Tuesday, February 4, 2020

MISA YA VIJILIA YA PASAKA C

MISA YA VIJILIA YA PASAKA

Mara nyingi tunahusianisha usiku au giza na uovu, tukisahau kwamba usiku na giza viko katika mpango ule wa uumbaji wa Mungu. Tukisoma kitabu cha Mwanzo, 1:31 kuna maneno mazuri… “Mungu akaona kuwa yote ni mema.”

Kutokana uelewa wetu wa Kiafrika kwamba usiku sio wakati mzuri, ni wakati wa maovu na kila uovu hufanyika katika usiku au katika giza, imani hii pia inatokana na kuathiriwa na imani ya ndugu zetu Waislamu kwamba usiku ni wakati wa majini, ni lazima tufikie hitimisho kwamba Usiku huu wa VIJILI ya leo ni Usiku wa pekee na wenye maana kubwa katika imani yetu.
· Mmeona tulianza na ibada ya Moto, kisha kubariki mshumaa wa Pasaka, kufukuzia mshumaa ule na moto mpya kabisa.
· Tumeingia Kanisani tukiongozwa na MSHUMAA wa PASAKA kuonesha kwamba Mwanga wa Kristo mfufuka unafukuza kila giza la dhambi.
· Tulipofika Kanisa, Mishumaa ingalipo inawaka tumeimba MBIU YA USHINDI- kisha
· Masomo 5 au/9 kuelezea safari nzima ya Upendo wa Mungu kwetu kama Muumba, Mtegemezaji na Mkombozi ambapo kazi nzima inapata ukamilifu wake katika Kristo wokovu wetu
Nukuu mbalimbali zinadhihirisha hilo
Mungu ni MUUMBA: “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26

TULIUMBWA KWA NEEMA YAKE:“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba,” Mwa 1:27

 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28

ISAKA NI ASHIRIO LA SADAKA YA KRISTO

“Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia,” (rej. Mwa 22:2)

“Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa22:12

“Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:17-18

NI MUNGU ANAYETUPIGANIA “Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake,” Kut 14:17

TUIMBE WIMBO WA SHUKRANI “Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1

KWARESMA TUMEMALIZA: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4

“Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu,” Rum 6:10-11

“Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka,” Mk 16:6

“Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7

Ni usiku ambao tunaonja kwa namna ya pekee ukamilifu wa Upendo wa Mungu katika mpango wa kumkomboa mwanadamu, tunathibitishiwa Uaminifu wa Kristo katika ahadi yake kwamba Atafufuka baada ya siku tatu. Huu ni usiku wa Pasaka ambapo ile huzuni yetu inaondoka na sasa tunaweza kuimba tena “UTUKUFU” na “HALLELUYAH”

Usiku huu ni wa pekee katika usiku wowote ule kwa sababu, huu ni Usiku wa Ushindi, ni Usiku wa Uhuru kutoka utumwa wa dhambi na minyororo ya shetani, ni usiku unaoeleza kilele cha historia yetu ya wokovu.

Njia iliyorahisi kuelewa na kuelezea tukio la usiku huu ni kutafakari kwa kina juu ya ujumbe upatikanao katika MBIU YA PASAKA
· Huu ndio usiku ambao nguzo ya moto iliangamiza giza la dhambi
·Huu ni usiku ambapo wale wenye kumsadiki Kristo wanatengwa na maovu ya dunia na giza la dhambi – wanarudishiwa NEEMA na kurudishiwa UTAKATIFU.
·  Huu ni usiku ambapo Kristo alikata minyororo ya MAUTI akatoka kuzimu kama MSHINDI kwa maana kuzaliwa kusingalitufaa kitu, tusingalikombolewa.

Wiki kadhaa zilizopita tulianza kile kinachoonekana ni safari ya huzuni, mkato wa tamaa na mateso mengi moyoni. Lakini ni katika usiku huu ile safari tuliyoianza imebadilika na kuhitimisha kwamba mambo yote furaha, amani, upendo, huruma na msamaha. Ukweli huo unajidhihirisha jinsi ambavyo tunaweza kuimba tena UTUKUFU na HALLELUYAH.

Lile wingu la GIZA zito lililofunia mioyo yetu sasa limefukuzwa na Mwanga wa Pasaka kwamba Mwanga huo umelishinda giza. Giza nene la Usiku halikuweza kuzuia Mwanga wa Kristo Mfufuka, ni kwa sababu hiyo tunaalikwa sote kuimba na kushangilia kwa nguvu zetu zote: “Alleluia, Alleluia, Alleluia kwa Bwana kwa sababu Bwana wetu Yesu Kristo ametimiza ahadi yake: “Nitafutuka siku ya tatu.” Kwa hiyo ndugu zangu yeye ni Jemedari asiyejua kushindwa, vita dhidi ya dhambi na shetani vimeisha kwa wote watakaopenda kuandamana na Bwana wetu Yesu Kristo, Yeye ni Mshindi – BWANA NA MWOKOZI wa wote watakaomsadiki.

Kwa ufufuko wake, katika Vijilia hii ya Pasaka, Yesu anatoa ujumbe muhimu sana. Yeye ni Bwana wa wazima na wafu, anao uwezo na mamlaka ya kutuponya na kutuweka huru. Tulikufa naye katika njia yake ya mateso wakati wa Kwaresma, na sasa tufufuke naye kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Ile nguvu iliyomfufua Yesu kutoka wafu, ni uwezo huo huo utakaotuwezesha sisi kufufuka kutoka katika giza na mahandaki yetu ya dhambi, kutuweka huru kutoka minyororo ya dhambi na utumwa wa shetani. Usiku huu ndugu wapendwa, Roho Mtakatifu ataiweka miili yetu huru katika udhaifu na unyonge wake (Rum 8, 11-12).

Usiku huu unafungua ukurasa mpya kwani Yesu wa Historia, aliyeteseka, aliyelia na kusulubiwa, aliyekufa na kuzikwa, sasa ni Bwana wa Utukufu asiyeweza kufa tena. Yeye ni Masiha, Bwana na Mwokozi wetu ambaye anatupenda na anataka sisi wote tuokoke.

Ni katika mantiki hiyo, kwamba Kristo Mfufuka ni UTUKUFU wa kila Muumini, tuna sababu ya kufurahi na kushangilia, ndiyo sababu usiku huu ni wa pekee kabisa. Ni mwaliko kwamba tuungane na mitume na kushuhudia kwamba: “Tumeuona Utukufu wa Kristo aliyefufuka. KRISTO TUMAINI LETU AMEFUFUKA – ALLELUYAH” tena kama mitume tunao wajibu mmoja tu “Sisi ni mashuhuda wa Ufufuko, tumekula na kunywa naye baada ya ufufuko wake kutoka wafu...”

Tangu sasa hatupaswi kumtafuta Kristo kati ya wafu, kwani hayuko tena huko, panieni yaliyo juu aliko Kristo. Tumtafute Kristo kati ya walio hai, tuuendee Mwanga ili giza la dhambi lisitawale tena mioyo yetu. Tubandukane na kila uovu, tusirudie tena matapishi ya dhambi kama nguruwe.

Uvueni utu wa kale na kuvishwa utu wa utukufu – utu mpya wa watakatifu na wateule wa Mungu. Kumbukeni thamani kubwa ambayo mlinunuliwa. Panieni, tangu sasa vitu vya thamani na wekeni hazina zenu mbinguni alipo Kristo. Mtume Paulo anasisitiza kwamba “Kwa kuwa mmerudishiwa maisha ya uzima katika Kristo, tafuteni mambo ya mbinguni alipo Kristo…”
Ndugu zangu, katika usiku huu mtakatifu, tuombeane, wale waliopo hapa na wale wasiokuwepo, tuiombee nchi yetu amani, furaha na upendo ili sisi wote tuweze kuimba na kushangilia Upendo, huruma, msamaha na amani ya Mungu kwa kila mmoja wetu. Ninawaombea nyote katika kilindi cha mioyo yenu mpokee zawadi hii ya utajiri wa upendo na amani ya Mungu kwa kila anayemwamini Kristo.

Huisheni Pasaka ya Kristo katika maisha yetu binafsi mkapate kuongoka na kuokoka. Kuweni watu wa shukrani daima na mashuhuda wa upendo wa Mungu katika kuenenda kwenu. Kumbukeni daima hamkununuliwa kwa thamani ya vitu viharibikavyo bali kwa damu ya Kristo. Uhuru tulioupata kwa Kristo ni uhuru unaotufanya WANA wa MUNGU – warithi na wadau Wenza katika Ufalme wa Mungu.

Kwa hiyo tuungane na mzaburi katika hii siku tukufu tukisema; “Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, tufurahi na kushangilia.” 
Alleluia, Alleluia, Alleluia! Amani ya Kristo mfufuka iwe nanyi

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)

No comments: