Tuesday, February 4, 2020

JE, TUNAWEZA KUSAMEHE NA KUSAHAU?

JE, TUNAWEZA KUSAMEHE NA KUSAHAU?

Kuna bado sintofahamu kubwa kuhusu maana halisi ya kusamehe. Mara nyingi watu husema “Samehe na Sahau” lakini inawezekanaje kusahau tukio lililotuachia majeraha makubwa vile.

Msemo huu hauna uhalisia katika maisha ya kawaida. Tunawezaje kusahau majeraha yale, wakati makovu yanabaki tukitembea nayo?

Tunawezaje kusahau maangamizi ya kinazi –Holocust au bomu la Hiroshima, au mauaji ya kimbari huko Rwanda mwaka 1994 ilingali bado watu wanaendelea kuathirika?

Nishawishike tu kusema kwamba tunahitaji “kusamehe na kukumbuka” ili uovu ule usitendeke tena.[1]

Lakini kosa si kosa. Mmoja anaposamehe siyo kwamba anafungua mlango wa magereza. Mmoja anaweza kusamehe na kuona haki inatendeka. Msamaha ni maridhiano na maelewano pasipo kupuuzia mizani ya haki. Tunachofanya ni kubadili namna ya kukumbuka, hali isiyoibua hisia za hasira, bali unyofu na kuchukua tahadhari.

Kusamehe siyo kusahau. Kutoka utotoni, tunafundishwa kusamehe na kusahau. Huu siyo uhalisia wa mambo na siyo sahihi kufanya hivyo, ila ni kujidanganya na kujihadaa. Ni sawa na mbuni kufukia kichwa kwenye mchanga akidhani kwamba hakuna anayemwona. Kwa mfano, kama msichana anasahau njia hatari ambapo kuna Baa na walevi wengi, tena mahali ambapo aliwahi kudhalilishwa kijinsi au kubakwa zamani, na kwamba inawezekana akatembea katika njia ile, ili achukue tahadhari huko ni kupotoka.

Mara nyingi tunajifunza kutokana na maang’amuzi ya zamani yaliyo mazuri au mabaya, kwa hiyo kusahau matukio ya zamani siyo kusamehe ila ni kuyagandamiza.

Tunaweza kuyakumbuka matukio hayo bila kushutumiwa kwamba hatujasamehe. *Lengo na nia ni kuchukua tahadhari ili tusiwe sababu ya kuwaumiza au kuruhusu kujeruhiwa tena.*

Kumbukumbu ya matukio ya zamani, hata kama ni hasi kiasi gani,  yanatuwezesha kuchukua tahadhari na kuwasaidia wengine wasije wakaingia katika shida ile ambayo sisi tumeipata.

Ni kumbukumbu ambayo haiamshi chuki, bali unyofu na utegemezi wa Mungu, tukijua kwamba sisi tunabaki viumbe dhaifu.

[1] Forgiveness puts the final seal on what happened that hurt you. You will still remember what happened, but you will no longer be bound by it.

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
Jipatie nakala ya kitabu changu juu ya haya

No comments: