Wednesday, January 29, 2020

AMRI ZA KANISA


                                         Amri za Kanisa

Kuna jumla ya amri sita za Kanisa. “Amri hizi za Kanisa zimepangwa katika fumo wa maisha ya maadili, zikifungamanishwa na kulishwa na maisha ya Liturujia. Sheria hizi zilizowekwa wazi na mamlaka ya kichungaji zina hali faradhi kwa lengo la kuwathibitishia waamini kiwango cha chini kabisa cha lazima katika roho ya sala na juhudi ya maadili, katika kukua katika mapendo kwa Mungu na jirani.”[1]  Nazo ni zifuatazo kulingana na Misale ya waumini:[2]
1.  Hudhuria Misa Takatifu Dominika na sikukuu zilizoamriwa.
Inamtaka mwamini kutakatifuza siku ya kumbukumbu ua fumbo la Ufufuko wa Bwana, lakini pia sikukuu kubwa za kuheshimu mafumbo ya Bwana, ya Bikira Maria Mwenye heri, na ya Watakatifu. Kwanza, kwa kushiriki adhimisho la Ekaristi ambamo jumuiya ya Kikristo inakusanyika, na kupumzika na kuacha zile kazi na shughuli ambazo kwayo zingezuia kutakatifuza siku hizo.[3]  Lakini pia mwamini apumzike kwa kuacha kazi nzito.[4]
2.  Funga siku ya jumatano ya majivu; usile nyama siku ya Ijumaa Kuu.
Ndugu yangu unayesoma kitabu hiki, unapoongelea Jumatano ya Majivu huwezi kutupilia mbali Kwaresima, maana Jumatano ya Majivu ndiyo mlanngo wa kutuingiza katika Kwaresima. Kumbe hatuna Kwaresima pasipo Jumtano ya Majivu. Siku ya Jumatano ya Majivu tunaanza rasmi kipindi cha Kwaresma ambacho kinadumu kwa muda wa siku arobaini. Kwa nini siku arobaini? Waisraeli walikaa jangwani sku arobaini, gharika kuu ilidumu siku arobaini, Yesu alifunga siku arobaini, kwaresma inadumu siku arobaini. Miaka/siku arobaini katika Maandiko matakatifu inawakilisha kipindi kamili cha mpito ambacho ndanimo jambo linaweza kufanyika na likakamilika. Hivyo Kwaresma ni kipindi kamili cha mpito ambacho ndanimo mapinduzi ya kiroho yanaweza kufanyika. Ni kipindi cha kufanya maandalizi ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka.  Na hivyo kinaambatana na kupakwa majivu yatokanayo na matawi tuliyotumia Dominika ya matawi; katika paji la uso kwa waamini lakini kwa Waklero kichwani. Katika kipindi hiki mama Kanisa anatualika kufanya tathimini ya mahusiano yetu na Mungu. Ni kipindi cha kufanya mapinduzi ya kiroho.Waamini tunahimizwa kwa naamna ya pekee kuhudhuria liturjia ya leo.[5] Majivu tutakayopakwa ni alama ya ukubali wetu kwamba sisi ni wadhambi, hatuna thamani mbele ya Mungu na tunahitaji kufanya toba.

Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni.[6] Baadaye utamaduni huu wa kupakana majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba. Mwaka 600 hivi, Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresma na akaongeza urefu wa kipindi hiki cha toba hadi siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya majivu kwaajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana. Sasa pale walipoamua kufanya toba ndio walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale walikuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile Malaya, wauaji, waasi n.k. Kuanzia karne ya 11, Kanisa lilipanua ibada hii na kuwahusisha waamini wake wote na si wadhambi waliokubuhu tu. Hatua za kuchukua ili tuweze kufanya vema mapinduzi ya kiroho, toba na kubadilika. Tukubali kwamba sisi ni wadhambi. Tusipokubali kuwa sisi ni wadhambi halafu hatutaona hitaji la kufanya toba na kubadilika. Ndio maana tunapakwa majivu ikiwa ni alama ya kukubali kuwa sisi ni wadhambi hatuna thamini mbele ya Mungu, na hivi tunahitaji kutubu. Kutumia misaada mbalimbali ambayo itatusaidia kumrudia Mungu: Sala, kufunga na matendo ya huruma. Na hivyo kwa kutambua tu wadhambi ndiyo maana tunapaswa kufunga siku hiyo ya Jumatano ya majivu.

Lakini pia usile nyama siku ya Ijumaa Kuu. Tukumbuke ndiyo siku Mkombozi wetu Yesu Kristo anakufa msalabani. Na hivyo hatupaswi kula nyama kama waamini wenye kutambua thamani ya wokovu wetu. Kwahiyo, ni siku ambayo waamini wanakuwa katika huzuni, wakiomboleza juu ya kuondokewa na Mpendwa wao. Kama tujuavyo katika hali ya maisha yetu ni kwamba nyama inatumika na kuthaminiwa kama chakula fulani cha hali ya juu, yenye thamani na nzuri sana; ni katika uzuri huo watu wanaona fahari na kuwafanya wafurahie. Mfano mzuri ni huu, ukitaka kuona au kusikia sherehe fulani wanaisifia kuwa ilikuwa nzuri; wengi waseamao utasikia yaani walijipanga kwelikweli: nyama ilikuwa ya kutosha kwa maana walichinjwa labda ng’ombe watano (5) na kitakachofuata ni kinyaji, utasikia kulikuwa na pombe ya kutosha kama ni ya kienyeji au bia au divai n.k. Kwa hiyo, hatunabudi kufunga siku hiyo kula nyama.

3.  Ungama dhambi zako walu mara moja kila mwaka.
Pia sheria hii yahakikisha maandalizi kwa ajili ya Ekaristi kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho.[7] Hii inaonyesha mwendelezo wa kazi ya wongofu na msamaha wa Ubatizo.[8]
4.  Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa Paska.
Kama nilivyotangulia kusema, sheria hizi za Kanisa kuwa inatoa walau kiwango cha chini. Kumbe amri hii yahakikisha kiwango cha chini cha kupokea Mwili na Damu ya Bwana kuhusiana na sikukuu za Pasaka, asili na kilele cha Liturujia ya Kikristo.[9] Na hii inaenda sambamba na wale wanaoweza kushiriki Misa zaidi ya moja. Waliowengi hawajui ya kuwa kama umemaliza Misa hii na ukampokea Yesu katika maumbo ya mkate na divai, unapoenda Misa nyingine una haki ya kumpokea tena. Siyo useme tu nimemaliza kumpokea Misa iliyopita na sasa sitaki au siwezi, wewe mpokee labda kama unaona hufai pengine kiroho. Lakini kulingana na mazingira unaruhusiwa kumpokea hata kama unajua kiroho ni mdhambi. Pengine ni kigangoni na Padre amekuja kwa kuchelewa kwa sababu za kichungaji, basi usishindwe kwenda kumpokea ilimradi tu ulikuwa umeshaweka nia ya kuungama kwanza. Na hivyo ukiwa katika nia hiyo unaruhusiwa kukomonika, ila unuie kuwa mara baada ya kukomonika basi unamtafuta Padre kwa maungamo. Ukifanya hivyo utakuwa hujatenda dhambi na katika kumpokea Yesu maadam hujasitahilishwa basi inakuwa siyo kufuru na unakuwa hujajitwalia hukumu yako.  
5.  Saidia Kanisa Katoliki kwa zaka.
Ina maana ya kwamba waamini wana wajibu na kazi ya kusaidia kutoa mahitaji ya Kanisa kila mmoja, kadiri ya uwezo wake.[10] Zaka hii inapaswa kutolewa fungu la kumi la kile unachojaliwa au ulichojaliwa.[11]
6.  Shika sheria Katoliki za ndoa.
Lakini kwanza tutambue kuwa ndoa ni sakramenti kwa wakristo na hasa kwa wakatoliki. Ndoa ni agano kati ya mtu mume na mtu mke. Ndoa ni aganao linalowafanya wanandoa kusihi pamoja kwa maisha yao yote.[12] Kwa kweli nakosa hata nguvu za kuongelea juu ya amri hii. Walio wengi naamini ni mashahidi, ya kwamba amari hii haitendewi haki na wale wenye kuitendea haki. Sina uhakika ni watu wangapi ambapo kwa uwazi kabisa tukiwauliza juu ya amri hii kama wanaijua vilivyo; hususani wanandoa. Mama Kanisa katuwekea sheria jumla mia moja na kumi na moja (111) za ndoa.[13]  Sheria zenyewe hizi zimegawanyika katika sehemu kumi (10) kwa kadiri ya Kitabu cha kanuni ya Kanisa Katoliki toleo la pili la mwaka 1983.
a)  Mtazamo wa kichungaji na nini kinatangulia maadhimisho ya ndoa (Pastoral care and what must proced celebration of marriage)
b)  Vipigamizi vya ndoa kwa ujumla (Diriment impediment in general)
c)   Vipingamizi vya ndoa moja kwa moja (Diriment impediment specifically)
d)  Makubaliano ya ndoa (Matrimonial consent)
e)  Nguvu ya ndoa (Force of marriage)
f)    Ndoa mchanganyiko (Mixed marriage)
g)  Kuadhimisha ndoa wa siri (The secret celebration of marriage)
h)  Athari za ndoa (Effects of marriage)
i)    Kuwatenganisha wanandoa kwa muda (Simple separation of spouses)
j)    Kuhalalisha ndoa ambayo haikuwepo (The convalidation of marriage).[14]




[1] KKK Na. 2041.
[2] Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Misale ya Waamini, Toleo la Kumi, TMP Book Department, Tabora- Tanzania, 2008, uk. 1077.
[3] Rej. MSK. Na. 1246- 1248.
[4] Rej. KKK Na. 2042.
[5] Rej. Katekisimu ndogo ya Katoliki Jimbo la Iringa, Na .97, 100.
[6] Rej. Ayu 2: 8, 30: 19; Zab 102: 10.
[7] Ibid.
[8] Rej. MSK. Na. 989, 719.
[9] Rej. Sheria za Kanisa Katoliki, CIC Na. 920, 708, 881.
[10] Rej. Sheria za Kanisa Katoliki, CIC Na. 222, 1249-1251, 882, 25.
[11][11] Rej. Law 27:30-33.
[12] Rej. Elias Nada, Karne ya Ishirini na Moja na Ndoa za Kikristo, Sayansi, Maisha ya Familia na Ndoa, Chapa ya pili, Timia Printers, Moshi, 2015, uk. 25.
[13] Rej. Sheria za Kanisa Katoliki za Ndoa, Mada ya saba Ndoa (CIC 1055-1165).
[14] The Code of the Canon Law, New Revisedd English Translation, Harper Collins Publishers, Newsland, 1983, 237-258.
[15] Eze 18:23-28.

No comments: