MADHARA YA KUTOKUSAMEHE
Kuna madhara kadhaa ikiwa hatusamehi waliotukosea. Hakuna lililo zuri katika haya kwani kila mmoja linatudhuru tena na tena:
1. Tabia ya kutokusamehe inasumisha mioyo yetu.
2. Kama hatuwezi kuwasamehe wengine, hatuwezi kujisamehe sisi wenyewe kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskarioti aliyeishia kujinyonga, na hii humaanisha ugumu wa kutaka kubadilika na kukua kufikia hadhi ya utu wetu. Katika hili mahusiano, maridhiano na upatanisho haufikiki.
3. Ikiwa hakuna mapatano na maridhiano, mahusiano yetu yanakuwa huzuni na hatima yake hutupelekea kifo cha nafsi, kiroho na hatimaye kimwili.
4. Chuki, hasira, huzuni, hisia za kulipiza kisasi ni kama kipindupindu, husambaa kwa wengine na hivyo kusumisha jamii kiasi cha kufikia mauaji ya kimbari kama ilivyotokea huko Rwanda na kwingineko ambako tunashuhudia mauaji ya aina hiyo.
5. Kutokana na maumivu makali ya kihisia, ni vigumu mtu kuwa na marafiki na kila karipio au kemeo ambalo linatolewa hata kwa nia njema ya kumrudi mtu, hutafsiriwa kama mashambulizi yasiyovumilika. Ndio maana, mhusika saa zote amevaa “zuio-helmet” na amejishehenisha mabomu ya litania ya matusi na malalamishi hata kwa wasiohusika kama namna ya kujihami.
6. Asiyesamehe ametengeneza uwanja wa mashambulizi katika nafsi na mwili wake. Ni mawindo wa magonjwa ya kila aina. Mioyo yetu haiwezi tena kuvumilia changamoto za kawaida. Tunaugua kila aina ya teso na jaribio. Kinga ya mwili inadidimia na hata inakwisha, hawa ndio wanaokuwa mabalozi mahospitalini maana hawaishi kuhuduhuria kila kukicha licha ya kwamba vipimo vinaonesha kwamba wao ni wazima.
7. Ni kovu la baadaye. Mmoja anapotambua kuwa, kwa kuwa hakujua kusamehe anajihukumu pia kwamba Mungu hawezi kumsamehe. Kwa hiyo kuna mkato wa tamaa na hatimaye kupoteza maisha ya sasa na baadaye.
8. Ingawa wanaweza kujihesabia haki, kimsingi wanaendelea kukosea na hata kuwaumiza wengine kwa kutokuwa tayari kuwasamehe waliowakosea. Wanapotambua kuwa hawawezi kulipa kisasi ipaswavyo, wanaumia zaidi.
9. Maisha kila siku ni msiba na matanga: Furaha zote za maisha ambazo walistahili kuzifurahia zinageuka kuwa matanga na huzuni kali.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
No comments:
Post a Comment