujiza inayothibitisha ufunuo wake.
Imani ni zawadi ya Mungu: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi
zenu, ni kipawa cha Mungu.” Ni kama hisi ya Kiroho inayotuwezesha kusikia ulinganifu wa mafumbo aliyotufumbulia, yaani kusikia sauti yake kabla hatujakaribishwa kumuona uso kwa uso.
“Lakini sisi
hatukuipokea roho ya dunia bali Roho itokayo kwa Mungu, makusudi tupate kujua tuliyokirimiwa
na Mungu, nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya
kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa
maneno ya rohoni. Basi, mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa
jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, ni
nani aliyefahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.” Ili ifanye hivyo imani inasaidiwa na vipaji vya akili na hekima, lakini yenyewe ndiyo inayotufanya tushike Neno
la Mungu pasipo
udanganyifu.
Ingawa mafumbo
yake ni ya giza kwetu, adili la imani ni bora
kuliko ujuzi mwangavu walionao malaika kwa umbile lao, kwa sababu imani tunayomiminiwa
inalingana na uzima wa milele, kwa kuwa ndiyo mbegu yake. Malaika wenyewe walihitaji zawadi hiyo waweze
kulenga hali
ipitayo maumbile waliyoitiwa. Mungu
anapotujalia imani, anapenya roho yetu na kusema
nayo si kwa mifuatano ya maneno, bali kwa wazo la ghafla. Imani ikifika, tunaachana na mfuatano wowote wa mawazo
tuliokuwanao pamoja na sababu zake: tunaviweka chini ili imani ivikalie kama mtawala. Imani ikiangaza akili kwa mng’ao wa kweli zake, mara utashi unahisi joto la upendo wa Mungu. “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati
wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani
yetu. Imani inatakiwa kukua kila siku.”
Mwito
ni huu; “Enyi mnaomcha Bwana, mwaminini Yeye sana, thawabu yenu haitawapotea.
Enyi mnaomcha Bwana, sasa tarajieni mema na furaha ya daima na rehema.
Angalieni vizazi vya kale mkaone: nani aliyemtumaini Bwana akaaibika? Nani
aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita akadharauliwa?”
Kumbe,“Imani inaweza
ikawa kubwa ndani ya Mkristo mmoja kuliko ndani ya mwingine, upande wa akili kutokana
na hakika na imara kubwa zaidi katika kushika ufunuo, na upande wa utashi
kutokana na utayari na utiifu au tumaini kubwa zaidi” kwa kuwa; “imani tunayomiminiwa inalingana na zawadi ya neema, ambayo
si sawa kwa wote” alisema Mtakatifu Thoma
wa Akwino. Yesu
Kristo mwenyewe aliwasema
wanafunzi wake kuwa wana imani haba ; kumbe alimuambia mwanamke Mkananayo kuwa Mama, imani yako ni kubwa!
Imani inaweza
kukua kwa upana na kwa dhati au nguvu. Inapanuka tunapozidi kujifunza yale yote Kanisa linayoyafundisha. Kumbe, wanateolojia wanayajua wazi, lakini si kwamba imani yao ni ya dhati
na ya nguvu kadiri ilivyoenea. Hivyo, tunakuta watakatifu wasiojua mengi katika hayo, lakini wanapenya mafumbo
yalivyofumbuliwa na Injili kwa usahili. Mitume
wa Yesu walimuomba imani
hiyo waliposema, Tuongezee imani. Yesu akawaambia,
“Yoyote mtakayoomba katika sala mkiamini,
mtapokea.” Tutayapokea hasa
tukijiombea kwa udumifu yaliyo ya lazima au ya kufaa sana kwa wokovu
wetu, kama vile ustawi wa
maadili.
Thamani ya imani inapimwa na matatizo inayoyashinda katika majaribu: “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu… yeye aliyeambiwa: Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu… Kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto. Wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno,
walijaribiwa, waliuawa kwa upanga;
walizungukazunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa
mabaya watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao.” Mambo kama hayo yanatokea hata
siku hizi. “Basi na sisi pia, tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye
kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”
Gregori
Mkuu
(540-604) alisema, “Mzingatieni
Kristo aliyevumilia upinzani wa namna hiyo kutoka kwa wakosefu. Hapo katika tabu yoyote mtaona dawa katika msalaba
wa Yesu. Humo mtakuta
vielelezo vya maadili yote”. Mtakatifu Thoma wa Akwino (1225- 1274) alisema, “ukiyakumbuka
mateso ya Yesu hatutaona chochote kuwa kigumu au cha tabu tusiweze
kukivumilia kwa subira na upendo.” Imani ikistawi inatufanya kwa kawaida tuzidi
kuhisi fumbo la Kristo; polepole hisi hiyo ipitayo maumbile inakuwa sala ya
kumiminiwa yenye kupenya na
kuonja, asili ya furaha na amani: “Furahini katika
Bwana sikuzote; tena nasema, furahini… Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote,
itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
ü Tunapaswa kuishi hivyo kwa kupima yote kwa mwanga huo wa
juu: kwanza Mungu, halafu nafsi yetu, jirani na matukio yote. Je, kuna haja ya kusema tumzingatie Mungu kwa
imani? Bila ya shaka! Kwa kuwa mara nyingi tunamzingatia kwa dhana zisizo na msingi, kwa miguso ya kibinadamu mno na kwa maono yetu, badala ya kupitia ushuhuda alioutoa juu yake mwenyewe. Pengine hata tunaposali
tunajisikiliza tu kwa kumkopesha Mungu mawazo yetu yanayotokana na umimi. Tunapojiamini
kipumbavu tunaelekea
kudhani huruma ya Mungu ni kwa ajili yetu, na haki yake kwa watu tusioelewana nao. Kumbe tukikata tamaa tunatilia shaka kimatendo upendo wa Mungu kwetu na
huruma yake kuu. Kwa imani tunamuona Mungu kupitia mafumbo ya maisha na mateso
ya Mwokozi na kupitia uhai wa Kanisa linalofanywa upya na Ekaristi
Takatifu tuipokeayo kila siku.
ü Jicho la imani linasifika zaidi na zaidi kwa ufishaji wa hisi na maono, maoni na matakwa yetu: hapo tu unakuja kuanguka polepole ule mtaji wa kiburi na majivuno unaotuzuia tusione mambo ya Mungu au tuone tu vivuli
vyake na tata zake.
ü Tunapaswa vilevile kujitazama kwa imani. Tukijitazama
kibinadamu tu, tunaona ndani mwetu sifa za umbile ambazo mara nyingi tunazizidisha. Baadaye,
majaribu yakituonyesha tulivyojidanganya tunavunjika moyo kwa urahisi. Kumbe kwa imani tunakuja kujua utajiri upitao maumbile ambao Bwana ametutia katika ubatizo na kutuongezea kwa Ekaristi Takatifu, yaani thamani ya Neema
inayotia Utakatifu, ya uwemo
wa Utatu Mtakatifu pamoja na Ukuu wa
Wito wa Kikristo. Tunakuja kujua pia vizuio vya ustawi wa uzima
huo, kwa mfano usahalifu wa mbegu ya uzima wa milele iliyopandwa ndani mwetu, na kiburi cha kipumbavu. Kwa
mtazamo huo wa juu tunakuja kujua mapema kilema kinachotutawala na kivutio maalumu cha neema tulicho nacho, ambavyo cha kwanza
kikomeshwe na cha pili kistawishwe.
ü Lakini NENO
la Mungu linatupa uhakika wa imani kwa kuwa “imani huja kwa kusikia Neno la
Kristo.
Mtu akiliamini neno la Mungu, kwamba Mungu hawezi kusema uwongo, moyo wake
utapokea uhakika huo wa imani). Ndani yake, litajengeka taraji la kupokea, kila
anapotoa. Atajua kuwa kutoa sadaka si kupoteza, bali ni kupanda kwa ajili ya
mavuno na baraka kutwaa zaidi. Kuanzia sasa, pokea uhakika kwamba, ukitoa kwa
imani ya kupokea, utapokea. Ukitoa bila imani ya kupokea, hautapokea, utakuwa
umechangia tu. Hivyo mbegu haiwezi kuzaa, kwa maana “….kila tendo lisilotoka
katika imani, ni dhambi.”
ü Hakuna
mkulima anayeweza kutoa kidogo, wakati anaamini mavuno ni mengi. Atoaye kidogo
hana imani ya kupokea. Anaamini inapotea na ndiyo maana anaona ni bora apoteze
kidogo. Lakini mwenye imani ya kupokea,
hutoa kwa wingi kwa sababu anajua sadaka yake haipotei, bali imepandwa na
itazaa sana. Kutoa sadaka pungufu ya ile uliyoazimia mwanzo au pungufu ya ile
aliyokuongoza Mungu kutoa.
Ukipanga moyoni mwako kutoka nyumbani kumpa Mungu kiasi fulani cha sadaka,
baada ya azima hiyo Mungu anakuwa ameipokea sadaka tayari. Wakati wa utoaji,
usipunguze. Laa! sivyo utakuwa unamwibia Mungu. Watu wengi hukosea kwa kufika
Kanisani wakiwa wamepunguza sadaka ya Mungu. Katika sadaka hiyo hiyo ananunua
gazeti, pipi, au analipa nauli.
ü Lakini tunayesahau zaidi kumtazama kwa imani ndiye
jirani. Tunamtazama kibinadamu tu, tukiathiriwa na dhana zisizo na msingi,
kiburi, wivu na vilema vingine. Kwa hiyo ndani yake tunakubali yale
ambayo yanatupendeza kibinadamu, yanatufaidisha au kutukuza; kumbe tunahukumu
yale ambayo yanatukinaisha, yanamfanya bora kuliko sisi na kutushusha. Dhambi ngapi za kuhukumu na kusingizia zinatokana na mtazamo huo uliofunikwa na utaji wa umimi!
Tukijifunza kumtazama jirani kwa imani ni faida kubwa pande zote. Hapo tunakuja kuwaona wakubwa wetu
kama wawakilishi wa Mungu, na kuwatii kwa moyo pasipo kuwasema. Tunaona kuwa
wasiotupendeza wamekombolewa kwa damu ya Kristo, pengine ni viungo vya mwili wake
vinavyokaribia moyo wake kuliko sisi: mara nyingi tunaishi miaka pamoja na watu
safi tusitambue uzuri wa roho zao. Vilevile, tukija kuwatazama kwa imani
wanaotupendeza, pengine tunavumbua wana maadili ya Kimungu kiasi cha kuzidisha na kutakasa mapendo tunayowaonea; pia kwa wema tunaona vizuio walivyonavyo
kwa utawala wa Mungu na tunaweza kushauriana nao tusonge mbele katika njia
yake.
ü Hatimaye tunapaswa kutazama kwa imani matukio yote ya
maisha yetu, ya furaha na ya uchungu vilevile. Mara nyingi tunaridhika kuyaona upande wa hisi
tu, au kwa akili iliyoathiriwa na dhambi. Mara chache tunayazingatia Kimungu,
kwa kuona kwamba “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema” :hata katika upinzani, matatizo makubwa yasiyotarajika
na dhambi (tukiweza kujinyenyekesha kutokana nazo). Katika kukosewa haki na
watu tunaweza kutambua haki ya Mungu ikiadhibu makosa ya siri ambayo hatulaumiwi na mtu; au
tunahisi majaribu ya Kimungu, na utakaso unaokusudiwa kupatikana kwa njia ya hayo.
ü Kabla ya imani yetu kutakaswa kwa majaribu kadhaa ya aina
hiyo, tujitahidi kukua katika imani, badala ya kupima yote kibinadamu tu. Ni
lazima tujinyime mianga midogo na ya bandia ili tujaliwe ile ya juu; tuache
kufuata mno akili yetu ili tuone uangavu mkuu wa mafumbo ya imani na kuishi kulingana nayo. Hivyo
tunaelewa kwa nini hatutakiwi kuitikia vishawishi dhidi ya imani, bali
kuvikataa au kuviruka kwa kukiri imani kwa dhati zaidi; Bwana anaviruhusu kwa maendeleo yetu tu.
Tujifunze imani aliyokuwa nayo Petro
ambaye baada ya kukesha usiku kucha akivua na hakupata chochote. Na kama ilivyo
kawaida ya wavuvi, kazi hiyo inafayika usiku. Lakini licha ya kutambua na kuwa
na uzoefu wa kazi hiyo ambayo alikuwa akiifanya, Bwana Yesu Kristo anapofika
pale na kumwambia azitupe nyavu zake na kutweka mpaka kilindini basi
alitekeleza vema. Kilichomsukuma ni ile imani tu aliyokuwa nayo, ndiyo maana
anakubali kwa kusema ‘kwa neno lako nitazishusha nyavu.’
Imani inaenda sambamba na matendo tu.
“hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria,bali kwa
imaniya Kristo Yesu,sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani
ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna
mwenye mwili atakayehesabiwa haki.” Gal 2:16
Kuna namna mbalimbali zinazotufanya
kukutana na Kristo Yesu; ambazo ni katika sala, kati ya wenzetu, katika Kanisa,
katika kusoma Biblia, kusikiliza neno la Mungu na hasa katika Misa Takatifu na
Sakramenti (Rejea Mt 18:20; 25:31-36; Mdo 9:3-6; 2Tim 3:14-17). Basi mpenzi
msomaji wa kazi hii nikualike kutafakari nami juu ya Sakramenti. Sakramenti ni
alama ya kuwepo kwa Yesu tayari kutuokooa, yaani kutupatia uzima kwa Roho wake.
Tunavyozidi kumwamini, ndivyo naye anazidi kutujalia uzima. Kuna jumla ya
Sakramenti saba katika Kanisa na ziliwekwa na Kristo mwenyewe; Ubatizo,
Kipaimara, Ekaristi Takatifu, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja
Takatifu ya Upadre na Ndoa.
Sakramenti
ni ishara ionekanayo wazi ya neema isiyoonekana iliyowekwa na Yesu Kristo ili
ilete neema au kuongeza neema rohoni. Sakramenti hizo saba zinagusa hatua zote
na nyakati zote muhimu za maisha ya Mkristo. “Sakramenti zinayajalia maisha ya
imani ya Mkristo, kuzaliwa na kukua, kupona na utume. Katika jambo hili kuna
ufanano fulani kati ya hatua za maisha ya kawaida na hatua za maisha ya kiroho.”
Kuna
Sakramenti zinazotolewa mara kwa mara au mara nyingi (Ekaristi Takatifu,
Kitubio, Mpako wa Wagonjwa na hata Ndoa), lakini pia kuna zile zinazotolewa
mara moja tu katika maisha ya Mkristo (Ubatizo, Kipaimara, Daraja Takatifu ya
Upadre).
Lakini zifuatazo ni sakramenti ambazo zinatumika kumwingiza mtu katika Ukristo
na kumfanya kuwa mdumifu katika misingi ya maisha ya Kikristo ni; Ubatizo,
Kipaimara na Ekaristi Takatifu.
Sakramenti
ni za Kanisa kwa namna mbili “kwamba zipo kwa njia yake’’ na “kwa ajili yake’’.
Ni “kwa njia ya Kanisa’’ kwa sababu Kanisa ni sakramenti ya tendo la Kristo
anayetenda ndani yake kwa njia ya utume wa Roho Mtakatifu. Na pia ni “kwa ajili
ya Kanisa’’ kwani ndizo sakramenti zinazolifanya Kanisa libaki katika Muungano
na Kanisa la mbinguni katika maadhimisho yake hususani katika Adhimimisho la
Ekaristi Takatifu; kwani zinadhihirisha na kuwasilisha kwa watu, hasa katika
Ekaristi, fumbo la ushirika wa Mungu ambaye ni upendo, mmoja katika Nafsi Tatu. Sakramenti zimewekwa ili kuwatakatifuza
wanadamu. Na ni katika kupokea Sakramenti, mwili wa Kristo unajengwa. Na hivyo
Kanisa linasisitiza jumuiya ya waamini wakristo wazifahamu Sakramenti na nguvu
katika maisha ya Mkristo.
Sakramenti
za Kanisa ni mwalimu tosha, kwani zinawafundisha waamini katika maadhimisho
mbalimbali katika Liturujia. Siku zote, Sakramenti zinadai imani thabiti katika
kuzipokea. Na mtu anazidi kuimarishwa katika ufuasi wa Kristo pale anapokuwa rafiki
wa Sakramenti mbalimbali. Kanisa siku zote linaisisitizia jamii ya waamini wawe
na tabia njema ya kupokea Sakramenti mara kwa mara kwa ustawi wa maisha yao kwa
utakatifu. Unapaswa kupokea sakramenti huku umeweka lengo na kusudi la kuipokea
sakramenti hiyo kwa ajili ya kujitakatifuza.
Sakramenti tuzipokeazo zitufae kwa wokovu wetu. Kama tutazipokea kwa lengo
jingine au pasipomastahiri yetu kama hatujajiandaa kiroho.Tutakuwa tunapoteza
muda na tunacheza mchezo wa kuigiza tu.Kwani tujikuta tunapokea sakramenti mara
dufu bila kuchota neema zozote zitokanazo na sakramenti hizo.
Hivyo
basi, Sakramenti ni kwa ajili ya kutakatifuza waamini wakristo.Sakramenti ni
muhimu sana kwa wokovu.Wokovu huo ni wakuwafikisha uzima wa milele. Katika Sakramenti
zote Roho Mtakatifu anahusika moja
kwa moja, Kwani Roho Mtakatifu ni Mungu aliye sawa na Baba na Mwana. Sakramenti
zote zinaangazwa na kuimarishwa na Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Roho
Mtakatifu na Fumbo zima la Utatu
Mtakatifu wa Mungu hujidhihirisha katika Maisha ya Mkristo kwa njia ya
Sakramenti mbalimbali. “Roho Mtakatifu huwaandaa waamini kwa Sakramenti kwa
njia ya Neno la Mungu na kwa njia ya imani inayolipokea Neno hilo katika mioyo
iliyo tayari. Kwa hiyo, sakramenti huimarisha na kuonesha imani.”
Ni kwa
njia ya Sakramenti ya Ubatizo tunakuwa watoto wa Mungu. Tunaondolewa dhambi ya
asili na dhambi nyingine.Tunakuwa jamii ya waamini wa Yesu Kristo.Na kwa
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti
hii ina nafasi ya pekee kwa kuwa ni “Sakramenti ya Sakramenti’’: nyingine zote
zimeelekezwa kwa Ekaristi kama lengo lao.
Tunampokea Yesu Kristo katika Maumbo ya Mkate na Divai, mapaji ya Mkate na
Divai hugeuzwa kuwa Mwili na Damu ya Kristo baada ya Mungu Baba kuwa amemtuma
Roho Mtakatifu aweze kuvitakasa vipaji hivyo (Mkate na Divai ) ili viwe Mwili
na Damu kweli ya Kristo. Hayo hufanywa katika adhimisho la Misa Takatifu
ambapo, Padri kwa kumsihi Mungu Baba aweze kugeuza Mkate na Divai kwa kumtuma
Roho Mtakatifu (Epiklesis). Hivyo
basi, hakuna Misa Takatifu bila adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ekaristi
takatifu ndiyo Kiini cha Maisha ya Kanisa Katoliki, kwani ndiye Kristo jana leo
na milele yote.
Sakramenti ya Kitubio, kwa
kujipatanisha na Mungu na jirani zetu; tunajipatia neema mbalimbali na hayo
yanafanywa kwa kuungama dhambi zetu. Sakramenti ya Kitubio hutupatanisha na
Mungu na jirani zetu pia.Tunarudisha urafiki wetu kwa Mungu kwa njia ya
Sakramenti ya Kitubio.Kitubio ni dawa ya
dhamiri zetu.Kitubio hutuponya majeraha tuyapatayo katika maisha yetu.Kitubio ni ishara ya unyenyekevu
na kujikubali mbele ya Mungu na kuhani wake
yaani Padre kuwa tuwadhambi na tukiungama tutasamehewa dhambi zetu.
Sakramenti ya Kipaimara
hutuimarisha katika kuutetea ukristo wetu kwa gharama zozote,kufa ikiwa
lazima,imani Katoliki ibaki salama.Ni kwa Sakramenti ya Kipaimara tunampokea
Roho Mtakatifu mara ya pili anayetutajirisha kwa vipaji mbalimbali vya Roho
Mtakatifu kama, : i.Hekima ii. Akili iii.Shauri iv.Nguvu v.Elimu
vi.Ibada vii.Uchaji wa Mungu.
Mpako wa
wagonjwa ni sakramenti inayomtia nguvu Mkristo aweze
kuyapokea maumivu na shida katika magonjwa yake kwa kumtumainia Yesu Kristo
aliye Mwokozi wetu na mfano halisi wa Mungu Mtu aliyepata mateso makali ,ni
nani atakayeyasimulia?.Sakramenti ya mpako wa wagonjwa huweza kumponya Mkristo
Kiroho zaidi na kimwili pia.
Sakramenti ya Ndoa ,ni
muungano wa mwanaume na mwanamke katika
kuendeleza kazi ya Mungu ya uumbaji, Kuishi pamoja kwa maisha yao yote.Ni
muungano katika Uaminifu unaofaidisha ustawi wa wanandoa wenyewe wafurahie
maisha yao ya ndoa na watoto watakaowapata wawalee Kikristo.Ni muungano
unaofanywa mbele ya shahidi rasmi wa Kanisa yaani Shemasi ,Padri au Askofu Mkatoliki.Na hivyo
hufanywa kuwa Sakramenti.
Waadhimishaji
wa Sakramenti ya Ndoa ni wahusika wenyewe yaani Mume na Mke baada ya Maridhiano
yao.
Ndoa Katoliki haivunjwi kwa mamlaka yoyote duniani , Ndio maana, Moja ya sifa ya Ndoa Katoliki ni Umoja, na
Uimara wa ndoa (Kudumu kwa ndoa mpaka kifo kiwatenganishe).
Na ni kwa vigezo hivyo, Ndoa Katoliki huwa Sakramenti.
Sakramenti ya Upadrisho, Daraja
Takatifu au Upadre ni Sakramenti inayompa mwanaume mkatoliki uwezo mtakatifu
ili :Atolee sadaka ya Misa Takatifu, Awashirikishe watu sakramenti na
Awahubirie na kuwafundisha watu rasmi (Rej.
Eb 5:1-4; 1Kor 11:24-25), Pia Awaongoze watu na kutoa baraka (Rej. KKK
Na.1592 na Na.1598). Maisha
yetu ya ukristo yanajikita katika kupata Sakramenti Mbalimbali za Kanisa.
Hivyo
basi, maisha ya Mkristo na yanaongozwa na Mungu wa Utatu Mtakatifu; katika kupokea
sakramenti mbalimbali za Kanisa kwa ajili ya wokovu wa roho zetu.
Sakramenti
hii huitwa Ubatizo kutokana na madhehebu
ya msingi ambayo kwayo yanafanyika; tendo
la kubatiza kwa Lugha ya Kigiriki
ni baptizein
likimaanisha ‘’Kutumbukiza’’ au
‘’Kuzamisha’’ ndani ya maji, ndiyo kama alama
ya maziko ya mkatekumeni katika kufa
na Kristo na kufufuka pamoja naye pia. Baada ya hapo anakuwa kiumbe
kipya. Anayebatizwa anauvua utu wa kale anauvaa utu upya na kujinyakulia sifa
ya kuwa kiumbe kipya Mwana wa Mungu. Anayebatizwa anaingia katika orodha ya
watoto na taifa la Mungu. Hivyo basi ubatizo ndio mlango wa Sakramenti zote
yaani ndio lango la kuingilia uzima katika Roho. Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa
huru toka dhambi na tunazaliwa upya na kuwa watoto wa Mungu, tunakuwa viungo
vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume
wake: Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika neno.
Tunampokea
rasmi Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza tunapopata Sakramenti ya Ubatizo. Kanisa
Katoliki linaamini, linaishi na kufundisha kuwa Ubatizo ndio njia ya kipekee
kwa kujipatia wokovu. Kwani Ubatizo ndio mlango wa Sakramenti zote, ndio lango
la kuingia katika maisha ya Roho Mtakatifu.
Na Sakramenti ya Ubatizo inamtaja na kumfunua Mungu Mmoja katika Utatu
Mtakatifu.Hivyo basi ndio maana anayebatizwa anaambiwa, (fulani) Nakubatiza kwa
jina la Baba na la Mwana na la Roho
Mtakatifu. Ndio Kanuni halali na yakufaa
inayotumika katika Kanisa Katoliki, inatumika
kwani ndio tulioachiwa na Yesu mwenyewe mwanzilishi wa Kanisa hili Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Ndiyo
maana tunaithamini Kanuni au fomula ya Ubatizo. Yesu Kristo aliwaambia “Basi
nendeni, mkayafanye mataifa yote kuwa wafuasi mkiwabatiza kwa jina la Baba na
la Mwana na la Roho Mtakatifu.”
Sakramenti
ya Ubatizo ni mlango wa sakramenti zote, ni muhimu sana
na kigezo mahususi kwa namna ya
pekee kwa ukombozi: Iwe kwa kuipokea au kwa kuitamani sakramenti hiyo. Kwa
Sakramenti hiyo watu wanaondolewa dhambi zao hususani dhambi ya asili, wanazaliwa
upya na kuwa wana wa Mungu na wanafananishwa na Kristo kwa alama isiyofutika, wanaingizwa
Kanisani.
Ubatizo
unakuwa halali tu, pale katika adhimisho la Sakramenti ya ubatizo Maji
yanapotumika kwa kumimina maji kichwani mwa mbatizwa kwa kutumia maneno
yanayopaswa kutumia kadiri ya Kanuni maalumu ya Adhimisho la Sakramenti ya
Ubatizo yaani fulani (unataja jina la anayebatizwa). Nakubatiza kwa Jina la
Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu amina.
Katika Sakramenti ya ubatizo tunampokea rasmi Roho Mtakatifu katika “Utatu
Mtakatifu” na kwa tendo hilo tunajinyakulia hadhi ya kuitwa wana wa Mungu,
kwani Mungu ametuzaa rasmi katika Ubatizo huo na Mungu.
“Kwa kuwa wanazaliwa na hali ya kibinadamu
iliyoanguka na kuchafuliwa na dhambi ya asili, hata watoto wachanga wana lazima
kuzaliwa upya katika ubatizo, ili wawekwe huru na nguvu za giza na kuingizwa
katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu, ambao watu wameitwa.” Watoto wanabatizwa kwa imani ya Kanisa kupitia
kwa wazazi wao na malezi ya Kikristo watakayopata tangu Kanisa la kwanza yaani
nyumbani mwa Mkristo. Ubatizo wa watoto wadogo umekuwepo tangu zamani.
Kwani tangu kale Wakristo wa Kwanza walipokuwa wanafanya zoezi hili la ubatizo
inajidhihirisha kuwa hata watoto wadogo nao walijumlishwa katika zoezi la
kubatizwa.
Sakramenti
ni tendo la Kikanisa, hivyo basi kwa busara ya Kanisa Katoliki inasisitiza
ubatizo wa Watoto. Watoto wanaozaliwa nao wapate haki hiyo ya kuitwa wana wa
Mungu kwa kutakaswa dhambi zao za asili. Wazazi
wanatambua majukumu yao ya kuwalea watoto Kikristo kwa kuwasaidia na kuwatunza
kiroho na kimwili. Kuwaongoza maisha mema ya kiuadilifu nay a upendo kwa Mungu
na jirani.
Upendo
wa Mungu siku zote hauna mipaka. Vilevile, hapendi hata mmoja wetu apotee. Kwa
sababu ya upendo wa Mungu kwa Mwanadamu Kanisa linaweza tu kuwakabidhi kwa
huruma ya Mungu, kama linavyofanya katika madhehebu ya mazishi yao. Kwani ni
kwa huruma ya Mungu na upendo wake iliyomfanya Bwana wetu Yesu Kristo; aseme
Waacheni watoto wadogo waje kwangu msiwazuie.
Hayo yanatutumainisha kwamba kuna njia fulani ya wokovu kwa ajili ya watoto
wachanga wanaokufa bila ubatizo. Na ndio maana Kanisa haliwazuii watoto kupata
Sakramenti. Kwani tunaambiwa na Mama Kanisa Katoliki kuwa Mtu yeyote ambaye
hajabatizwa ndiye pekee anayeweza kubatizwa.
Kipaimara
ni Sakramenti inayotuletea Roho Mtakatifu na mapaji yake ili kutufanya wakristo
imara na askari hodari wa Yesu Kristo hata tuweze kushuhudia imani yetu kwa
maneno na matendo.
Kipaimara hukamilisha neema ya ubatizo; ni sakrament inayomtoa Roho Mtakatifu
kwetu ili kututia mizizi ya kina kwa uthabiti zaidi Katika Kristo. Huufanya
muungano wetu na Kanisa uwe wenye nguvu zaidi, hutuhusisha kwa karibu zaidi na
utume wake na hutusaidia kuishuhudia imani kwa maneno yanayofuatana na matendo.
Wakati wa Sakramenti ya Kipaimara, paji la Roho Mtakatifu linaimarishwa ndani
mwetu na linatubidisha kuwa na moyo wa kutumikia jirani zetu na kutetea
Mafundisho ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, na kubaki Imara
bila kutetereka katika kutetea Imani yetu ya Kikristu.
Ni kwa
Sakramenti ya Kipaimara Kanisa linatuimarisha na kututaka tuipokee Imani ya
Kanisa Katoliki kiutu uzima, bila Mchezo! Na hivyo basi, kila mmoja anapaswa
aishi kama “nuru” au mwanga aweze kuangaza kati ya jirani zake na kutumia
karama kwa faida ya wote, na kuonesha amekomaa katika Ukristu na anayafanyia
kazi yale Kanisa Katoliki linayoyafundisha kwani siku zote kanisa letu katoliki
linafundisha kwa msaada wa Roho Mtakatifu ambaye ndiye “kingo” au nguzo
“msingi” na msimamizi mkuu wa shughuli zote za Kanisa katika kuinjilisha
ulimwengu wote (Rej. Papa John Paul II). Watu wote wapate kumjua Yesu Kristu.
Kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri kuwa Yesu Kristu ni Bwana.
Sakramenti
ya Kipaimara huweka chapa isiyofutika sawa na ile ya ubatizo,chapa hiyo isiyofutwa
huwekwa ndani ya Roho ya Mkristo alama ya kiroho au muhuri usiofutika, kwa
sababu hiyo sakramenti hii hupokewa mara moja tu katika maisha. Inasema, Kanisa
la Mashariki, wao ni tofauti na Kanisa letu hili la Kilatini, wao huadhimisha
Sakramenti kwa watu mara baada ya ubatizo na hufuatwa na ushirika katika
Ekaristi, mapokeo ambayo huonesha wazi umoja wa sakramenti hizi tatu za
kuingizwa katika Ukristo.
Katika
Kanisa letu hili la Kilatini, Sakramenti hii hutolewa kwa yule aliyetimiza umri
wa kuweza kutumia akili, nayo imehifadhiwa iadhimishwe, kwa kawaida na askofu
kuonesha kwa namna hiyo kwamba sakramenti hii huimarisha vifungo vya kikanisa.
Mwanafunzi wa Kipaimara, aliyetimiza umri wa kutumia akili hutakiwa kuungama
imani, awe katika hali ya neema, awe na nia ya kupokea sakramenti na kuwa
tayari kuchukua nafasi yake ya mfuasi na shahidi wa Kristo katika umoja wa
Kanisa na katika malimwengu.
Madhehebu
ya lazima ya Kipaimara ni mpako kwa Krisma takatifu katika paji la uso wa
mbatizwa (Kwa Kanisa la Mashariki: pia juu ya viungo vingine vya milango ya
fahamu), pamoja na kuwekewa mkono wa mhudumu na pamoja na maneno: Accipe signaculum doni Spiritus Sancti)
(Pokea muhuri wa paji la Roho Mtakatifu)
katika madhehebu ya kirumi; na (Signaculum
doni Spiritus Sancti) “muhuri wa
paji la Roho Mtakatifu’’)katika madhehebu ya Byzantina. Kipaimara
kinapoadhimishwa kwa kutenganishwa naUbatizo, muungano wake na Ubatizo
huoneshwa, miongoni mwa namna nyingine, kwa kurudia ahadi za ubatizo. Adhimisho
la Kipaimara wakati wa adhimisho la Ekaristi huonesha mkazo wa umoja wa
sakramenti za kuingizwa katika Ukristo.
Pengine
Sakramenti hii ya Kipaimara inaweza ikatolewa kwa mtu wakati wa hatari ya kifo
kama alikuwa bado hajapata Sakramenti hii maanake ikafuatana na Sakramenti ya
Mpako wa Wagonjwa. Sakramenti ya Kipaimara ni ishara ya ujio wa Roho Mtakatifu,
ndani ya mtu kwa hali isiyo ya kawaida. Sakramenti hiiimedhamiria kuwapa
Wakristo wa kawaida kuonja matukio yale ambayo wanafunzi wa Yesu waliyapata
siku ya Pentekoste. Ujio wa Roho Mtakatifu unamjaza mtu ari ya kukiri imani
yake hata wakati anapopata vipingamizi vyenye mateso makali vya kumwondoa
katika mkono wa Mungu, kama ilivyokuwa wakati wa dhuluma.
Sakramenti
ya Kipaimara humfanya mkristo ajazwe na Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu kama
Kanisa linavyofundisha. Mapaji saba ya Roho Mtakatifu anayopokea Mkristo katika Sakramenti ya Kipaimara
ni: i.
Hekima ii. Akili iii. Shauri iv. Nguvu
v. Elimu vi. Ibada vii. Uchaji wa Mungu
Sakramenti
ya Kipaimara inawaimarisha Wakristo kukabiliana na misukosuko ya kiimani,
,kutangaza Enjili hata katika maeneo na nchi zenye vipingamizi na ukanwaji wa
Ukristo,kupokea mateso kwa utulivu kutoka mikononi mwa Mungu, na kuishi kulingana
na wajibu wake kama mzazi, afisa, mwajiriwa, jirani au katika nafasi
nyinginezo.
Katika
Sinodi ya kwanza Jimbo Katoliki Kigoma (25 Mei, 2006 -1 Oktoba, 2011)
ilisisitizia juu ya Sakramenti ya Kipaimara kuwa ‘’Yawepo pia Mafundisho
endelevu baada ya Kipaimara hadi hatua ya kupokea sakramenti ya ndoa. Mafundisho
hayo yatawahusu pia wale waliobatizwa katika utu uzima.
Sakramenti
ya Kipaimara inampatia Mkristo muhuri, kwa
hilo wabatizwa wanaendelea na njia ya
kuingizwa Ukristo. Wanatajirishwa na paji la Roho Mtakatifu na
wanajishikamanisha na Kanisa. Wanaimarishwa katika Imani na kupaswa kuwa
mashahidi wa Kristo kwa kutangaza na kuilinda Imani kwa maneno na matendo yao.
Sakramenti
ya Kipaimara inaadhimishwa kwa kupakwa
Mafuta ya Krisma(Chrism) kwenye
paji la uso wao na kuwekewa mikono na
kwa maneno yanayotambulika kulingana na mwongozo unaotambulika na mamlaka yenye
kuonesha maadhimisho ya Sakramenti hiyo.
Krisma (Chrism) inayotumika katika adhimisho la
Sakramenti ya Kipaimara lazima yawe yamebarikiwa na Baba Askofu katika
adhimisho maalum la Misa Takatifu. Hata kama Sakramenti hii ya Kipaimara
inaadhimishwa na Padre, Mafuta ya Krisma (Chrism)
yanayotumika ni yale yaliyobarikiwa na Askofu katika adhimisho la Misa Takatifu
maalum.
Askofu katika Jimbo lake anatoa Sakramenti ya
Kipaimara kisheria hata kwa waamini wasiokuwa wa Jimbo lake, labda kama itakuwa
imeelezwa katazo kutoka kwa Askofu wao
wa Jimbo.
Ili
adhimisho la Sakramenti liadhimishwe kisheria katika Jimbo jingine,labda wawe
ni waamini wake,Askofu anahitaji apate ruhusa,walau ikiaminiwa na Askofu wa
Jimbo.
Padre
mwenye uwezo wa kuadhimisha Sakramenti
ya Kipaimara anaweza kupewa idhini ya
kutoa sakramenti ya kipaimara katika eneo
maalum alilopewa kisheria na
lenye kuwa na mpaka alihudumie, hata kwa wale wanaotoka nje ya eneo lile
aliloruhusiwa kisheria anaruhusa ya kuwapatia Sakramenti hiyo. Labda kama ikiwa
tu, kuna katazo kutoka kwa Askofu wao au Wakili wa Askofu wao (kama Vicar
General).Hawezi, hata hivyo kutoa huduma kihalari kwenye eneo jingine, labda
kama ametimiza masharti ya Sheria ya Kanisa namba 883, Ibara 3. Inayosema,
Wafuatao wanauwezo kisheria, kuadhimisha Sakramenti ya Kipaimara.
1. Katika
eneo mahususi ambalo ana uwezo wa kisheria, wale ambao wanaweza kuhudumu Sakramenti hiyo kisheria wanapata nguvu ya
kisheria na kuwa sawa na Askofu katika
adhimisho hilo la Sakramenti ya Kipaimara.
2. Kwa kuwa Padre, kwa minajiri kwamba ni
Padre(ana nguvu za Kikrelo/ Kikuhani au
kwa ruhusa aliyopewa Kisheria na Askofu Jimbo, anayebatiza au kuwapokea watu wazima katika umoja kamili
wa Kanisa Katoliki.
3.
Katika hatari ya Kifo, Paroko au Padre yeyote. Maelezo ya Ibara toka Katekisimu
bila kubadirisha maana ya sheria hii, bali kupanua ugo wa kuielezea, Kama
Mkristo yu katika hatari ya kufa, kila kuhani anaweza kumpa Kipaimara.
Walau
mimi mwenyewe mwandishi wa Kitabu hiki nimewahi kushuhudia matukio mawili
yanayojikita katika sheria hiyo. Padre aliweza kutoa sakramenti ya kipaimara
tukiwa zahanati fulani ambapo mgonjwa maisha yake yalikuwa yanaelekea kumaliza
muda wake hapa duniani. Kwa kweli Kanisa hutamani kila mmoja wa watoto wake,
hata wadogo wa mwisho, asitoke duniani hapa bila kukamilishwa na Roho Mtakatifu
kwa paji la utimilifu wa Kristo.
Inashauriwa
kwamba Sakramenti ya Kipaimara iadhimishwe Kanisani wakati wa Misa Takatifu. Hata
hivyo, kwa sababu ya haki na ya msingi, inaweza ikaadhimishwa mahali pengine
nje ya Misa na katika eneo linalofaa.
Katika
Madhehebu ya Kilatini, Mhudumu wa Kawaida wa Kipaimara ni Askofu. Ikiwa ni
lazima askofu, anaweza kuwapa mapadre idhini kutoa sakramenti ya Kipaimara.
Ingawa inafaa kutokana na maana yenyewe ya Sakramenti, aitoe askofu mwenyewe, ikikumbukwa
kwamba kwa sababu hiyo adhimisho la sakramenti ya Kipaimara, mintarafu muda, limetenganishwa
na ubatizo. Maaskofu ni waandamizi wa mitume, wao wamepokea utimilifu wa
Sakramenti ya daraja. Adhimisho la sakramenti hii linapofanywa na Maaskofu
huonyeshwa wazi wazi matokeo ya kuwaunganisha wale wanaoipokea kwa ndani na Kanisa,
na vyanzo vyake vya kitume na utume wake wa kumshuhudia Kristo.
Mwadhimishaji Rasmi wa Sakramenti ya Kipaimara ni Askofu.
Padre anaweza pia kihalari kuadhimisha sakramenti hii, ana uwezo wa kuadhimisha
kwa kigezo cha ujumla kwamba ni Mkrelo, au pale anapokuwa amepewa mamlaka
kisheria na Mamlaka yenye kuweza kutoa ruhusa hiyo yaani Askofu au Wakiri wa
Askofu.
Roho
Mtakatifu yuko macho na anafanya kazi siku zote bila kupumzika, kwani yeye ni
Roho wa Mungu. Roho huyo Mtakatifu hufanya kazi katika ulimwengu wote kwa kuwasaidia,
kuimarisha, kufariji, kufundisha, kukumbusha, kubadilisha au kufanya watu wawe
na uchaji wa Mungu kwa wote, wanaume na wanawake, wazee na vijana, watoto kwa
wakubwa. Katika Sakramenti ya ubatizo tunampokea rasmi huyo “Roho Mtakatifu” na
kwa tendo hilo tunajinyakulia hadhi ya kuitwa wana wa Mungu, kwani Mungu
ametuzaa rasmi katika Ubatizo. Tena ni kwa Ubatizo tunapokelewa rasmi kuwa
wanaushirika na Kanisa. Hivyo basi, kwamba Sakramenti ya Ubatizo ndio mlango
pekee wa kuingia rasmi katika Ushirika na Kanisa la Mungu. Na hapo hapo, ni kwa
njia ya Ubatizo Roho Mtakatifu anaingia kwa Muamini na kuanza kufariji kiroho
na kifadhila (yaani, fadhila za Kikristu, Imani, Matumaini na Mapendo).
Ekaristi takatifu ni Yesu mzima, Mungu
mtu chini ya umbo la mkate na divai. Ni sakramenti inayokamilisha hatua ya
kumwingiza mtu katika ukristo. Ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya
Kikristo. Ukweli kwamba Ekaristi Takatifu ni Yesu mzima, Mungu-mtu chini ya
umbo la mkate na divai haukubaliki kwa wengi, ingawa ukweli huu ni maneno ya
Yesu Kristo mwenyewe. Yesu mwenyewe anasema; “Mimi ndimi mkate wa uzima
ulioshuka kutoka mbinguni, aulaye mkate huu ataishi milele, na mkate nitakaotoa
mimi ni mwili wangu kwa kuupatia ulimwengu uzima.” Mtume Paulo pia anakiri uwepo wa mwili
na damu ya Kristo katika maumbo ya mkate na divai baada ya mageuzo anaposema:
“Kikombe tunachokibariki, je, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate
tunaoumega, je, si ushirika katika mwili wa Kristo? (1 Kor. 10:16).
Sakramenti ya Ekaristi takatifu
iliwekwa na Yesu Kristo mwenyewe, siku ya Alhamisi kuu pale alipokuwa akila
karamu ya mwisho pamoja na wanafunzi wake. Katika hali isiyo ya kawaida siku
hiyo Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wafuasi wake akisema:
“Twaeni mle wote; huu ndio mwili wangu, utakaotolewa kwa ajili yenu” Na baada
ya kula alichukua kikombe chenye divai, akashukuru tena, akawapa wafuasi wake
akisema; “Twaeni mnywe wote, hiki ni kikombe cha damu yangu, damu ya agano
jipya na la milele itakayomwagika kwa ajili yenu na kwa ajili ya wengi kwa
maondoleo ya dhambi; FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA MIMI.”
Tumepokea masimulizi ya kuwekwa kwa
sakramenti ya Ekaristi takatifu kutoka katika injili ndugu zote tatu na kutoka
kwa mtume Paulo. Maandalizi ya kuwekwa kwa sakramenti hii tunayapata katika
injili ya. Tangu mwanzoni kanisa limebaki aminifu
kwa amri ya Bwana: “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume na katika
ushirika na katika kuumega mkate na katika kusali…….. ilikuwa hasa siku ya
dominika, siku ya ufufuko wa Yesu, wakristo walipokutanika kuumega mkate.” Mt. Yustino shahidi mwaka 150
aliandika: “Tunachokipokea si mkate wa kawaida wala kinywaji cha kawaida; ila
kwa vile Yesu Kristo mwokozi wetu alizaliwa
kwa neno la Mungu kwa ajili ya wokovu wetu, basi chakula kilichofanywa
kwa sala ya Ekaristi iliyowekwa na Kristo mwenyewe ni kweli mwili na damu ya
Kristo.”
Mtaguso wa Trenti unatupatia ukweli
ufuatao juu ya kuwekwa kwa Ekaristi: “Bwana, akishawapenda walio wake,
aliwapenda upeo. Akijua kwamba saa yake ilishafika ya kutoka ulimwengu huu ili
kurudi kwa Baba yake, walipokuwa wakila, aliwaosha miguu yao na aliwapa amri ya
mapendo. Kusudi awaachie amana ya upendo huu, kusudi asijitenge kamwe na walio
wake, na kusudi awafanye washiriki pasaka yake, aliiweka Ekaristi kama
kumbukumbu ya kifo chake na ufufuko wake, na aliwaamuru mitume wake
waiadhimishe mpaka atakaporudi, akiwafanya makuhani wa agano jipya.”
Ni makuhani peke yao waliopewa
sakramenti ya daraja takatifu kihalali wanaweza kusimamia Ekaristi na kugeuza
mkate na divai kuwa mwili na damu ya Bwana. Makanisa mengine hawana Ekaristi
takatifu kwa sababu hawana makuhani wenye Daraja Takatifu.
Yesu Kristo aliyefanya muujiza wa
kugeuza maji kuwa divai kule Kana (Yn 2: 1-11), Yesu aliyefanya muujiza wa
kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano (Yn 6: 1-12); ndiye pia anayefanya
muujiza wa kugeuza mkate na divai kuwa mwili na damu yake kupitia mikono ya
padre. Padre alipewa mamlaka haya na Yesu mwenyewe pale alipowaambia mitume:
“Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”
Yesu alipochukua mkate na kusema huu ni
mwili wangu, halafu baadaye akachukua divai na kusema hii ni damu yangu;
wanafunzi wake waliendelea kuuona mkate na divai. Mkate na divai havikubadilika
umbo la nje kuwa nyama na damu. Hata leo hii padre anapofanya muujiza huu;
mkate na divai hugeuka kuwa mwili na damu ya Yesu kwa namna ipitayo ufahamu
wetu ingawa maumbo ya mkate na divai huendelea kuonekana.
Wapo wengi ambao wanakwazwa sana na
fundisho hili la Kristo, mbaya zaidi hata Wakatoliki wenyewe. Hali hii
haitakiwi kutushangaza kwa sababu Yesu alipotoa tangazo la kwanza la Ekaristi
takatifu wengi walikwazika na hata wanafunzi wake waligawanyika. “Neno hili ni
gumu, ni nani awezaye kulisikia?” (Yn 6: 60).
Yesu anajua kwamba fundisho hili ni gumu, lakini hawezi kubadilisha
ukweli kwa sababu watu hawaelewi. Ndiyo maana aliwaambia hata wanafunzi wake;
“Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka” (Yn 6: 67). Mkatoliki, swali hili ndilo
ambalo Yesu anakuuliza leo: “Je, unataka kuondoka kwa sababu huelewi mkate na
divai vinageukaje kuwa mwili na damu ya Kristo?”
1. Lazima mtu awe mkristo mkatoliki ambaye
yupo katika hali ya neema; maana yake asiwe katika dhambi ya mauti. “Kwa hiyo
kila aulaye mkate au kukinywea kikombe cha
Bwana kwa hali mbaya anakufuru mwili na damu ya Bwana” (1 Kor 11: 27)
2. Awe amesali sana na awe anamtamani
Yesu. Ni wale tu wanaosali na kumtamani YESU wanaweza kujibu kama alivyojibu
Petro Yesu alipouliza; “Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Petro alijibu: “Bwana,
twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele” (Yn 6: 68)
3. Pia awe ameacha chakula au kinywaji
chenye ulevi muda wa saa moja. Maji anaweza kunywa wakati wowote. Mgonjwa
anaruhusiwa kunywa dawa wakati wowote kabla ya kupokea. “Maana mwenye kula na
kunywa bila kufanya tofauti kati ya mwili wa Kristo na chakula cha kawaida
anajilia na kujinywea hukumu” (1Kor 11: 29)
ü Ekaristi hukuza muungano wetu na Kristo
na Kanisa lake. “Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu hukaa ndani yangu nami
hukaa ndanu yake” (Yn 6: 56).
ü Ekaristi Takatifu hutuondolea dhambi
nyepesi na kupunguza hatari ya kutenda dhambi ya mauti. Huwezi kuungana na
Kristo ukiwa katika hali ya dhambi; na hivi faida mojawapo ya ekaristi takatifu
kutuosha na dhambi za zamani na kutukinga na dhambi zijazo. Muhimu ni kwamba, Ekaristi takatifu haiondoi dhambi ya mauti.
Ndiyo maana tunashauriwa kuungama kwanza kabla ya kupokea.
ü Ekaristi takatifu huilinda na kuongeza
neema ya utakaso, tuliyopokea katika ubatizo na kipaimara iliyo uzima wa roho
zetu.
ü Ekaristi Takatifu inadumisha na
kustawisha mapendo ambayo katika maisha ya kila siku yanaelekea kudhoofika. Kwa
mapendo haya ekaristi takatifu inaunda umoja wa kanisa. Ekaristi Takatifu
inatufanya tuwe mwili mmoja katika Kristo.
ü Kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu,
tunatiwa nguvu na kuongezewa hamu ya kuurithi uzima wa milele. “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho” (Yn
6: 54)
Katika
adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, wakati wa Mageuzo waadhimishaji, Padre au
Askofu, humwomba Mungu amtume Roho Mtakatifu ili ageuze mkate kuwa mwili na
Divai kuwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.Si kwamba kabla ya Mageuzo hayo, Roho
Mtakatifu anakuwa mbali, hapana. Ila tu, ni katika Mageuzo na kwa namna ya
pekee Roho Mtakatifu anaombwa azishukie dhabihu hizo za Mkate na Divai lililo
tunda la Mzabibu, ambalo halijachanganywa na chochote isipokuwa yale maji Padre
anapochanganya mwenyewe altareni. Ili viwe Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo. Na kitendo hicho tunakiita sasa Epiklesis.
Epiklesis, Roho Mtakatifu
anaombwa ashuke katika vipaji vya mkate na divai, kuzigeuza kuwa Mwili na Damu
ya Kristo. Kwa uwezo wake ubadilishao
hufanya fumbo la Kristo litukie hapo linapoadhimishwa na katika wakati huo.
Kuhani anaitandaza mikono yake juu ya vipaji kuonesha mpaji wa uzima Roho wa
Mungu anamiminwa juu ya mkate na divai ili kuvigeuza kuwa Mwili na Damu ya
Kristo. Wakoselebranti (Mapadre walioshiriki Adhimisho la Misa Takatifu) nao
wanatandaza mikono yao kama kuhani kiongozi, isipokuwa kama wameshika kitabu
hutandaza mkono mmoja.
Roho
Mtakatifu, Katika maadhimisho ya Sakramenti nyingine licha ya
Upatanisho.Tukifahamu kuwa, Roho Mtakatifu ndiye Mtendaji Mkuu katika
Maadhimisho ya Sakramenti zote.Kwa namna ya pekee anafanya kazi katika
Adhimisho la Misa Takatifu inayoadhimishwa na kuhani (Padre, Askofu, Papa, Baba
Mtakatifu naye ni Askofu wa Jimbo la Roma). Ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
dhabihu za Mkate na divai, zinageuka kuwa mwili na damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo.
Padre
anamsihi Mwenyezi Mungu amtume Roho Mtakatifu ili dhabihu za mkate na divai
viweze kuwa mwili kabisa wa Yesu na danmu azizi ya Yesu, Ekaristi Takatifu,
inapatikana katika Misa Takatifu. Na kuhani ndiye mwenye ofisi hiyo ya
kuadhimisha fumbo zima la Ekaristi Takatifu, akijifahamu kuwa yeye ni chombo
kinachotumika kuwaunganisha Waamini na Mungu kwa tendo la adhimisho la Misa
Takatifu.
Katika
adhimisho la Misa Takatifu, wakati wa Mageuzo, Padre anamwomba Mwenyezi Mungu
kwa unyenyekevu mkuu Roho Mtakatifu aweze kubadili maumbo ya mkate na divai
viweze kugeuka kuwa Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, anasema “Basi ee
Bwana tunakusihi umtume Roho wako Mtakatifu dhabihu hizi umtume Roho wako
Mtakatifu aweze kugeuza mkate na divai viwe mwili na damu ya Bwana wetu Kristu
’’.
Roho
Mtakatifu anatia mioyoni mwa Familia ya Mungu juhudi ya kutangaza Injili.Yeye
ndiye mwinjilishaji mkuu katika harakati zetu za kuinjilisha ulimwengu.Ni
pamoja na kuhimiza Sala katika familia na katika jumuia ndogo ndogo za
Kikristo. Roho Mtakatifu kwa sala zetu tukimwomba, Ulimwengu hutakatifuzwa,
Baba Mtakatifu, Maaskofu, Mapadri, Watawa wa Kike na Wakiume, Wanafamilia na
Vijana wetu. Roho Mtakatifu hutakasa huwanyunyizia makundi mbalimbali ya Vyama
vya Kitume wakijiweka katika Sala na usikivu wa NENO la Mungu (Maandiko
Matakatifu ya Biblia). Roho Mtakatifu huwezesha kupata kila aina ya Neema na Baraka
wanazohitaji katika maisha yao.
Kwa upande wa wale wanaopokea Sakramenti ya
Ekaristi Takatifu waliobatizwa utotoni wanapaswa watayarishwe na wapewe
sakramenti ya Ekaristi Takatifu wakiwa wana jua vema ukuu wa Sakramenti hii.
Kwamba kweli wanampokea Yesu Kristo mzima katika maumbo ya Mkate na divai. Na
baada ya Komonio ni vema yawepo mafundisho endelevu hadi watakapofuata
mafundisho ya Kipaimara.
Baada ya mageuzo, mkate na divai
vinakuwa kweli mwili na damu ya Yesu, na katika kila kipande cha HOSTIA mnakuwa
na Yesu kristo mzima, Mungu-mtu. Mkate na divai hugeuka kuwa mwili na damu ya
Yesu hata kama padre anayefanya mageuzo hayo ana dhambi ya mauti kwa sababu
anayefanya mageuzo ni Yesu mwenyewe.
Kwa kuwa Kristo mwenyewe yumo katika
sakramenti ya Ekaristi takatifu ni lazima kumheshimu kwa ibada ya kuabudu. Na
hivi ni wajibu wa wakristo kuabudu sakramenti kuu hii kwani hicho ndicho kipimo
cha shukrani na ishara ya mapendo yetu kwa mkombozi wetu.
“Yapo makosa mengi sana duniani, ukikosea wa kuoa au
wakuolewa naye. Hilo ni pigo katika Maisha yako yote. Na kila mwanajamii
atakaye kuona ukiwa na simanzi za fujo katika ndoa yenu atatikisa kichwa kwa
kukusikitikia. (Inatoka kwenye Misemo ya Hekima kwa kabila ''Wasukuma'') Na
hakuna mtu mwenye mapenzi mema katika jamii angefurahia kuona wanandoa majirani
wanaishi kwa kukimbizana na kuishi maisha ya vurugu siku zote.’’ Kumbe
ni vema wachumba wachunguzane kwa kipindi kirefu kuhusu tabia zao na na sio
uchumba unaofanywa baada ya kukutana kwenye basi au ‘’treni ‘’(gari moshi) au
kwenye kituo cha mabasi.
Ni
busara ya Kanisa Katoliki kuzidi kusisitiza siku zote mpaka leo kuwa wakatoliki
wanapotaka kuweka uchumba; wasali sana, ili Mungu awasaidie kupata wachumba
wema. Kanisa linaongezea kutoa ushauri kwa wanaotaka kuoa; Waulize shauri kwa
wakubwa wao, kama tunavyotafakarishwa na neno la Mungu kwa maonyo,
likisema: ‘Mwanangu usifanye kitu bila shauri;
hivyo hutakuwa na kujuta baada ya kufanya.’
Kwa
ustawi na uimara wa ndoa, Kanisa Katoliki linamuasa mkatoliki anapotaka kuoa au
kuolewa achague mchumba aliye pia mkatoliki au atakayekuwa mkatoliki baadaye.
Wakati wa uchumba wa uchumba watunze usafi wa moyo, wapokee Sakramenti za
Kitubio na Ekaristi takatifu mara nyingi. Sakramenti ya ndoa yawalazimu watu wa
ndoa: kuishi uimara wa ndoa yaani kukaa
pamoja kwa uaminifu mpaka kufa, kupendana na kusaidiana, kupenda kupata watoto,
kuwalea vyema na kuwaongoza kwa Mungu.
Hivyo
basi ,ndoa haiwezi kufunguliwa wala na Kanisa wala na Serikali ila kwa kufa tu, kwani ndoa
Katoliki ni Sakramenti na hivyo basi, ndoa naiheshimiwe.Madhara ya
‘’mparanganyiko’’ wa wanandoa kisaikolojia huwaathiri mpaka watoto na hata
wajukuu pia.
Mungu
mwenyewe ndiye asili ya Ndoa . Hivyo basi ndoa yatoka kwa Mungu.Kama ndoa inatoka kwa Mungu. Kwanini sasa
isiheshimiwe? Katika maandiko Matakatifu tunasoma, Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia
msaidizi wa kumfaa (Rej. Mw 2:18). Na
tunasoma tena kuwa ni kutokana na
ubavu wa mwanamume hapo mwanamke alipatikana baada ya Mungu kumpa Mwanaume
usingizi mzito tunasoma “Basi, Mwenyezi
Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito na alipokuwa usingizini, akamtwaa
ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama. Na huo ubavu Mwenyezi
Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke akamleta kwa huyo
mwanamume. Ndipo huyo mwanamume akasema “Naam ! Huyu ni mfupa kutoka mifupa
yangu na nyama kutoka nyama yangu. “Huyu ataitwa “Mwanamke’’ kwa sababu ametolewa
katika Mwanamume’’. Ndiyo maana mwanamume humwacha Baba yake na Mama yake,
akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja (Rej. Mw 2:21-24).
Mungu
anaupinga “Ulimbukeni” wa watu
wanaojiita wanakwenda na wakati ‘’ Kila
mtu atakaye mwacha mkewe isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine
azini, naye amwoaye yule aliyeachwa azini (Rej.
Mt 19:9). Sababu iliyotolewa na Yesu ya kuachana kwa sababu ya Uasherati
iliongelewa katika mazingira ya mwandishi alimaanisha kuwa kwa wale wanaooana
huku ni ndugu wa damu mfano, Kaka na dada au Baba na bintiye hata kama
walifunga ndoa Kanisani kwa kujificha au kumdanganya Padre au Shemas, hapa
tunaiita ni “batili’’ kumbe sasa hata haikuwa ndoa kwani hakuna ndoa baina ya
ndugu wa damu.
Kumbe basi, ndugu wa damu iwe kwa uhusiano wa kisheria au wa kiasili wanazuiwa
na Kanisa kufunga ndoa.Na hiyo kwa kweli ni Sheria ya Mungu na hakuna mamlaka
yoyote chini ya jua yanayoweza kuipindua wala kuibadilisha.
Na
matokeo yake wanajikuta wamo katika maisha ya kuishi kwa mikataba na baadaye
wanabaki mitaani wana wayawaya bila kuwa na mbele wala nyuma. Na watoto “wanapigika’’
kwa kukosa malezi ya wazazi wao.
Wakati
mwingine inaitwa Sakramenti ya Huruma ya Mungu au ya Kujipatanisha na Mungu. Na hivyo Roho Mtakatifu ndiye
huzikumbusha na kuzisuta dhamiri zetu pale tunapokuwa tumemkosea Mungu, pale
tunapovunja amri zake Mwenyezi Mungu. Ni Roho Mtakatifu anayetupatia mguso na
msukumo wa kwenda kwenye Sakramenti ya Upatanisho (Maungamo na Toba ya kweli).
Tujongee
kwenye kiti cha Huruma (Kwenye Maungamo) bila woga wowote ili tutakaswe, na
kuondolewa dhambi zetu.Kwani dhambi ni adui wa Roho wa Mungu. Tunapotenda
dhambi tunamfukuza Roho Mtakatifu, Kwani Miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu
kama Mtume Paulo anavyosema. Pia kwa kujisomea unaweza kufunua Biblia Takatifu
Tuishi tukiongozwa na Maisha ya Roho wa Mungu
(Gal 5:25 , 2:17,3:13 ; 1Kor 15:45; Rum 8:2)
Tumkimbilie
Kristo, kwa kupitia Mtumishi wake Padre, aliyekuhani na Kristo Mwingine
atuondolee dhambi zetu, pale tunapojikuta tumekurupusha amri za Mungu. Kwa
daraja ya Upadre, Padre anapewa mamlaka ya kuondolea dhambi kwa wale
wanaomkimbilia ili wajipatie rehema na utakatifu kwa Mungu. Kujitakasa kiroho
kwa Sakramenti. Tuzingatie sana kuishi tukiwa na Roho safi na dhamiri
zisizokuwa na “makunyanzi.’’
Sakramenti
ya Kitubio au Upatanisho ni muhimu sana katika maisha yetu. Yesu mfufuka
aliwaambia mitume wake “Amani kwenu’’ kama vile Baba alivyonituma mimi nami
nawatuma ninyi. Alipokwisha sema hayo; Akawavuvia na Kuwaambia ‘’ Pokeeni Roho
Mtakatifu; Mkiwaondolea watu dhambi zao wataondolewa, msipowaondolea,
hawataondolewa.
Hiyo ni moja ya kazi muhimu sana za Roho Mtakatifu katika Kanisa. Na Mkatoliki
yeyote yule anayedharau Sakramenti Takatifu yoyote, ajue yuko mbioni kutengwa
na kanisa au ameshajitenga yeye mwenyewe moja kwa moja kwa kujua au
kutojua.Angalisho kwa vyama vya Kitume na Vikundi vya Sala tuwe macho,
tuheshimu Sakramenti zote Saba. Baada ya kuona kuwa Sakramenti ya Kitubio
haipokelewi na wengi kuna haja kubwa sana iwepo
nia na mpango madhubuti wa
kuifanya sakramenti hii ipendwe na waamini wapewe upya Katekesi,
na waone umuhimu wake katika maisha.
Mpako
wa wagonjwa ni sakramenti inayomtia nguvu Mkristo aweze kuyapokea maumivu na
shida katika magonjwa yake akimtumainia Yesu Kristo aliye Mwokozi
wetu.Sakramenti ya mpako wa wagonjwa huweza kumponya Mkristo Kiroho zaidi na
kimwili pia.
Ni kwa Sakramenti ya mpako wa Wagonjwa na
Sala za Makuhani, kanisa lote huwakabidhi
wagonjwa kwa Bwana aliyeteswa na
kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Na kwa hakika lawahimiza wajiunge kwa hiari
na Mateso na Kifo cha Kristo ili kutoa mchango wao kwa manufaa ya Taifa la
Mungu.
Ni
Mungu katika Utatu Mtakatifu mwenye kumponya mgonjwa kiroho na kimwili. Roho
Mtakatifu humpatia ujasiri mgonjwa aweze kuyapokea maumivu kwa imani katika
kumtegemea Mungu mwenyewe aliye asili ya afya na uhai wetu kwa ujumla. Yesu
Kristo aliyepata mateso makali msalabani haachi kumfariji mgonjwa.Pia
Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni ishara ya matumaini, kumwachia Mungu aweze
kutenda kadiri ya Mapenzi yake. Mkristo anaalikwa na Mama Kanisa kuwa na imani,
kusadiki. Kristo mwenyewe aliwataka wagonjwa wasadiki kwamba nguvu ya Mungu
inatenda kazi. Kristo ni Mganga aliweza kutumia ishara mbalimbali katika
kuponya wagonjwa kama vile mate na kuwekea mikono, tope na kuosha.
Ndio
maana tunaambiwa kuwa Yesu Kristo alipokuwa kwenye utume wagonjwa walimtafuta
angalau wamshike hata upindo wa vazi lake. Tunasoma pia, kwa nguvu ya ufufuko
wa Yesu Kristo, wagonjwa njiani walitamani hata kivuri cha mtume Petro
kiwafikie tu wapate kupona. Waliamini kuwa wangeponywa na Mtume Petro, kwani
alikuwa ameshafufua mfu. Hivyo hivyo ni katika Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa
Kristo anaendelea kutugusa. Ni wajibu wa Wakristo wote kuwapoza wagonjwa,
kuwafariji, kuwasaidia kwa hali na mali.
Ninaposema
Daraja Takatifu (Holy Orders), nina maana ya yale Madaraja matatu; yaani Daraja
ya Ushemas, Daraja ya Upadre na Daraja ya Uaskofu. Kwa namna nyingine Daraja ya
Ushemas inaitwa Daraja ya tatu ya Ukasisi. Pia Daraja ya Upadre inaitwa Daraja
ya pili ya Ukasisi. Na Daraja ya Uaskofu inaitwa Daraja ya kwanza ya Ukasisi. Daraja
hii ya kwanza ya Ukasisi ndiyo inayompa Askofu kuwa na ule uwezo na nguvu kuu
ya Upadre (A Bishop has that fullness of Priesthood) tofauti na madaraja
mengine mawili ya Ushemas na Upadre. Kwani Askofu ndiye Jimbo na ndiye mwenye
mamlaka yote katika Jimbo husika. Mashemas na Mapdre hawa ni wandamizi wa
Askofu, wapo kumwakilisha na kumsaidia kazi za kitume popote pale anapotamani
kuwepo; lakini anakuwepo kwa uwakilishi wa watu hao.
Historia ya Daraja Takatifu na uhtaji wake
Katika
Kanuni ya Imani, tunakutana na sehemu inayosema “Roho Mtakatifu aliyenena kwa
vinywa vya Manabii’’ ni ushahidi tosha kabisa na hatuna shaka, hii ndiyo ungamo
la Imani la Kanisa Katoliki. Roho Mtakatifu alitenda kazi ndani ya Manabii katika
Historia nzima ya Wokovu wa mwanadamu. Katika Agano la Kale tunakutana na uvuvio
wa Roho Mtakatifu kwa Manabii na hilo tunaliona kuanzia Nabii Musa.
“Kuhani
atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli na atasamehewa kwa
sababu si kosa walilokusudia na wameleta
sadaka yao ya kuteketeza kwa Mwenyezi Mungu
kama dhabihu na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya kosa lao.’’
Pia, “Naye
Mose akamwomba Mwenyezi Mungu, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu uliye asili ya Uhai
wote, nakuomba umteue mtu wa kusimamia
jumuiya hii, Ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao
zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji.”
Tunaona
jinsi Nabii Mose alivyomwomba Mwenyezi Mungu
amteue mtu wa kuwaongoza taifa la
Waana wa Israeli naye ni Yoshua mwana wa Nuni, tunaambiwa Yoshua alikuwa
mtu mwenye Roho nzuri,aliyepaswa
kuwekewa mikono na asimamishwe mbele ya Kuhani Eleazari.Tunazidi kuambiwa kuwa kuhani Eleazari alimwekea mikono kichwani
Yoshua na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi Mungu.
Ishara
ya Kuhani Eleazari ya kumwekea mkono juu kichwani mwa Yoshua inamaanisha
kumwomba Roho Mtakatifu amshukie Yoshua aweze kufanikisha vema na salama kazi
ya Mungu ya kuwaongoza Waisraeli katika safari ya kuelekea nchi ya ahadi. Madhehebu
haya ya kuwawekea Mikono kichwani yamebaki katika Liturujia ya kuwaweka wakfu
Makuhani wa Mungu, yaani katika adhimisho la Misa ya kumweka wakfu Shemas,
Padre na Askofu. Kwa kumwekea mikono ni kumwomba Roho Mtakatifu aweze
kumshushia mapaji yake katika huduma ya Ushemasi, Upadre au Uaskofu. Roho
Mtakatifu anamwongoza “Mtoa huduma wa Mungu” (Kuhani) aweze kulihudumia kanisa
kulingana na Matakwa ya Mwenyezi Mungu kama vile Yoshua alivyopaswa kulitumikia
vema taifa teule la Mungu (Waisraeli).
Basi
Roho ya Mwenyezi Mungu ikamjia Othnieli, naye akawa mwamuzi wa Waisraeli. Roho
wa Mungu alikuwa naye. Othniel alikuwa ni jibu la ombi la Waisraeli baada ya
Mungu kuuficha uso wake mbele ya Waisraeli kwani Waisraeli walikengeuka na
kuirudia miungu ya uongo mabaali na maashira.
Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi Mungu wakamsahau Mwenyezi Mungu,
Mungu wao,wakaabudu Mabaali na Maashera (miungu ya kipagani).
Basi
hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli … Hata hivyo agano la Kale bado linaonesha nguvu ya Roho
Mtakatifu, Kitabu cha Kwanza cha Samweli (1Sam
10:6) ,ambapo tunasoma ‘’Roho ya
Mwenyezi – Mungu itakujia kwa nguvu ,nawe utaanza kutabiri pamoja nao na
kugeuka kuwa mtu mwingine, Hapa Samweli anaendelea kupata mahusia na maneno
yenye kumpatia nguvu katika kutekeleza yale Bwana Mungu aliyomwamuru, katika
Mstari wa Sura hiyo ya 10, Samweli anaelezwa kuwa Wakati mambo hayo
yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja
nawe. Ama kweli haya ni maneno ya
Faraja na yenye kutia nguvu kwa Mhudumu wa kazi zimuhusuyo Mungu.
Ni neno
lenye kuonesha tumaini na Moyo Mkuu ambamo Roho Mtakatikifu aliye Mungu hutoa
paji lake la Faraja. Roho huyu Mtakatifu mwezeshaji wa shughuri zote za
Kumuhubiri Yesu Kristu. Kazi za Roho Mtakatifu zinajifunua katika kuonesha
nguvu ya KiMungu katika maisha ya mwanadamu.
“Nawaandikia
ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina
lake. Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu
mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda Yule mwovu.
Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba. Nimewaandikia ninyi,
akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi,
vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi
mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala
mambo yaliyomo katika dunia. Mtu
akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani,
yaani, tama ya mwili, na tama ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba,
bali vyatokana na dunia”
Lakini vilevile maisha yetu yananena juu yetu kuwa, “ hao ni wa dunia;
kwa hiyo wanena ya ya dunia na dunia huwasikia.”
Naomba tutafakari namna mbili tu ambazo
ni miongoni mwa milango ya fahamu mitano (5) ya mwanadamu. Nayo ni Sikio na
Macho, ambazo zinafanya kazi kwa ukaribu sana. Hivyo ni milango ya fahamu
inayotegemeana kwa lugha nyingine. Upofu unakuondoa kwa vitu lakini kuwa kiziwi
kunakuondoa kwa watu. Hausikii ushauri wao, nasaha zao, onyo, maneno ya kutia
moyo na pongezi. Usipoweza kusikia utasahau na namna ya kuongea. Padre wa
Kanisa Katoliki anapombatiza mtoto mdogo anamgusa mtoto masikio na kinywa kwa
kidole gumba akisema, “Bwana Yesu, aliyewafanya viziwi wasikie, na bubu waseme,
akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya
kikristu, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba”
Wapendwa ndugu zangu katika Kristu,
vijana na walezi na kwa namna ya pekee wewe msomaji au wasomaji wa kitabu hiki.
Napenda nitafakari nanyi juu ya jicho, tukiongozwa na masomo ya Maandiko
Matakatifu; Yoshua Bin Sira 17:1,6-14 na Matayo 6:22-23. Jicho ni mojawapo ya njia
za fahamu zilizo kwenye kichwa. Kichwa ni sehemu yenye viungo kama ubongo,
wenye kazi nyingi kama vile kufikiri, njia za fahamu kama vile jicho, mdomo,
masikio, pua na sehemu ndogo ya ngozi. Haya yote yameumbwa na Mungu na ni zawadi
kama tulivyosikia kwenye somo la kwanza. Katika kutenda kwake jicho na sehemu nyingine
za mwili husika- husaidiana. Kichwa ni injini ya mwili. Mt. Lucia anatufundisha
akisema “jicho ni moyo wa nje wa mwili wetu linaloonyesha maisha ya ndani ya kila
mmoja wetu. Limefanywa kwa ajili ya mwanga
ili liweze kuona, kutafakari na kumpenda Mungu na viumbe katika ukweli na upendo,
katika uzuri na usafi wa moyo, katika haki na utakatifu. Tulilinde na maovu yote
ya kiroho na kimwili.”
Ø Jicho
ni moyo wa nje wa mwili wetu; moyo ulioko ndani ya mtu hufanya kazi ya kusukuma
damu, ni pampu ya damu. Jicho
kama moyo wa nje, hutusukuma kutenda tuyaonayo. Moyo hutamani kutenda, kumiliki
na kutawala. Jicho pia kama moyo wa nje wa mwili husukuma mwili kutamani na kutenda.
Jicho likiona kitu kizuri mfano gari zuri, nyumba nzuri au binti mzuri au picha
yake nzuri kwenye mtandao au studio, tembea yake na mitikiso ya mwili, mwili mzima
unapagawa, unahemka au binti akiona mvulana mzuri, mwili wake mzima unasisimka,
unatamani. Siku hizi tamaa ziko nyingi mno, tamaa ni maisha ya ndani ya mtu-kiumbe.
Ø Jicho
linaonyesha maisha ya ndani ya kila mmoja. Jicho huonyesha wema, uzuri, uso wa kimalaika wa mtu pamoja
na ubaya, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi, upumbavu Mk. 7:21, Mt.
Paulo naongezea katika waraka wake kwa Wagalatia 5:19, kuabudu sanamu, uchawi,
uadui, ugomvi, mabishano, mafarakano, hususda, ulevi, ulafi, kijicho; haya yote
ni matendo ya giza lakini…
Ø Jicho
limefanywa kwa ajili ya mwanga.
Yesu aliwaambia Mafarisayo, jicho ni taa ya mwili (Mt. 6:22-23). Basi, kama jicho
lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Lakini, ikiwa jicho ni bovu,
mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga uliona ndani yako ni giza, basi hilo ni giza,,
na hilo ni giza la kutosha mno. Giza huwa linapotosha (povusha).
Ø Jicho
limefanywa ili kuona. Kama
vile tulivyotaja hapo juu vipo ndani yako basi kwako mwanga ni giza ni giza na kama
kwako mwanga ni giza, basi giza ulilonalo ni giza hasa. Ni giza kweli kweli, ni
giza topea, pitahulka. Moyo huo wa nje wa mwili wetu umekufa. Jicho halioni.
Linafunguka mpaka mwisho lakini halioni. Nabii yuko sahihi wana macho lakini hawaoni.
Mt. Yohane anatueleza maisha halisi, juu ya giza, wale waliokaa katika giza la
uvuli wa mauti, matendo ya giza tumeyataja juu.
Ø Jicho
limefanywa ili kutafakari.
Sasa wangapi tuna tumia macho yetu kupitisha vitu safi vya kutafakari? Kwenye mtandao
mnachukua vitu gani? Jicho linapendelea kuangalia nini na kusoma nini? Jicho limefanywa
kwa ajili ya uzuri na usafi wa moyo (Mt. Lucia ansema). Asilmia 75 ya habari na
elimu tuliyonayo hutokana na kuona kwa jicho. Kwa jicho tunaona na baadae tunatafakari
hekima na upumbafu, maarifa na ujinga, uzuri na ubaya, Mungu na shetani, ya mwili
na kiroho. Lakini jicho limefanywa ili tumtafakari Mungu na si ubatili.
Ø Jicho
limefanya ili kumpenda Mungu.
Hivyo mambo ya kiroho, kimbingu na kimungu, hekima ya matendo ya watu, hayo yote
ndiyo yanayotupatia heshima, uadilifu na
utakatifu. Na si mambo ya mwili, kidunia na ya binafsi wa ubinadamu wetu.
Ø Jicho
limefanywa ili kuvipenda viumbe.
Kama vile anga, nyota, sayari, mwezi, jua, bahari, milima, mabonde, mito, miti,
wanyama, wadudu, ndege, vifaa vya sayansi, matokeo ya teknolojia, haya yote ni kweli
za maisha. Kutokana na maajabu haya tuzidi kumpenda Mungu, na si kuviharibu.
Askari anaweza kupofukia vitani lakini wanaokwendahuko wana macho wote,
wanaharibu kila kitu… jicho limefanywa kwa ajili ya ukweli na upendo, haki na utakatifu
(Mt. Lucia) ili kwa akili na njia zote za fahamu zilizo kichwani (mdomo, pua,
ngozi na masikio, tungekuwa na muda tungetafakari haya) tuweze kuwa watu wa ukweli
na upendo, haki na utakatifu.
Imani ni jicho la roho. Basi tunzeni
macho yenu, mboni za macho yenu, kwa kuwa jicho ni kwa ajili ya Mungu. Na Mt.
Lucia anatundisha “tulilinde jicho na maovu yote ya kiroho na kimwili.”
Kwa kutambua na kujua namna sikio
linavyoweza kupata kitu kupitia sauti, kunahusianishwa zaidi na Akili ambapo
baada ya pinna kukusanya yale mawimbi ya sauti kutoka kila kona ya dunia ndipo
hapo mawimbi hayo yanatumwa kwenye ubongo kwa ajili ya kutolewa ripoti ya taarifa
ambayo hutujia na kutuelewesha nini kilikuwa kikiongelewa. Kwa kuwa yeye aliyetuumba
ni mweza vivyohivyo ukijaribu kutafakari juu ya mchakato unavyofanyika mpata ujumbe
kutumwa inafanyika haraka sana kwa uwezo aliotukirimia huyu mwumba wetu. Mafundisho haya ni yamejikita katika mlalo kulingana na kile alichotoa Fr.
Faustin Kamugisha tarehe 7/09/2012, pamoja na mengine mengi kulingana na uzoefu
wangu.
Kiziwi
hafokewi. Ni msemo wa
kiafrika. Mtu aliye na matatizo ya kusikia hatakuelewa ukimfokea. Tukumbuke
kuwa licha ya sikio la kimwili kuna masikio ya kiroho au ya moyo. Ni katika
msingi wa masikio ya moyo tunasema, asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Si suala
la kusikia la masikio ya kimwili bali kusikiliza na kuzingatia na kuyafanyia
kazi. Kuna mwanaume aliyekuwa anasoma gazeti akumuomba amusomee mke wake
utafiti uliofanywa. Mwanaume akasoma, “Utafiti umegundua kuwa wanawake
wanaongea maneno mengi mara mbili ya wanaume.” Aliposema hivyo mke wake asema,
“ Tunasema meneno mengi kwa vile tukisema mara ya kwanza hamsikii.” Hapo mme
wake akauliza, “Hivi unasemaje?” Mwanamme huyo alifokewa na mke wake. Ni katika
msingi huu tunasema, kiziwi hafokewi. Kumfokea mtu huyu hakutamsaidia.
Kwa kurejea Mithali 20:12 anatujuza
“Sikio lisikialo na jicho lionalo, Bwana ndiye aliyeyafanya yote mawili”. Hivyo
kwa utambuzi huo kwamba limeumbwa na Mungu mwenyewe akiwa na nia nzuri kabisa kwetu
sisi, hatunabudi kulitumia vema kama alivyonuia tulitumie yaani katika matumizi
sahihi kabisa. Na kama tusipofanya hivyo basi tunakuwa tunakiuka maadili na hivyo
kutufanya au kutupelekea katika kutenda dhambi. Ndipo hapo linatimia lile neno
la wahenga lisemalo “Sikio la kufa halisikii dawa.” Nasi vivyohivyo kama tutakaa
na kusikiliza kila jambo linalonenwa pengine juu yetu, tutakuwa tunauendekeza upagani,
ambapo tutaanza kuwa watu wa chuki, fitina, na wazuri wakusengenya wenzetu yaani
kwa kuwa mashushushutu.
Kwa kuwa tunajua na kutambua mwili ni mmoja
tu ,bali una viungo vingi na kila kimoja na kazi yake binafsi. Vivyohivyo kama ilivyo
kichwa kimoja ila kina viungo mbalimbali na vilivyotofautitofauti kama vile
Sikio=kusikia au kusikiliza, Jicho=kuona, Pua=kunusa, Ulimi=kulamba na Ngozi
=kuhisi. Lakini sikio linahusiana sana na mdomo ambao injini yake ni ulimi katika
kutenda na kufanyakazi ya mawasiliano kwa vitendo.
Tukirejea Wagalatia 5:19-21 tunaona matendo
yaliyo ya kimwili ambayo yanasababishwa zaidi na viungo vyetu vya mwili kama yalivyotajwa
katika andiko hilo. Kwa mfano, ugomvi, fitina au uzushi, hasira ambavyo tunavipa
nafasi kubwa ya kutenda na kufanyika kupitia sikio baada ya kusikia. Hapo jibu
lake siku zote linajibiwa kwa uharaka na mdomo kupitia ulimi bila kusita, na hivyo
kutufanya sisi kugeuka kuwa kama wanyama wengine kupitia matendo yetu yanavyo kuwa
yakienenda kama shetani, maana kama tunaweza kusikia na mara moja tukakifanyia kazi
bila kufikiri mara mbili wakati tumepewa utashi wa kung’amua lipi jema na lipi baya.
Na kama Yoshua Bini Sira 18:19 anatuasa kuwa tujifunze kabla ya kunena, na siyo
kila tulisikialo linatupasa kulitolea majibu kwa kunena laa! hasha, keti utafakari.
Kupitia tuyasikiayo, mdomo umekuwa kimbelembele
kunena tu, na mwisho kujaza chuki baina yetu. Kikubwa basi lazima tufike mahali
tuifunge au kuituliza midomo yetu. Hapo kama ilivyo “si kila avumaye baharini ni
papa laa! Hasha ana wengine wamo”. Vivyohivyo si kila tulisikialo tuliamini na kulipa
nafasi au uzito kwa asilimia zote 100%, ndiyo maana hata kiwango cha mashine kufanyakazi
hakifikii 100%. Tukirejea YBS 33:19 anatuasa kusikiliza na kutegea masikio yetu
kwa makini ili tuelewe na kuweza kuchanganua maneno hayo au maana ya sauti hizo.
Mk. 7: 33-37 juu ya EFATHA Na mwisho kabisa ndiyo maana hata katika ubatizo
wa watu kwenye kipengele cha EFETA kwa kuanza na maneno yafuatayo ”BwanaYesu, aliyewafanya
viziwi wasikie, na Bubu waseme akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake,
nakuungama kwa mdomo imani ya kikristu, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba. Amina.
Tunaambiwa kwa kutajwa jina Mfano
Flavian EFETA sikia, funguka. Yaani Padre anafanya Ishara ya msalaba katika
sikio na kumalizia kwenye mdomo, ikimaanisha kwa kile tukisikiacho tukapate kukinena
kwa midomo yetu ilimradi kiwe cha kumtukuza Mungu. Kwahiyo ndugu zangu tujitahidi kuitumia midomo
yetu vema, pia kuwa makini kwa sauti zote tusikiazo ili kabla ya kuamua chochote
tukifikirie mara mbili kwa kuangalia pande zote za shilingi yaani Upande wa faida
na hasara.
kuna kutia vidole masikioni. Alimgusa. Mara masikio yake yakafunguka.....(rej. Mk 7:35) Ambaye
hasikii mguse kwa neno alopendelea kwanza. Mtu hasikilizi ujumbe sababu ujumbe
haujamgusa. Mguse kwa mambo ambayo kwake ni kama ngozi yake. Ni sehemu yake.
Kwa mfugaji Yesu ni mchungaji. Ni malisho. Kupitia hapo mfugaji ataanza
kukusikiliza. Kwa hakimu na jaji Yesu ni mshauri wa ajabu. Kwa fundi seremala
Yesu ni mlango. Ni katika msingi huo ili wenye shida ya maji wakusikilize
lazima uwaguse kwa kuongelea shida ya maji na kutafuta uvumbuzi. Ujumbe kuhusu
watoto au mwanaume utamfanya mwanamke aanze kusikiliza.
“Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi wakamsihi amwekee mikono.
Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema
mate, akamgusa ulimi akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia Efatha, maana
yake, funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea,
akasema vizuri” (Marko 7:32-35). Kuna
matendo saba katika kumtibu kiziwi na bubu. (1) Akamtenga na watu (2) Akatia
vidole vyake masikioni (3) Akatema mate (4) Akamgusa ulimi (5) akatazama juu
mbinguni (6) Akaugua (7) akamwambia Efatha. Kwanza ni kutengwa na watu. Watu wanaweza kumfanya
mtu asisikilize. Kuna saikolojia ya umati au mkutano inaitwa kwa Kiingereza
“mob psychology.” Wakati mwingine maneno anayopata mwanamke toka saluni
yanaweza kumfanya asimsikilize mume wake. Maneno anayopata mwanaume toka
kilabuni yanaweza kumfanya asimsikilize mke wake. Lazima tuachane na marafiki
wabaya wenye ushauru mbaya.
Tatu akatema mate. Mate ni ya kulainisha. Ambaye hasikilizi anahitaji
jambo la kumlainisha. Linaweza kuwa neno zuri au neno la kutia matumaini, au
kumsikiliza kwa makini akiongea. Kumsikiliza mtu kwa makini ni kumlainisha. Lenin aliweza kusikiliza kwa makini
kiasi cha kumchokesha mzungumzaji. Usiseme fulani hanisikilizi nawe msikilize.
Nne ni kumgusa mtu ulimi. Mpe mtu
ambaye anafanya makosa kwa kutumia ulimi utaratibu wa kutumia ulimi. Mwenye
kuongea sana akajikuta hasikilizi wengine anahitaji ukimya. Kuna watu ambao
wanaposikia pointi moja wanafikiria namna ya kujibu pointi hiyo na hawatilii
maanani poinyi nyingine. Wanahitaji utamaduni wa kuwa kimya. Baba mmoja wa busara wa Kijapani, wakati wa
kipindi cha Meji (1868-1912) alipokea
mgeni aliyekuja kuuliza juu ya siri ya mafanikio. Lakini badala ya kusikiliza,
mgeni huyo aliendelea kuongelea mawazo yake. Kitambo kidogo baadaye, baba
mwenye busara alimwandalia chai. Aliweka chai kwenye kikombe cha mgeni mpaka
kilipojaa pomoni ,aliendelea kujaza chai bila kukoma. Hatimaye mgeni hakuweza
kujizuia, “Hauoni kuwa kikombe kimejaa?” alisema. “Hauwezi ukaongeza
chai.” “Namna hiyo hiyo, na kama kikombe
hiki umejaa mawazo yako namna gani naweza kukuelezea siri ya mafanikio.” Sikiliza
vinginevyo ulimi wako utakufanya uwe kiziwi. Ni methali ya Amerika.
Tano, Yesu alitazama juu mbinguni.
Alitaka Mungu baba aingilie kati. Tunaambiwa na nabii Isaya, “…Mungu atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo
macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa…” (Isaya 35:
4-7). Tunahitaji msaada wa Mungu pengine kutambue kuwa sauti ya Mungu ni sauti
ya watu. Tusikilize sauti ya Mungu. Kusikiliza sauti ya Mungu. Atupashwi
kumwambia Mungu, “sikiliza mtumishi wako anaongea,” bali “sema Bwana kwa kuwa
mtumishi wako anasikiliza.”
Sita, akaugua. Kuugua ni kupumua kwa nguvu.
Alioneshwa kuguswa na matatizo ya wengine. Alimtazama kiziwi na bubu kwa
huruma. Kiziwi hafokewi. Nasi hatuna budi kuguswa na matatizo yaw engine, ndipo
watakuwa tayari kutusikilizwa. Saba, alisema efatha yaani funguka. Neno
linaumba. Tutumie maneno kutatua matatizo ya kutosikiliza. Tutoe mwito. Tutumie
matangazo na vipeperushi. Mfano palipo na soko yawekwe maneno haya. Nunu
mahitaji usinunue UKIMWI. Palipo na wengi yawepo maneno haya: Ulevi noma.
Mwenye masikio ya kusikia na asikie.
Siku hizi tumekuwa katika ulimwengu wa
kila kitu karibu kuwekwa ndani ya uwezo wetu. Hii yote imechangiwa na
mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia. Kumbe katika kila jambo tuwe makini kabla
ya utekelezaji, kwa kuchambua na kupima kipi ni kipi na kipi sicho. Na hivyo, kukubali
maneno ya mtu asemaye kwamba avutwa na Roho wa Mungu sharti kuchunguza ukweli
wa maneno yake.
1Yoh 4:1-3 “Wapenzi, msiamini kila
roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii
wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwajua Roho wa Mungu: kila roho
ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho
isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo
mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.” Kwa
kutambua sasa wapinga Kristo, maana yake ni wale walio kinyume na ukweli wa
Mungu; hivyo ni waongo. Mtu aliye mwongo hakika huyo hawezi kushuhudia ukweli
wa Mungu, zaidi atafanya upotoshaji. “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye
anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye
anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye:
ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” Kwahiyo, alama kwamba
anampenda mtu ampenda Mungu kweli ni mapendo yake kwa jirani. Sasa kama unaweza
kuwadanganya wengine ya kuwa unaponya hiki na kile, kumbe hamna mkono wa Mungu
wewe ndiye mpinga Kristo.
Maana
siku hizi tunaona wachungaji wakijitokeza wengi sana, na wengine kusema
wamevuviwa ama wamefunuliwa na Mungu kuanzisha Kanisa fulani. Lakini utagundua
ya kuwa ni wapinga Kristo pale unapowasikia wakijinadi na kutafuta wateja wale
ambao hawajaimarika na kuiva kiimani kuwa waje tunaponya maradhi mbalimbali.
Zaidi ya hayo katika ibada zao hutosikia neno Kristo Yesu ndani ya madhehebu au
ibada zao; hao tambua ni wapinga Kristo. Ndugu yangu unayekisoma kitabu hiki,
wafikishie na wengine ambao bado hawajatambua mbinu chafu wanazotumia manabii
hawa wa uwongo na wapinga Kristo. Kabla ya kwenda kwao wajitahidi kuyapima na
kuyachunguza maneno ya washawishi wao. Ndiyo maana zaidi utasikia wakijigamba
kwa mambo yahusuyo miujiza na mengin mengi yahusuyo hayo. Wanasema itika wito
kata neno, ila mimi nasema hata huo wito wa kwenda kuwasikiiza usipoteze muda
wako usijeukadanganyika na kushawishiwa nao.
Lakini
tutambue ya kuwa mimi na wewe tunaojiona ya kuwa tu wafuasi wake Kristo, kama
maisha yetu hayafuati matakwa ya Mungu; nasi tu wapinga Kristo. Kwa mantiki
hii, tunaposhindwa kufanya mapenzi ya Baba, ni sawa na kumchukua Mwana wake
(yaani Yesu Kristo) na kumrudisha au kumkumbusha mateso tuliyomtendea. Japo
kwake Mungu aliyatenda kwa upendo na huruma, kusudi tupate kuokolewa. Kumbe
tutambue moja kwa moja, tunaposhindwa kuishi au kuyaishi yale tunayoyafahamu;
tutambue kwamba tu wapinga Kristo pia. Ili sasa tuweze kujinasua na janga hilo
la kumpinga Kristo, mimi na wewe tujitahidi kuishi vema na katika kweli kile
tunachofundishwa Naye. Kwani tukiendelea
kumsikiliza Yeye basi anatueleza kututapotea kwani Yeye ndiye njia, kweli na
uzima. Na hivyo tutabaki tumeshikamana naye mpaka huko alipotuahidia kufika,
kwani tutakuwa watoto wema, waaminifu na wasiomsaliti au kumpinga Yeye
aliyemtuma kwetu. Na hivyo Yesu ni njia ya kwenda kwa Baba.
Bwana asema hivi, “Amelaaniwa mtu Yule
amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake
amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema.
Bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.
Kuna wakati kama wanadamu tunashindwa
kumwona Mungu katika yale tukuanayo katika maisha. Na hii yote inachochewa na
hali ya kuwategemea wanadamu wenzetu. Utasikia mara mtu fulani amekumbwa na
janga, oh hapo kuna mkono wa mtu. Lakini wanashindwa kutambua ya kuwa yeye
aliyeumba kila kitu ndiye mwenye mamlaka ya mambo hayo. Yesu mwenyewe anautoa
mfano huo wa wagalilaya walikuwa wameuliwa na Pilato, sasa anawahadharisha ya
kuwa kuuawa kwao siyo kwamba walikuwa wakosefu kupita wengine walioishi Yerusalemu.
Bali ni mpango wake na hivyo mwito wake akiwata nao waliobaki watubu vinginevyo
wataangamia pia. Rej Lk 13: 1-5.
Na hivyo majanga hayo tupitiayo siyo
adhabu ya Mungu. Bali mambo ya kupita tu. Na hivyo tubaki kumshikilia sana
Mungu kwa kuwa na matumaini kwake. Kama binadamu pale tukutanapo na matatizo
basi ndiyo wasaa wa mateso, huzuni, taabu, shida, usumbufu, udhia n.k , na
kujiona kuwa hatusikilizwi na watu sisi. Hapo ndipo tunakuja kuona watu wa aina
mbili; Yule ambaye katika mahangaiko anamsahau Mungu naye ambaye katika
mahangaikobasi ndipo anamtafuta Mungu. Kumbe tujiunge na Mwanafalsafa Simone
Weil (1909-1943) Mfaransa wa mambo ya jamii aliyesema “Jinsi ilivyo vigumu
kumsikiliz mtu aliye katika mateso ndivyo ilivyo vigumu kwake kutambua kuwa
huruma inamsikiliza.”
Yesu Nakutumainia (Jesus I Trust in Yoo
or Jesus I Trust in Thee), ni maneno tunayoyaona katika picha aliyoonyeshwa
Mtakatifu Sista Faustina Kowalska.
Maneno haya
yanatoa ni kwa jinsi gani maisha yetu
yanapaswa kumwelekea Kristu. Kwa maneno mengine yanatupa picha halisi ya maisha
yetu ya kuwa yanaaswa kumtegemea Mungu. Na hivyo daima tuanze na Mungu na
kumaliza na Mungu. Kwa kufanya hivyo, hakika hatutapungukiwa na kitu. Kwani
Mungu ndiye mtoa na mwezeshaji wa kila kitu. Amebarikiwa mtu Yule anayemtegemea
Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake.
Kwanini tuwe watu wa kutaka tuone
ishara ndiyo tuamini? Kumbuka Yesu alimwambia Thomaso ya kuwa waheri wale
wasioona wakasadiki. Lakini pia tunashindwa kutambua kuwa Yesu mwenyewe
alishatuambia ya kuwa hakuna ishara tena baada ya ile ya Yona. Kwa hiyo, tusing’ang’anie mambo yasiyo ya
msingi.
Wakatokea
Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni;
wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, “Mbona kizazi hiki chatafuta
ishara? Amin, nawaambieni: Hakitapewa ishara kizazi hiki.” Akawaacha, akapanda
tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.
Sasa ndugu zangu ambao tumekuwa
tukikimbilia na kuamini miujiza eti ya siku hizi, kweli tunamwelewa Yesu? Kuna
mtu amebaki ni mtu wa kutangatanga. Ameugua tu cha kwanza cha kufikiria ni juu
ya wachungaji wanaotenda miujiza. Akiamini hao watamponya. Hiyo hali binafsi
naiona kama mchezo wa kuigiza tu. Kama kweli unaamini juu ya Mungu kuwa ni
mweza wa yote, kwa nini usibaki ulipo na siyo mpaka kuanza kutafuta watu wa
ziada? Tubadilike pia tujitambue na kuanza kujiuliza mara kadhaa. Kwa nini
kuponywa kwako ni mpaka uwafuate? Mungu yuko mahali pote, na hivyo kama kweli
una imani atakusaidia na kukuponya katika maradhi yako. Tusikae na kusubiri
miujiza. Siyo kila kitu cha kushangaza au cha muujiza chatoka au kinatendwa na
Mungu. Chunguza vizuri baadhi yao utawakuta wanatumia nguvu za giza. Sasa
usipojua hayo, nawe unaenda kuwa mshirika wao. Na tambua shetani akishakukamata
kujitoa ni ngumu sana. Tusikubali kuchumbiwa au kutongozwa (kushawishiwa) na
shetani, ni mbinu tu anatumia kutuvutia kwake tusipokuwa imara katika imani.
Siku hizi mimi na wewe tumekuwa hodari
sana kwa mambo ya kidunia zaidi. Kwa mfano, unamkuta kijana amekariri wimbo wa
msanii fulani, anauimba mpaka unabaki
kushangaa kwamba inawezekanaje jabo hilo. Au kijana anajua kikosi cha
timu fulani, kuanzia kikosi cha kwanza (First Eleven), walioko katika benchi
(Subsitituion) wote. Huyo huyo kijana, anajua historia ya mchezaji fulani wa
mpira au historia ya msanii fulani. Sasa cha kushangaza na cha ajabu, jaribu
kumwuliza juu ya Katekesimu hakumbuki chochote. Tusiende mbali, hakumbuki wala
hajui hata tarehe ya Ubatizo, Kipaimara, Komunyo ya Kwanza. Achilia hayo,
mwulize juu ya Historia ya Mtakatifu Somo wake, hajui chochote. Huyu kijana
ambaye anauwezo mkubwa wa kujua mambo haya mengine ya kidunia, na mbaya zaidi ni
Mkristo Mkatoliki ilia mambo ya Kiroho hajui wala hakumbuki ila ya kidunia
ndiyo yako mikononi mwake.
Sasa je! Tunaenda wapi au tunalipeleka wapi
Kanisa la kesho na Roho zetu tunaziandaa kwenda wapi? Hamu yetu iwe katika mambo ya mbinguni na
siyo ya kidunia. Kol 3:2
Sisi wote tu mali yake Mungu. Ubaguzi
watoka wapi? Kuna wakati mwingine tunaleta mambo ya kutisha na kushangaza. Kama
Wakristo kuanza uwaza na kuwekeana mipaka kwa kuangaliana; huyu kabila gani,
ukoo gani, anatokea wapi, maskini, tajiri. Haya yote hayana nafasi kwa kuwa kwa
Mungu wote tu sawa. Gal 3: 27-28, 1 Kor 12: 13
Kumbe hatuna sababu ya kuanza kuwekeana
mipaka. Wakati kupitia kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo basi tumekuwa na
uhusiano Mwema baina yetu kwa sisi pia na Mungu. Kwa kuivunja minyororo basi
amekuwa daraja kwa sisi kupita. Vivyo hivyo, nasi kama wafuasi wake tunaalikwa
kuendelea kutunza na kuuishi uhusiano huu mwema. Tuishi pasipo kutazamana
kijicho wal akudhaniana vibaya au kufikiriana vibaya. Tuishi kwa amani, bila kudharauliana,
bila kuonyesha umaridadi, au kujiona sisi ni bora zaidi kuliko wao au wale. Tukizingatia
ya kuwa wote kama Wakristu lengo letu (final destiny) ni kufikia Utakatifu mara
baada ya maisha ya hapa dunaiani. Kumbe tukishindwa kuishi Upendo, hapo ndipo
tunakaribisha ubaguzi na matabaka kati yetu. Ndiyo maana hata tunapoishi
tutambue na kujua ya kuwa maisha siyo tu hapa duniani bali kuna maisha baada ya
kifo.
Tusiwe watu wa kuitwa Nomine Christus;
yaani Wakristo jina, tupambane kweli kweli. Tujifunze mfano wa Watu waliopewa Talanta, ambapo Yesu anautoa juu ya mtu
atakaye kusafiri lakini kabla ya kusafiri akawaita watumwa wake na kuweka mali
zao kwao. Kuna aliyepewa Talanta tano, na mwingine talanta mbili na mwingine
talanta moja. Akishakurudi akawakuta
watumwa wawili wamezalisha mara mbili ya talanta walizopewa ila Yule mmoja
aliyepewa talanta moja hakufanya au kuongeza chochote. Kwa hiyo hao watumwa ni Wakristo. Yesu
anawaachia neema zake ili wazitumie kupata matunda. Baadaye atawadai watoe
hesabu ya kutumia neema zake. Na neema
hizi ndugu zangu tunazipata kupitia Sakramenti takatifu mbalimbali tuzipatazo
katika kutujenga na kutuimarisha zaidi na kubakia kweli kuitwa Wakristo.
Ukristo wetu unatudai kutoa matunda.
Kama Yesu alivyo mzabibu wa kweli, nasi hali kadhalika tunaalikwa kuiga kwake. Mintarafu kielelezo cha mzabibu (rejea
Yer 2:21; Isa 5:1) katika Injili tatu za kwanza Yesu anatumia kielelezo hicho
kwa kueleza Ufalme wa mbinguni (Mt 20: 1-8, 21:28-31, 33-41). Yesu anatumia
uzao wa mzabibu kwa ajili ya Ekaristi Takatifu ya Agano Jipya (Mt 26:29). Hapo
Yesu anajiita mzabibu wa kweli, uzao wake utakuwa Taifa jipya teule, wala
halitadanganya matumaini ya Mungu. Taifa jipya hilo litaishi katika uzima wa imani
na mapendo kwa sababu wanaishi katika Kristo. Taifa teule ndiyo mimi na wewe ambaye
tunamwamini Kristo, na hivyo tu Wakristo maana tumeshikamana naye na
kunamdhihirisha pale tunapofanya yale yampendezayo; na kwa kufanya hivyo
Ukristo wetu utakuwa unazaa matunda.
- Gal 5: 22, 23a, 25 Matokeo ya
kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu……
Tufike mahali tuone matatizo ni maisha
na maisha ni matatizo. Au kwa lugha nyingine tufike mahali tukubaliane na hali
zetu, tusiwe watu wa kuishi maisha ya kuiga
Biblia ya Kikatoliki Toleo la Iringa.
Katekisimu
ndogo ya Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Songea.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Paulines
Publications, Nairobi, 2000.
Mchamungu Henry, Maadhimisho ya Sakramenti kuendana na Sheria za Kanisa, Nesmap
Printing Technology, Dar es Salaam, 2017.
Mtaguso Mkuu, Maelezo ya Hati 16 za Vatican II,
Jimbo
Kuu Tabora, Toleo la Nne 1993.
OTT Ludwig, Fundamentals of Catholic Dogma, J. C. Bastible (ed), P. Lynch
(trans.), Tan books and Publishers, Inc, Rockford, 1960.
Saba
Raymond, Wewe ni Kuhani Milele, Tafakari
ya Mababa wa Kanisa juu ya Upadri, Toleo la Pili, Benedictine Publications
Ndanda- Peramiho Tanzania, 2017.
The
Code of the Canon Law, New Revisedd English Translation, Harper Collins
Publishers, Newsland, 1983.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania, Misale ya Waamini, Toleo la Kumi, TMP Book
Department, Tabora- Tanzania, 2008, Uk. 920-921.