Tuesday, February 4, 2020

FAMILIA TAKATIFU NI DARASA

FAMILIA TAKATIFU NI DARASANI

Inapendezaje kuona kila mwanafamilia akijifunza kutoka kwa Familia Takatifu (ya Yesu, Maria na Yosefu) namna ya kuishi kulingana na mpango wa Mungu.

Familia Takatifu ni kioo cha mafanikio ya utii kwa Mungu, heshima kwa wote, uelewano, umoja na mshikamano kati ya wanaFamilia.

Mwenyeheri Papa Paul VI aliwahi kusema: “Familia Takatifu ya Nazareti ikatufundishe umaana na thamani ya Familia, mshikamano wao wa upendo, ufukara na uzuri wa kujikubali vile walivyo, utakatifu na upekee wao.

Tujifunze kutoka Nazareti kwamba malezi na majiundo tunayoyapata kutoka kwenye Familia ni ya maana sana, kwani hutupa utambulisho wa kile tunachoweza kuwa, hadhi na heshima yetu, tena hayawezi kuachwa wala kupuuzwa tukabaki salama.”

Changamoto ni sehemu ya Maisha katika Familia.

Papa Francis, akitafakari Injili ya Luka 1: 16-38, anatuambia kwamba, Familia Takatifu ilikuwa na nyakati za hofu na mashaka, mateso na mahangaiko, ugumu na kuchanganyikiwa kama vile;

· Tunavyoweza kuonja kwenye tukio la kupashwa Habari Bikira Maria mwenye Heri (rej. Lk 1:26-38),

· Mashaka na mahangaiko ya Yosefu akiisha kufahamu kwamba mkewe ana Maria ujauzito nje ya taratibu za kawaida za Kiyahudi (rej. Lk 1:26-37),

· Safari kuelekea Bethlehemu, na kuzaliwa kwa mtoto Yesu horini (rej. Lk 2: 1-7),

· Katika mahangaiko ya kifamilia tunafahamu fika kwamba Familia Takatifu ilikimbilia Misri kumwokoa mtoto Yesu (rej. Mt 2:13-14)na tena walikuwa na wakati mgumu walipogundua kwamba mtoto Yesu hekaluni (rej. Lk 2:41-51).

Je hii ni hali halisi katika nyakati zetu hapa Afrika? Huo ndio ukweli wenyewe hata sasa. Katika mazingira yetu ya Afrika, tunafahamu kwamba Familia nyingi zinapitia kipindi kigumu pia kutokana na uwepo wa vita, mauaji ya kimbari, hali ya ukimbizi, ugaidi na matendo mengine yanayofiisha maisha ya Familia katika ujumla wake.

Tunafahamu mambo haya dhidi ya Familia sio mageni kwani hata Maandiko Matakatifu yanathibitisha hilo tangu mwanzo wa uwepo wa wanadamu. Tukisoma simulizi la Kaini kumuua ndugu yake Habil (rej. Mwa 4:1-16) tunaweza kuuona ukweli huo.

ITAENDELEA

JIPATIE KITABU CHA UTUKUFU WA FAMILIA KWA
MAFUNDISHO KAMILI.

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538

No comments: