Sababu zinazoweza kupelekea Kifo[1]
Kila mmoja wetu amekwisha kutambua ya
kuwa kifo ni lazima tukipitie. Kwa kuwa hata katika uumbaji (uhulushi) tunajua
ya kwamba mwanadamu ni mwili na roho. Mara tu baada ya kutungwa kwa mimba, basi
Mungu mwenyewe ndiye aiwekaye roho hiyo. Mwili daima unakufa, lakini roho kamwe
haifi. Ndiyo maana mtu baada ya kufa mwili ule unaoza kwani umeumbwa kwa
kitufaa (matter or material). Kwa lugha nyingine ni kwamba; ‘material body or
things normally corruptible, hence decay’.[2]
Kwani kupitia kuonja mauti, ndiyo njia pia itupasayo kufika kwa Baba. Huko
ndipo tutaenda kuishi na kustarehe kwa umilele. Sasa kwa kuwa kifo ni matokeo
ya dhambi ya asili waliyoifanya wazazi wetu wa kwanza yaani Adamu na Eva.
Zifuatazo zinaweza zikawa sababu ambazo zinaweza kupelekea kifo, kwa kila mmoja
wetu. Japo ni fumbo kwetu kama wanadamu kutambua tutakipitia kifo kwa njia ipi.
Ila uhakika tulionao tu ni kwamba lazima kifo tukipitie.
1 Magonjwa
Kama tutambuavyo mapisi (historia) ya
Adamu na Eva kule bustanini, ya kuwa waliishi vizuri na wanyama tena. Lakini
baada ya kukosa utii, Mungu aliamua kuwafukuza bustanini na kuwapa mapigo
kadhaa. Kama tutambuavyo ya kuwa hata dhahabu hujaribiwa kwa moto, ndivyo hivyo
nasi tunakutana na magonjwa mbalimbali ili kuyafanya maisha yaende cha
mikikimikiki. Kwa hiyo, maisha yetu kutokana na waandami (watangulizi) yaani
wazazi wetu wa kwanza, nasi hatunabudi kuyapokea mahangaiko, mateso yatokanayo
na maradhi. Kwani ardhi yote imelaaniwa kwa sababu wazazi wetu, vivyo hivyo
nasi tunapatwa na yale aliyosema Mungu kama laana juu yetu.
Sasa katika maisha yetu tunaona na
kushuhudia watu wengi wakifa kwa sababu mbalimbali za magonjwa. Na
kinachosikitisha zaidi ni kwamba wakati huu watu wamekuwa wengi na magonjwa
nayo yameongezeka sana. Kuna magonjwa ya aina mbalimbali ila zaidi ni ya
kuambukizwa na yale yasiyoyambukizwa. Lakini yote katika yote unachelewa kupata
huduma basi ugonjwa ukawa umeshamaliza au umeshatawala mwili kwa kiasi kikubwa
basi hata matibabu unayowekupata yanaweza tu kukusaidia kusogeza siku au hata
masaa. Magonjwa ambayo ni tishio sana kwetu mpaka sasa ni Mgandamizo wa damu
(Presha), kisukari, ugonjwa wa moyo, saratani au kansa, UKIMWI pia malaria.
Haya kwa kiasi kikubwa yamekuwa changamoto sana siku hizi. Mbaya zaidi
yaliyomengi yanayoonekana kuwa kama tishio kwa kipindi hiki, mengi yanachangiwa
na matumizi ya vyakula. Tunajikuta tumelalia kula vyakula vya kisasa (vyakula
vinavyopita viwandani) zaidi kuliko vile vya asili. Vyakula vilivyojaa sana
mafuta.
Tahadhari ni kwamba watu waanze kuwa na
mazoea ya kupima na kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kujua maendeleo ya
afya zao. Hii isifanyike kwa ratiba bali iwe kila mara unapopata nafasi ya kufanya
hivyo basi fanya. Kwani unapogundulika unatatizo fulani na ukawa tayari kufuata
maelekezo ya Madaktari, aidha kwa kuacha kula aina fulani za vyakula au kwa
kula aina fulani tu za vyakula basi utakuwa katika nafasi nzuri ya kuuweka
mwili wako katika mazingira safi ya kupamabana na maradhi mengine ambayo
yanaweza kujitokeza.
Lakini pia kuna maradhi mengine sisi
wenyewe tumekuwa chanzo cha kuyasababisha. Kwa mfano kuna magonjwa ya mripuko
ambayo unakuta chanzo chake kikuu ni kushindwa kutunza mazingira yetu salama.
Hali tukitambua kuwa tukiyatunza mazingira hakika nayo pia yatatutunza. Kwa
mfano kuna watu wanakufa kwa sababu ya mripuko wa ugonjwa wa Kipindupindu au
Ebola. Sasa mtu watu hawa waathirika wanapokosa msaada wa huduma ya haraka
lazima tuwapoteze, maana hamna namna. Kwa hiyo, tuwe makini na tutunze
mazingira yetu nayo yatatutunza na kutuweka salama.
2 Ajali
Si kila ajali inatokea kwa sababu ya
uzembe wa wale wenye dhamana ya kuongoza vyombo hivyo vya safari. Lakini zilizo
nyingi chanzo kikubwa ni uzembe wa wahusika. Kuna aina mbalimbali za usafiri
ukiwemo wa nchi kavu (Barabarani), majini pia angani. Sasa mara nyingi utakuta
ni uzembe wa Dreva ama Nahodha ama Lubani kushindwa kuwa makini wakati
anaongoza chombo. Na hii inatokana na kuwa na mawazo tawanyishi. Yaani mawazo
yake muda fulani yanakuwa yametawanyika, badala ya kuwaza kile chombo
anachoongoza anawaza yaliyo nje ya pale. Sasa hali hiyo inapoendelea inaweza
kumfanya apoteze mwelekeo. Apotezapo mwelekeo tu, maana yake anaposhindwa kufuata
vigezo na masharti ya uongozaji basi utasikia ajali imetokea.
Si hivyo tu, bali wakati mwingine
inatokana na uchakavu wa vifaa au vimbo hivyo. Yaani unakuta ni chombo cha
usafiri na kila siku au kila mara kiko safarini, kwa bahati mbaya uangalizi
unapokuwa hafifu au mdogo. Sasa kama hamna uangalizi (kufanya service), kuna
siku kinaweza kuwa kibovu na kwa kuwa hakina uangalizi wa mara kwa mara au
kabla ya kuanza safari; basi mwisho wa siku kikiwa safarini na tatizo
limeshakuwa kubwa utasikia kimepata ajali na watu kadhaa wamefariki dunia papo
hapo na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Kwa hiyo, kuwa na muda wa kuwa
tunavihakiki ubora wake ni muhimu sana.
Mara nyingine pia mazingira ya hali ya
hewa yanaweza kusababisha ajali. Kuna wakati hali ya hewa ndani ya maji
inachafuka yaani unakuta mawimbi yameongezeka na chombo kiko safarini au chombo
kiko angani na huko kinakutana na kani ya mvutano na hivyo kupelekea chombo
hicho kupoteza mwelekeo. Hatimaye kinashindwa kumudu au kukabiliana na hali
hiyo, basi kinabaki kuongozwa na hali ya hewa ya wakati huo. Na baadaye
utasikia kimepata ajali. Kama tujuavyo Meli ya Mv. Bukoba ilivyozama tarehe
21-05-1996 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 800.
Lakini pia sababu nyingine ya ajali
inakuwa ni Dreva mwenyewe asiyejali mwendokasi. Mfano ulio hai ni huu, kuna
aina tatu za Madreva; Dreva Kenge (huyu ni Dreva wa kukurupuka, pasipo kujali
ubora wa chombo chake pia mwendokasi), Dreva Nyoka (huyu anaendesha kwa
kupindapinda, yaani anaenda kwa kukatakata makona mfano anataka kumpita
mwenzake shemu mbaya au isiyoruhusiwa na akiwa katika mwendokasi), na wa mwisho
ni Dreva Kinyonga (huyu ni Dreva anayeendesha kwa usalama na anafuata kanuni
zote za barabarani vizuri). Kumbe mwendokasi unapelekea wakati mwingi ajali,
maana anapokutana na kona kali na yuko mwendokasi lazima limshinde kukata kona,
mwisho wa siku gari litamshinda kumtawala na kuanguka au kupindukapinduka.
Ajali nyingine zinakuwa za mtu husika
mwenyewe. Pengine ni fundi umeme. Sasa akiwa yuko juu ya nguzo akateleza na
kuanguka, kwa bahati mbaya akaangukia sehemu mbaya. Kumbe inaweza kumpelekea
katika kifo. Wakati mwingine watoto wanapenda kukwea juu ya miti yenye matunda
misimu yake ikifika. Sasa inatokea wakati fulani akiwa amekwea anakanyaga tawi
vibaya au tawi alilokanyaga bila kujua likawa limeshakauka. Mwisho wa siku anajikuta
ameshashuka nalo chini. Na pengine mazingira ya pale chini yakawa hayako
vizuri, basi anapoanguka vibaya basi inaweza kumpelekea katika kifo.
3 Vita
Kinyume cha vita ni amani. Kwa hiyo,
kwa maneno mengine vita ni ukosefu wa amani. Kumbe vita inaambatana na utumiaji
wa nguvu kupita kiasi (yaani silaha). Vita kwa yenyewe siyo kitu kizuri, kwani
mara zote inaenda sambamba na umwagaji wa damu kwa watu wasio na hatia au wenye
hatia. Licha ya kwamba katika maadili inaongelea katika sababu yenye haki, basi
kwa haja ya hali ya kujihami n akujilinda basi itumike. Lakini katika yote,
licha ya sababu inayotambulika hata kimaadili. Bado vita lazima ihusishe
mauaji. Kwa mfano wa vita ya kwanza ya dunia mwaka 1918, pia tazama mauaji ya
kimbari (Mauaji dhidi ya Wtutsi) kule Rwandwa kati ya 7-04 mpaka 15-07 mwaka
1994. Sasa takribani watu 500,000 mpaka 1,000,000 waliuawa. Kati yao asilimia
70 wakiwa Watutsi;[3] vita
zote hizi zilihusisha mauaji ya watu wengi sana. Tusiende mbali sana hata kwetu tukikumbuka vita ya Tanzania na Uganda
(Vita vya Kagera) dhidi ya Idi Amin Dada iliyodumu kwa muda miezi sita, kuanzia
mwaka 1978 mpaka 1979. Inasadikika takribani Askari wa Tanzania 373, Raia pia
takribani 1500 na Askari 600 miongoni mwa 3000 wa Libya nao waliuawa.[4]
Ilihusisha vifo vya watu wengi tu. Na katika hao wapo waliokuwa hawana hatia lakini
wengine walikuwa ni wenye hatia.
4 Mamlaka
Katika nchi basi serikali imetoa
dhamana kwa chombo fulani kushughulikia mambo kama hayo ya utoaji wa uhai. Kwa
mfano nchi ya Tanzania imetoa mamlaka
katika vyombo viwili kwa wale wanobainika kuwa waharifu. Kuna chombo cha
Mahakama, ambayo ndiyo inayotoa hukumu kwa watu wanaobainika kufanya makosa
makubwa. Lakini utekelezaji wa agizo la mahakama unafanya na chombo cha
Magereza. Kumbe, pale mtuhumiwa anapokuwa amehukumiwa kifo yaani kunyongwa na
mahakama; ni jukumu la Magereza kuteke agizo hilo kwa mujibu wa mamlaka
waliyonayo. Sasa utekelezaji wa mamlaka huo unapofanyika, basi hupelekea kifo
kwa mtuhumiwa.
5 Kujitoa mhanga
Tumekuwa tukisikia mashambulio
mbalimbali yanayotekelezwa na vikundi mbalimbali katika nchi fulani.
Mashambulio haya ndiyo kusema kwa lugha nyingine ugaidi. Utekelezaji wa kujitoa mhanga huu
unawezakunywa na mtu mmoja, kwa kutumia silaha za miripuko; ambapo anatekeleza
shambulio hilo la kujitoa mhanga akiwa katika mazingira ya kuzungukwa na watu
wengi. Ni dhamiri ya kuwa kwa kutenda hivyo anajikuta kajiua na kuwaua wengine
wengine. Kwa mfano tumekuwa tukisikia vikundi kama Alshababu kule Nchini
Somalia, Boko haram kule Nchini Nigeria, Alkaida na vingine vingi. Ambavyo mara
kadhaa vimekuwa vikiripotiwa kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga katika njia
kadhaa. Kumbe kwa kitendo cha kujitoa mhanga tayari kinaambatana na mauaji ya
watu.
6 Umri mkubwa
Hiki ni kifo cha asili (natural death).
Kama tujuavyo kuwa uhai tumepewa na Mungu na unatoka kwa Mungu. Vivyo hivyo na
maisha yetu yote yako kwa Mungu, kwani ndiye ajuaye ni katika umri gani basi
tutapaswa kuyiacha dunia hii. Kwa hiyo, siyo wote walioandikiwa kufikia uzeeni,
bali wale wachache. Sasa unapokutana na Mzee kabisa aliyekula chumvi ya kutosha, yaani aliyefikia
hatua ya kulelewa kama mtoto maana hajiwezi kwa lolote. Basi anapokufa tunaona
kuwa ni kama haki yake, kwani umri wenyewe unaruhusu. Na watu wa namna hii mara
nyingi huwa wanakufa wakiwa usingizini. Yaani kabla ya kulala mmeagana vizuri
na hakuwa na tatizo au ugonjwa, ila asubuhi mnaamka kwenda kumjulia hali
mnakuta ameshakufa. Kumbe umri unapokuwa wa kutosha basi mwisho wa siku zile
seli nazo zinachoka mpaka kufikia hatua ya kutojiweza, hatimaye kupelekea kifo.
7 Majanga ya asili
Majanga ya asili wakati mwingine
tunajitafutia vifo kupitia yenyewe aidha kwa kutokujua au kwa kujua. Kwa mfano
mtu anaamua kwenda kujenga bondeni ambapo anajua mafuriko yakitokea hawezi
kubaki salama, lakini anapoambiwa na kutahadharishwa ya kuwa anapaswa ahame ila
yeye anabakia huko. Yakumkuta yakifika licha ya kuwa ni majanga ya asili lakini
yeye kajiweka katika mazingira ya kukumbwa na matatizo. Kuna majanga ya
kumbunga, tetemeko la ardhi, Tsunami, njaa, ukame pia miripuko ya Volkano. Haya
yote ni baadhi ya majanga ya asili, hivyo yanapotokea kwa hakika hayawaachi
watu salama. Kuna baadhi wanaenda nayo, yaani kifo kinawakabili. Hatuwezi
kuyaepuka kwa kweli zaidi tunaaswa tu kuchukua tahadhari. Kwa mfano tetemeko la
ardhi lililotokea mkoa wa Kagera mwaka 2017 lilisababisha maafa makubwa, watu
kupoteza nyumba zao na mali zao pia wengine walipoteza maisha (walikufa).
8 Kifo cha maamuzi binafsi
kuna watu tumekuwa tukiwaona au kusikia
au hata kushuhudia wakipoteza maisha aidha kwa kujitakia au kwa kutojitakia.
Wale wanaojitakia ni kama wale wanaofikia hatua ya kukata tamaa ya kuishi, na
mwisho wa siku wanaamua kuchukua uamuzi aliouchukua Yuda Iskalioti wa kujiua
kwa kujinyonga. Sasa watu wa hivi mimi nawatazama katika mwono huo, ya kuwa
wamejitakia. Lakini kuna wale wanakufa bila kujitakia. Kwa mfano unasikia mambo
ya utoaji mimba ambao ni dhahiri ni kuuwa tu. Au mwingine anajifungua vizuri
mtoto lakini mwisho wa siku anaamua kumtupa chooni au kichakani. Hicho nacho ni
kifo cha mtu asiye na hatia na hakujitakia.
[1] Rej. Richard A. Kungi, Kupata nguvu Saa ya Majonzi, Maana na
Uponyaji katika Kifo cha Umpendaye, FGD Tanzania Limited, Dar es salaam,
2018, uk. 4-12.
[2] Ludwig OTT, Fundamentals of Catholic Dogma, J. C. Bastible (ed), P. Lynch
(trans.), Tan books and Publishers, Inc, Rockford, 1960, uk. 96-100.
[3] WIKIPEDIA- Rwanda
genocide, https://en.m.wikipedia.org/wiki/Rwanda-genocide, retrived on
12/05/2019.
[4] MWANANCHI, https://www.Mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Yusufu-Lule-aondolewa-madaraani-30/1597296-4925576-format-xhtml-uwyeepz/index.html, recited on 12/05/2019.
No comments:
Post a Comment