Tuesday, February 4, 2020

FAMILIA ZILIZOJERUHIWA NA ATHARI ZA UTENGANO KATIKA NDOA

FAMILIA ZILIZOJERUHIWA NA ATHARI ZA UTENGANO KATIKA NDOA

Tunapoyatembelea Maandiko Matakatifu, tunakutana na uhalisia wa hali ya Familia kwa nyakati mbalimbali. Uwepo wa dhambi katika Familia umekuwa ni sababu ya mateso na mahangaiko mengi. Familia nyingi zinashuhudia uwepo wa mmomonyoko wa maadili, hujuma na manyanyaso baina ya wanaFamilia, ugaidi juu ya mazingira, ulafi wa uvunaji wa rasilimali ghafi kusikojali uwiano wa vizazi na uumbaji kumekuwa ni chanzo cha mateso mengi kwa Familia zetu.

Leo hii mwanadamu, kwa kisingizio cha maendeleo amekuwa ni chanzo cha maangamizi yake mwenyewe kutokana na kuongezeka kwa magonjwa, ajali, vita, na vurugu nyingine zinazomsibu mwanadamu. Kuongezeka kwa jangwa, ukame na uchafuzi wa mazingira unayaweka maisha ya wanaFamilia katika hatari zaidi kuliko viumbe vinginevyo vyote.

Mwanadamu amepoteza wajibu aliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu katika kuutunza na kuusitawisha ulimwengu kwa faida yake mwenyewe (rej. Mwa 3:17-19), kukosekana kwa uwiano wa kijamii na kiuchumi kumekuwa ni chanzo cha mateso ambapo Manabii wengi tangu Eliya (rej. 1 Falm21) mpaka Kristo wamekemea kukosekana kwa haki (rej. Lk 12:13; 16:1-31).

Familia tangu Agano la Kale, zimepitia kipindi cha mlolongo wa mateso na umwagaji wa damu unaojidhihirisha wazi katika mauaji ya Abeli yaliyofanywa na ndugu yake Kaini. Tunasoma pia juu ya mtafaruku baina ya watoto na wake mababu zetu Ibrahimu, Isaka na Yakobo, majanga na maafa yaliyoifika Familia ya Daudi, matatizo ya kifamilia yanayojidhihirisha katika Familia ya Tobia na malalamiko ya Ayubu:“Amenitenga na ndugu zangu…ndugu zangu na rafiki zangu wamenisaliti, ….” (rej. Ayu19:13-14, 17).

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538

No comments: