Tuesday, February 4, 2020

MUNGU ANATUPENDA VILE TULIVYO

MUNGU ANATUPENDA VILE TULIVYO

Ukweli ni kwamba tunaposema ya kuwa Mwenyezi Mungu ananipenda kwa upendo wa milele, upendo usio na mipaka au masharti, hatumaanishi kwamba hawapendi wengine.

Ni kwa pendo lile lile anadhihirisha upekee wa kila mmoja wetu, na ndio maana Amri kuu ni kumpenda Mungu na Jirani. Huo ndio ukamilifu wa sheria na manabii. (rej. Isa 19:16-25).

Ni kwa upendo wake Mungu juu yangu, aliweza kumtolea mwanae wa pekee awe sadaka fidia kwa ajili ya kunipata mimi nilipoanguka katika dhambi. Kwa pendo hilo tumerudishiwa uzima wa milele. Yesu alinipenda na kuyatoa maisha yake kwa ajili yangu.

Ukweli huu unapokuwa ni maang’amuzi ya maisha kupitia msukumo wa Roho Mtakatifu, hakika maisha yangu yanabadilika kwani Kristo anakaa ndani yangu nami ndani yake.

Upendo huu hauna masharti wala mipaka. Upendo kwa mdhambi, adui, mwana mpotevu aliyetapanya mali na urithi wa Baba yake.

Mungu ananipenda kwa pendo hilo. Upendo wa masharti sio upendo, na hilo sio pendo stahiki la Mungu.

Huo ni upendo ambao hatustahili ila watokana na ukarimu unaoendana na makusudi ya Mungu kutuumba sisi.

Mwana mpotevu alitambua kwamba hakustahili pendo la baba ila maonyo na adhabu, lakini anachokutana nacho ni kile ambacho kilimwacha hoi akibubujikwa na machozi mabegani mwa Baba anayemliwaza, akiwaalika watumishi wake kumvika mwanae huyo vazi liliko bora, viatu na pete.

Baba anayewaalika watumishi wake kuandaa karamu kubwa kwa ajili ya huyu ambaye alikuwa amepotea sasa amepatikana, huyu ambaye alikuwa amekufa sasa amefufuka.

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea....

No comments: