Tuesday, February 4, 2020

USIOGOPE HISIA ZAKO, MWACHIE MUNGU

USIOGOPE HISIA ZAKO! RUHUSU UZIMA WA MUNGU UCHANUE NDANI YAKO.

Samehe nawe utaishi ukifurahia maisha. Kuwa na furaha hakumaanishi kuogopa hisia zako, ila kuweza kuongea juu ya hisia na hali yako binafsi.

Ni kujiongelea nafsi katika hali ya utulivu ili kubainisha kile kinachoendelea nafsini mwako, chimbuko, mwendelezo, athari na hatima yake.

·  Ni ujasiri wa kuwa tayari kujisikiliza mwenyewe hususani inapobidi kusema “Hapana” kwa hili au lile unapopima mwenendo mzima na athari zake katika maisha yako na wale wanaokuzunguka.
· Ni uthabiti na utayari wa kusimama imara wakati wa kukosolewa, kushushuliwa au kuhukumiwa pasipo haki.
·  Ni katika kuwabusu watoto au ndugu zako, kuwakumbatia wazazi wako, kuwasherehesha marafiki zako ukiwaimbia mashairi hata pale ambapo wanatuudhi na kutukejeli.

Kuishi maisha ya furaha ni kuruhusu ule uzima ulio ndani yetu uchanue katika hali ya kawaida, uhuru na ufurahivu. Ukomavu wa kweli ni pale ambapo tunaweza kwa ujasiri

· Kwenye mahusiano kukiri kwamba “Nimefanya makosa.”
· Kuomba radhi pasipo unafiki tukisema “Samahani ndugu, niwie radhi.” Mnijalie nafasi nyingine ya kujirekebisha.
· Kutambua uwepo wa wengine na kuwaalika katika maisha yako unaposema “Ninahitaji msaada na uwepo wako.”
·  Ni kuweza kuwaahakikishia wengine ukiwaambia “Ninawapenda mno.”

Kwa yule aliyefikia upeo huu kimaisha, hakika yeye ni bustani yenye fursa za furaha kwa nafsi yake wenyewe na kwa jirani yake.

Kila wakati wewe utakuwa ni chimbuko la furaha, usitawi, uvumilivu, utulivu nafsi, amani, busara na hekima, na unapokosea utaweza kujifunza na kuanza maisha upya tena.

Ni katika ukweli huo, utaingia kwenye mafungamano ya upendo wa kweli na Mwenyezi Mungu, Nafsi, jirani na uumbaji wote. Utagundua kwamba kuwa na furaha sio suala na kuwa mkamilifu kimaisha,

·Ila kutumia machozi kumwagilia ugumu wa nafsi na kujifunza kuwavumilia wengine
·Katika unyenyekevu unajifunza kwamba katika kupoteza na kukosa kujifunza  saburi na kuwahitaji wengine.
· Kutumia makosa yetu kujizamisha katika utulivu wa ndani.
· Kujifunza kuteseka pasipo chuki.
· Kutumia makwazo kama mlango wa kufunguka kiakili.

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538
Itaendelea

No comments: