FAMILIA NI UFUNGUO WA GETI LA UTAKATIFU
Wapo baadhi ya watu wanaofikiria kwamba wito wa Utakatifu ni kwa ajili ya mapadre, wamonaki, watawa wa kiume na kike, na wale waliopokea zawadi ya wito wa kipekee ambao hawaoi au kuolewa.
Papa Mt. Yohani Paulo II anatukumbusha kwamba “Wanandoa na wazazi wanajumuishwa katika mwaliko wa kuwa watakatifu. Kwa ajili yao, wito huu wa kuwa watakatifu unatokana na maadhimisho ya Sakramenti ya ndoa na uaminifu wao katika viapo na upendo wa kifamilia.” (rej. Familiaris Consortio no. 56).
Papa Fransisko katika mausia yake kwa watu wote “Furahini na kushangilia” ya tarehe 19 Machi 2018 anatukumbusha tena kwamba “Tuna kishawishi cha kufikiri kwamba utakatifu ni kwa ajili ya wale waliotengwa na malimwengu wakitumia muda mwingi katika sala, ibada na maadhimisho ya kiroho. Huo sio ukweli halisi. Kila mmoja wetu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ameitwa kuwa mtakatifu kadiri ya maisha na shughuli tunazozifanya, yaani kuishi maisha yetu na kutoa ushuhuda wa maisha katika yale yote tuyafanyayo, na popote tunapojikuta.
Papa Francis katika mausia yake ya Utakatifu katika ulimwengu mamboleo anatukumbusha mambo ya msingi anaposema:
· Je, wewe umeitwa katika maisha ya wakfu? Uwe mtakatifu kwa kuishi viapo na maagano yako kwa furaha na amani.
· Je, wewe umeolewa au kuoa? Uwe mtakatifu kwa kuishi ukimpenda na kumjali mwenzi wako wa ndoa kama vile Kristo anavyolipenda Kanisa lake.
· Je, wewe ni mfanyakazi ili kujipatia riziki ya maisha? Uuishi utakatifu wako kwa kuzingatia weledi, ujuzi, ukweli, uadilifu, uwajibikaji, uaminifu na kwa haki katika kuwahudumia Familia, jamii na ulimwengu!
· Je, wewe ni mzazi, babu au bibi? Uwe mtakatifu kwa kuwajibika katika hali ya utulivu kuwafundisha wanao au wajukuu zako, na wote walio wadogo namna iliyobora ya kumfuasa Kristo, ukiifanya Familia yako kitalu cha maisha na uhai, shule ya mapendo na altare ya utakatifu.
· Je, wewe uko kwenye nafasi ya madaraka na mamlaka? Uwe mtakatifu kwa kutenda kwa haki na kwa manufaa ya wote ukijiepusha na kila aina ya ubinafsi, umimi na ufisadi.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538
No comments:
Post a Comment