BAADHI YA MAMBO YANAYOJERUHI FAMILIA
MAGONJWA NA ULEMAVU
Kuna baadhi ya Familia ambazo zimejeruhiwa kutokana na mmoja kuwa na magonjwa hatarishi na yasiyoponyeka au mmoja kuwa mlemavu.
Au mmoja wa wanandoa anajiingiza kwenye ulevi wa pombe na madawa ya kulevya au kujiunga na madhehebu hivyo kwamba analazimika kubadili mfumo wa maisha.
Katika hali kama hizo umoja na muungano wa wanandoa husika unaingia matatani. Kwa kawaida wanawake ndio wanaodhurika zaidi, kwani mwanamke aliye mgonjwa anaweza kurudishwa nyumbani kwa wazazi na ndugu zake apate kuuguzwa huko.
Katika hali kama hiyo unakuta kwamba mwanaume anaingia kwenye mahusiano mapya na hata kuoa tena.
UKOSEFU WA UAMINIFU KATIKA FAMILIA
Papa Francis akiongea juu ya Familia anasema,unaweza kubaini jinsi ambavyo watu wanaweza kujiingiza katika mahusiano kadhaa pasipo kusita wala kuona shida.
Watu wanaweza kuendelea kubadilisha mahusiano kama vile wanabadilisha mashati au magauni.
Mahusiano leo hii yanafananishwa na mitandao ya kijamii, kana kwamba upendo unaweza kuunganishwa au kutounganishwa kadiri mtu anavyojisikia au kupenda na vivyo hivyo mahusiano yanaweza kuanzishwa na kusitishwa kadiri ya mmoja anavyowaza na kusukumwa na mihemko yake.
Leo hii mahusiano yanajengwa juu ya matumizi kama vile tunavyotumia vitu au mazingira, na hili linadhalilisha utu na thamani ya ubinadamu wetu.
Kutokana na dhana ya matumizi ya vitu na mazingira, baada ya kumaliza matumizi yake, basi kinachofuata ni kutupa vile visivyofaa tena. Kwa hiyo watu leo hii wanatumiwa na kutupwa, wananyonywa na kudhulumiwa utu wao, wanapimwa kwa vigezo vya ubora wa kufaidiana na kama hakuna kufaidiana basi tunaagana.
Baadhi ya mateso na mahangaiko mengine katika ndoa ni kukosekana kwa uaminifu, vurugu, uongo na manyanyaso, mapenzi holela na ya tamaa kwa mmoja wa wanandoa.
Kuna Familia ambazo zinajikuta pia zimesambaratishwa kutokana na uwepo wa vita, kifungo magerezani au kazi. Familia nyingi zinateseka kutokana na ile hali ya vurugu, vita na uhamiaji.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255755552538
No comments:
Post a Comment