Wednesday, January 22, 2020

Maisha ni sasa


Napenda kuanza kwa kusema kuwa ‘The means justify the end.’ Nikimaanisha namna ya maisha yetu ya sasa ndiyo yanayo au yatakayotuwezesha kuiona ya kesho. Maneno mengine, ni kwamba maisha tuishiyo leo ndiyo yanayotabiri kesho yako wewe, mimi na yule. Kwa hiyo namna ya kuishi kwetu leo, inatupatia fursa ya maandalizi ya maisha ya hapo baadaye mara baada ya maisha ya hapa dunia. Kwa mantiki hiyo, tuna kila sababu ya kujitahidi kuishi maisha ya kulenga hapo baadaye itakuwaje. Kufikiri zaidi (foresee or aim high) itakuwaje, na kama umeshaanza kuishi kwa kuona na kutenda kwa kuangalia au kulenga juu ya mwisho wako ni vizuri.

Endelea na kasi hiyo, kwa kusonga mbele na usirudi nyuma kamwe (Ever forward never backward). Kama mwaliko wa siku zote wa Mheshimiwa Rais Dr. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara zote anavyopenda kutuasa kama wananchi kuwa tusibaki kutazamana tu bali anasema “Wewe chapa kazi tu.
Pia tukiongozwa na methali isemayo, ‘Ngojangoja yaumiza matumbo’ tuchangamkie fursa kwani wakati wenyewe ndiyo huu wa kufanya na kuandaa maisha yetu ya hapo baadaye kuwa mazuri. Tusikae tukabweteka mpaka kufikia wakati ule wa NINGE…. Ninge…. Hii huja mwisho wa safari, ambapo tunakuwa tumeshachelewa na haiwezekani tena. Kama tusemavyo kuwa ‘maji yakishamwagika huwa hayazoleki.’ Ni kwa mantiki hiyo hiyo tunaona mfano ule wa mtu tajiri na Lazaro. Tajiri anvyomlilia Ibrahimu kwa kumwomba amtume basi aende duniani ili awambie juu ya hali aliyokuwa akipitia ili basi nao wasiweze kuingia huko. Lakini tunaambiwa kati yao wametenganishwa na shimo kubwa, na hivyo haiwezekani. Kwa kuwa kuna wengine walioko huko dunia basi wasipowasikiliza hao nao pia wataingia kwa tajiri alipokuwa. Hapa anatufundisha kuwa haiwezekani tena kurudi nyuma, na hivyo tusiisubirie hiyo ninge….tukajikuta tumeshachelewa sana.[1] Kumbe kwa kuwa mimi na wewe bado tuna nafasi ya kujirekebisha basi tufanye hivyo; kabla ya NINGE… haijaja kusikika masikioni mwetu maana muda utakuwa umeshaisha tena wa kusema tunaweza kurekebisha maisha yetu.
Na hivyo kama wasemavyo kuwa ‘Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi.’ Kuna mtu mwingine anapenda kuyafanya maisha yake kuwa ya mazoea. Tafadhali, mwanadamu daima ni mwili na roho pia mwanadamu hulka yake ni kubadilikabadilika kama kinyonga. Kubadilikabadilika huku ni kule kutoka hali hasi na kwenda hali chanya. Mfano mtu ameshauriwa kuuacha mwenendowake mbaya na afanye hivyo kweli kwa kubadilika au kubadilisha mwenendo wake. Si hivyo tu, ni busara ya kawaida kwamba unapoenda sehemu ukawakuta wanaomboleza basi nawe jiunge nao katika maombolezo hayo. Na kwa kufanya hivyo kile kinachofanyika pale ni kwa manufaa ya jamii nzima, wala siyo cha mtu binafsi.
Sasa, kuna watu wengine kupitia mazoea tunashindwa kuelewa somo hilo juu ya mabadiliko. Kwa mfano, kuna mtu anamchukulia mtu fulani kuwa wa mfano kwake katika maisha; mbaya zaidi mtu yule maisha yake ni ya ajabu ajabu. Kwanini sasa aige maisha hayo? Ukifuatilia utakuta wanatabia zinazoendana au kukaribiana. Wana namna zinazoendana katika yale wayapendayo na yale wasiyoyapenda katika maisha yao. Na huu kwa hakika ni mfano uliohalisi, kwamba jaribu kuchunguza wale watu waliomarafiki. Utakuta kuna kitu wanashirikiana aidha kitabia na mwenendo mzima wa maisha.
Kumbe tambua kuwa kila mtu anabahati yake kuanzia leo. Sasa wewe utasema naishi hivi kwa maana hata fulani anaishi hivi na maisha yanaenda. Ila jua kila mmoja alizaliwa kwa mama yake pekee, si hivyo tu tena kila mmoja alizaliwa peke yake, anaishi peke yake, atakufa peke yake na mwisho atazikwa pekeyake. Kwa kujua hilo ndiyo maana kila mtu anakuja na bahati yake. Kwa hiyo, haya malimwengu yasikusumbue kabisa; kwa kuwa tumeyakuta. Kwani tumezaliwa tuli uchi na tutarudi vivyo hivyo.[2] Huyu rafiki yako, swahiba, shosti wote umewakuta tu. Kumbe huna sababu yoyote ya kumfanya mtu huyo awe kama mungu-mtu. Ndiyo maana ukiwa mtu wa kuchukua na kuiga kila kitu kama kilivyo (copy and paste) kwa mwingine unaweza kuishia kubaya. Maana huwezi yeye ameandikiwa nini na Mungu, maana yeye tunaambiwa alitujua tungali tumboni mwa mama zetu.[3] Ndo hiyo utashangaa mwenzako, licha ya maisha yake mabaya aliyokuwa anaishi ila dakika za mwishoni anamrudia Mungu; ila wewe isitokee hivyo. Kwa hiyo tujihadhari sana katika maisha yetu. Tujiepushe na kuiga kila kitu bali yale yaliymazuri basi tuyaige na kuyafuata. Lakini katika yale yanayoweza kutupotosha au kutupeleka katika njia isiyo sawa, ambayo inaweza kututenga naye Mungu; basi hatunabudi kuyatupilia mbali. Kwa maneno mengine hatunabudi kuachana nayo tena moja kwa moja.


No comments: