DOMINIKA YA 5 YA KWARESMA MWAKA C
Somo la kwanza: Isaia 43:16-21
Somo la pili: wafilipi 3: 8-14
Injili Yh 8:1-11
ACHILIA MAWE YAKO, MUNGU AKUTENGENEZEE NJIA.
Mapendooo sanaa.
Somo la kwanza linatoka
katika sehemu ya pili ya kitabu cha nabii Isaia.
Katika sehemu hii nabii isaia anawatangazia waisraeli kuwa watapata uhuru na watarudishwa katika mji wao na nchi yao. Mungu anaahidi kuwatoa utumwani.
Somo hili linatukumbusha kuwa kipindi hiki cha kwaresma ni wakati wa kutoka katika utumwa wa dhambi na kurudi kwa Mungu. Jumapili iliyopita tulisikia waisraeli walifika katika nchi ya ahadi, ila waliacha kumwamini Mungu na wakaanza kutegemea mataifa mengine.
Mara ngapi na sisi tunawategemea wanadamu kuliko Mungu? Tunashindwa kumwona Mungu katika maisha yetu.
Waisraeli wanapofika nchi ya ahadi wanamsahau Mungu aliyewatoa misri,wakamsahau alivyowaongoza kwa miaka arobaine. Hata sisi tunashindwa kuishi kulingana na masakramenti na viapo vyetu. Katika somo la kwanza, MUNGU anajidhihilisha kwetu kama Mungu mwenye nguvu anayetengeneza njia pasipo na njia. Kumbuka waisraeli walipotoka misri walifika mahali njia yao ikafika mwisho, mbele ni maji nyuma ni adui. Sasa wafanye nini?
Ndipo Mungu akawatengenezea njia pasipokuwa na njia. Mara nyingi katika maisha tunajikuta kama waisraeli tukishindwa kusonga mbele au kurudi nyuma, mbele changamoto, nyuma changamoto, kila kona changamoto ila ninachokiamini ni kwamba Mungu anaweza kututengenezea njia pasipo na njia. Wakati mwingine tunajikuta tumezungukwa na changamoto za maisha hatujui tufanye nini.
Tukitafuta suluhisho hatupati, ila Mungu hajabadilika tunapomtumainia anatuonyesha njia ya kutokea. Katika somo hili Mungu anasema atatenda jambo jipya, ndio ndugu zangu, MUNGU anataka akufanyie jambo jipya, kuna kitu kipya Mungu anataka akifanye katika maisha yako , yawezekana ni Leo, yawezekana ni wiki hii au mwaka huu lakini Mungu Leo ameapa atatenda kitu, atafanya jambo jipya kwetu.
Tumruhusu afanye jambo jipya katika Familia zetu, Jumuiya zetu, ndoa zetu, maisha yetu nk. Siku inakuja pia ambapo hata wanyama watafurahi.
Watakula na kunywa pamoja na wanadamu kama ilivyokuwa mwanzoni. Mungu anataka aturudishe kwenye bustani ya Edeni kwenye amani na Furaha kama ilivyokuwa mwanzo.
Yesu katika somo la injili anamsamehe mwanamke aliyeletwa kwake kwa kosa la uzinzi. Tumesikia kwamba Yesu alikuwa Hekaluni akifundisha, Mara huko nje ikatokea vurugu, watu wanasema mpige, muue, mpeleke kwa mwalimu, mzinzi huyu, hafai huyu na hatimaye wakamleta kwa Yesu wakasema. Mwalimu mwanamke huyu amefumaniwa akizini na Musa alisema, wanawake sambuli hii ni wakuua tu, wewe unasemaje?
Ila niliposoma walawi 20:10 nimeona sheria hii ni tofauti na wanavyoeleza. Sheria inasema; kama mwanaume amefanya uzinzi na mke wa jirani wote wawili wanatakiwa kuuawa.
Lakini pili wanapofumaniwa walitakiwa wapelekwe kwa kuhani na pia ushahidi uwepo. Tatu kuhani alitakiwa aandike chini walichokifanya halafu hukumu itolewe.
Sasa katika somo la Leo hawa Mafarisayo wanapindisha sheria. Kwanza kabisa wanasema amefumaniwa ila hawasemi nani aliyemfumania na hivyo hakuna ushahidi, pili wanamleta mama peke yake, je, alikuwa akizini peke yake?
Mafarisayo walitaka kupindisha sheria ili labda kufunika maovu, yawezekana alifumaniwa na mtu mkubwa au na farisayo mwenzao, au pia wanamsingizia.
Mara nyingi na sisi huwa tunapindisha sheria kutetea dhambi. Eti sijaiba nimechukua tu, sijatamani nimeangalia tu, nimeongea uongo mtakatifu, ndugu yangu acha kupindisha sheria katubu.
Ila Mara nyingi tunaona akina mama wanaonewa sana, Mara nyingi msichana anapopata mimba tunamuona ni mzinzi na kusahau kuna jamaa amezini nae, anapotoa mimba tunamuona mwanamke ndiye mbaya na kusahau yupo jamaa aliyempa hela ya kutoa mimba, yupo Dokta aliyemsaidia kutoa, wapo marafiki waliomshauri nk. Ila sasa Mara nyingi akina mama ndio wanaoonekana wabaya.
Ifike wakati tuanze kuwasaka wanaowaharibia mabinti maisha, sitashangaa kuona wamo kanisani tena hata kwenye kwaya wanapiga steps kama kawaida. Ila na nyie wanawake msijirahisishe sana, sio kila fursa unaichangamkia, wengi ni matapeli wa mapenzi.
Jamani vijana, ifike sehemu mpande bei, kijana usiwe mtumba kila mtu anakushika na kukutupa chini. Panda bei ili anayekusogelea ajue dhamani yako. Pandeni bei jamani. Yawezekana hata huyu mama ilikuwa ni Mara yake ya kwanza sema tu hakutaka kupanda bei.
Huyu mama anapopelekwa kwa Yesu, tumesikia Yesu anaandika chini, hakuna anayejua aliandika nini isipokuwa wengi wanasema aliandika dhambi zao kama ilivyoanfikwa katika yer 17:13. Dhamiri zao zilipowasuta waliachia mawe yao wakaondoka kwa aibu kuanzia wazee .
KWARESIMA ni kipindi cha kuachia mawe ya dhambi. Embu angalia ni jiwe gani ililolishikilia, achia Leo mawe ya uzinzi, wizi, umbea, ulafi, uongo nk. Kila mtu ana jiwe lake achia.
Lakini pia, nilipotafakari sana somo la Leo, nimeona afadhali wakati mwingine kuwa na maadui kama huyu mama kuliko kuwa na marafiki. Kumbe maadui wanaweza kukusaidia kumwona Mungu.
Najaribu kufikiria huyu mama alikuwa na mashosti wangapi, ila hakuna aliyewahi kumpeleka kwa Yesu ila hawa maadui zake.
Afadhali kuwa na maadui wakati mwingine wanaweza kuwa chanzo cha kuinuliwa kwako au chanzo cha kukutana na Mungu. Afadhali wao kuliko kuwa na marafiki buku ambao hawanafaida kwako.
Usiogope adui anaweza kukufanya umwone Yesu. Katika somo hili dhambi ninayo iona kubwa sio uzinzi wa mama, ila ni Mafarisayo kujiona wema wakati ni wabaya. Hii dhambi ni kubwa, kwa sababu ni dhambi ya kujidanganya sana.
Ndio maana Yesu akijua mioyo yao anawajibu; "kama hujawahi kutenda dhambi basi uwe wa kwanza kutupa jiwe." Hivi ungekuwepo ungetupa?
Hapo ndipo wazeee wakajitathmini wakaona miaka mingi wametenda dhambi, wakakumbuka Jana yake, wiki hiyo, mwezi huo, mwaka mzima walikuwa wakitenda dhambi wakaona aibu wakaondoka bila kuaga. Kama ni kupigwa mawe wangeanza na hao wakubwa.
Aliyebaki ni Yesu na Yule mama. Yesu aliye mwema na mama aliyesamehewa akawa mwema wengine hawafai kusimama mbele ya Yesu.
Wapendwa atakayesimama mbele ya Yesu ni Yule tu aliyesamehewa. Paulo katika somo la pili anasema; kwake mambo yote ni mavi yakilinganishwa na Yesu aliyempokea moyoni.
Paulo yuko tayari kuachilia yote ili abaki na kristo. Je, mimi na wewe tuko tayari kumtanguliza kristo katika maisha yetu?
Je, tunaona mavi yetu. Ifike sehemu tuseme, nyumba ndogo ni mavi, umbea ni mavi, kutoa mimba ni mavi, ulevi ni mavi. Tubaki na tutosheke na kristo kama Paulo.
Nawatakieni DOMINIKA njema ya kubaki na kristo.
Ni mimi ndugu Niliye mdogo kuliko wote.
No comments:
Post a Comment