DOMINIKA YA 4 YA PASAKA MWAKA C
Somo la kwanza: Mdo 13:14,43-52
Somo la pili: Ufn 7:9,14-17
Somo la Injili: Yn 10:27-30
WACHUNGAJI NI WENGI ILA KRISTO NI MCHUNGAJI MWEMA.
Tumsifu Yesu Kristo.
Wapendwa sana taifa la Mungu Leo ni Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema, na pia ni Dominika ya kuombea miito Mitakatifu ya Upadre na Utawa. Ndugu zangu, tunaishi katika ulimwengu ambapo kila kukicha anatokea Mchungaji, nabii, Askofu nk.
Ni kweli wachungaji ni wengi, ila naomba wanangu muwe makini sana kwa sababu Wachungaji wema na wa kweli ni wachache mno. Wengi mnaowaona wakipiga kelele mijini, ni matapeli na wafanya biashara.
Miezi michache iliyopita tulisikia Mchungaji mmoja huko Afrika kusini amemfufua mtu, ila baadae ikagundulika ulikuwa usanii tu, pia Juzi tulisikia tena Mchungaji mwingine alinywesha waumini Jik na kuua baadhi ya waumini wake. Ndio maana nasisitiza kusema wachungaji ni wengi ila wachungaji wema ni wachache muwe makini wanangu. Mchungaji mwema hatafuti sifa wala pesa, bali anatumikia kondoo zake tu. Kweli tunaowaona wengi wao wanatumikia?
Sifa moja ya mchungaji ni ujasiri, hata pale ambapo anakutana na vitisho anasimama imara katika imani yake. mazingira yanaweza kuwa magumu ila yeye huangalia kondoo na si vinginevyo. Je, hawa tunaokutana nao kila siku wana sifa hizi. Wewe jiulize kwa nini wamejazana mijini na si vijijini? Kwa nini wanajitangaza sana kwenye Tv na redio?Jibu unalo, naomba wakatoliki tusidanganyike tuwe imara.
Tusipokuwa makini tutanyweshwa mpaka mikojo na vinyesi. Ninaposoma somo la kwanza bila shaka naona kweli Paulo na Barnaba ni Wachungaji kweli wala sio wababaishaji. Walienda sehemu mbali mbali wakihubiri ukweli wa Kristo mfufuka. Walikutana na changamoto nyingi lakini hawakukata tamaa. Waliongea kwa ujasiri na kutetea ukweli.
Ndugu zangu tungekuwa na ujasiri kama huu wa kutetea ukweli, kutetea imani katoliki, kutetea ndoa zetu, bila shaka ingempendeza hata Mungu. Siku hizi watu wako tayari kuuza hata watoto, mke, Mume nk kwa ajili ya pesa au utajiri. Imani iko wapi? Msimamo uko wapi? Ifike sehemu tuwe na ujasiri wa kukataa dhambi na kusimamia ukweli kama Paulo na Barnaba. Hapo ndipo tutakuwa si wakristo tu, Bali tutakuwa wakristo wema.
Leo Dominika ya Kristo Mchungaji mwema, tunaalikwa tuwe wakristo wema, uwe mke mwema, Mume mwema, baba mwema, mama mwema, mtoto mwema, kijana mwema, mtawa au padre mwema. Ni Jumapili hakika ya kuwa wema. Katika somo la Injili Yesu ni Mchungaji mwema ambaye anasema anajua kondoo zake. Kumbe Yesu anatujua, anakujua wewe, anajua madhaifu yako kwa sababu ni Mchungaji mwema. Yeye anasema anajua kondoo wake, kumbe anakujua wewe, usihangaike sana na waganga nk anakujua sana, anajua njaa na kiu yako.
Kabla sijaendelea naomba nitoe mfano. Mtu mmoja alikuwa akichunga kondoo zake porini, kwa mbali akasikia sauti ya simba mkali na mwenye njaa. Mara moja akawaita kondoo zake na kuanza kuwaongoza waelekee Nyumbani ili kumkimbia Simba mkali. Ila alifika sehemu ambapo kuna Mto na hivyo kondoo wakashindwa kuvuka ule mto. Huku nyuma simba alikuwa anawafuata mbio ili awale. Sasa Yule mchungaji alijilaza juu ya Mto na kujifanya daraja, hivyo kondoo wakapita juu yake na kuvuka ng'ambo ya pili. Ila kondoo wa mwisho alipomaliza kuvuka tu, simba akawa amefika pale na kumshambulia Mchungaji ila kondoo wakapona wote. Mchungaji huyu ni Yesu Kristo aliyejilaza juu ya Mti wa msalaba ili sisi kondoo tuweze kumfikia Mungu Baba. Ndio maana hakika kristo ni Mchungaji mwema sana. Ila tunatakiwa tusikie sauti yake, lakini sio kusikia tu bali tuitambue. Sauti ni nyingi ila kondoo mwema ataitambua sauti ya Mchungaji wake.
Wewe unatambua sauti ya Kristo? Lakini tutaitambuaje, wakati hatuendi kanisani na Jumuiyani. Kama tuko mbali na Mungu sauti yake itakuwa ngeni kweli. Kwa mtu anayekaa mbali na kanisa, kila sauti kwake ni sawa tu haina tofauti. Sauti ya mchepuka sawa, wa waganga naaam, ya utapeli abeee yani kila sauti twende.
Sauti ya Kristo inatuongoza, inatukanya, inatuonya na pia inatutia nguvu. Ila kuna sauti za kukatisha tamaa, kukejeli, kurudisha nyuma, kupotosha nk tujiepushe na sauti hizi. Vijana wapendwa, huko mitaani sauti ni nyingi ila vhagueni sauti ya Yesu, hiyo inatosha kwa sababu inaelekeza. Tofauti ya Kristo Mchungaji mwema na wachungaji wengine iko wapi?
Kwanza Kristo anatangulia na sisi tunafuata nyuma. Kwa kawaida kondoo wanatangulia Mchungaji anakuwa nyuma. Ila kwa Yesu, yeye anatangulia na kondoo wanafuata nyuma. Ndio maana alimwambia Petro, rudi nyuma yangu. Wapendwa tumwache Yesu atangulie na sisi tufuate. Tuache kihelehele kama Petro, Mara nyingi tunakwama kwa sababu hatumruhusu Yesu atangulie. Kwenye kazi yako mwache atangulie, kwenye ndoa yako mwache atangulie tu, katika ujana wako mwache atangulie na wewe ufuate. Akitangulia pia atatuonyesha njia ya mbinguni, yaani njia ya kufika kwa Baba. Sisi peke yetu hatuwezi kufika. Yeye ndiye njia, uzima na ukweli.
Yesu hatubagui ndio maana katika somo la pili tunasikia waliokizunguka kiti cha enzi ni kutoka kila kabila, taifa na lugha. Wameshika matawi ya mitende ishara kwamba ni washindi. Wapendwa wa Mungu, watakaovumilia mpaka dakika ya mwisho bila kukata tamaa watakuwa washindi.
Biblia inasema hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena wala jua halitawapiga. Yaani mimi natamani kufika huko ni mwone Yesu wangu kama alivyo. Mungu atafuta machozi yote katika macho yao walioshinda. Hakika ni raha sana, tena kufutwa machozi na Mungu, sio Mtu ni Mungu mwenyewe.
Niliposoma somo hili nimetamani sana siku moja nifike huko. Najua wengi pia tunatamani, ila sio rahisi kunakupambana na hata kumwaga Damu pia. Tuutafute ufalme huu kwa gharama yoyote hata kama ni kwa kumwaga Damu.
Nawatakieni Jumapili njema ya kuutafuta ufalme wa Mungu.
Kaka Niliye mdogo kuliko wote
No comments:
Post a Comment