MSAMAHA NI ISHARA CHANYA YA KUJIHESHIMU AU KUJISTAHI
Kama tunataka kuwa na maisha mapya, tunahitaji kuwasamehe na kutafuta kusamehewa. Kama mwana mpotevu, katika Injili tunapaswa kuyazingatia moyoni na kumrudia Baba, na kueleza hisia zetu kwake, kisha kuuishi upendo wake usio na mipaka wala masharti, tukiamini kuwa Yeye ni mwingi wa Huruma na rehema, na kwamba yuko tayari kutusamehe, kwani kwake hakuna mipaka katika kupenda na kusamehe.
Tunapotambua madhaifu yetu na kukaribia kiti cha Huruma ya Mungu, Yeye anatualika na kutukumbatia, na Huruma yake haina ulinganifu.
Huenda baadhi yetu tunaona shida kujisamehe, lakini tunaamini kuwa Mungu atatusamehe. Tunahitaji kuamini kuwa upendo mkarimu wa Mungu unaodhihirishwa na Kristo.
Yesu anatutafuta sisi wadhambi, na anapotupata, kuna furaha kubwa mbinguni. Anatusubiri tumrudie. Kadiri tunavyotambua udhaifu wetu, ndivyo tutakavyokuwa tayari kuwapokea wengine katika madhaifu yao.
Jinsi tunavyojisamehe na kujipatanisha na mapungufu na mipaka yetu, ndivyo tutakavyowasamehe na kujipatanisha na wengine.
Ninakumbuka nilipomsubiri aliyenikosea aniombe msamaha, au kutambua kuwa alinikosea. Hili halikutokea. Nilijikuta ninashindwa kujitawala mwenyewe.
Baadaye nilitambua kuwa ninapaswa kujiruhusu kuona na kufungua moyo wangu kumsamehe aliyenikosea hata kama hajachukua hatua kuomba msamaha au kutambua kosa lake.
Hili linatudai kuwa na moyo mkarimu na mapendo. Ninawajibika kwa matendo yangu na namna ya kukabiliana na changamoto za mahusiano.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
No comments:
Post a Comment