MAAMUZI YA KUSAMEHE YANAHUSU: AKILI, MOYO NA HISIA
Msamaha ni ishara ya ukomavu wa kiimani. Katika maisha yote na katika safari ya kila mmoja wetu, msamaha ni zawadi kwa yule anayesamehewa kwani akiupokea msahama ule anahuishwa kwa ndani kabisa na kuruhusu kuumbwa tena upya.
Msahama ni zawadi kwa anayeuotoa kwani kwa kufanya hivyo anajihakikishia maisha ya furaha, amani, matumaini na mwingi wa afya njema.
Msamaha ni chaguo au ni hisia za kiroho, kutaka kuwa huru na mwenye afya. Haina maana kwamba tunadharau yaliyotokea na kuyafanya madogo ila tunataka kuanzisha mwendo mbadala wa maisha. Wapo waliofuga hasira, chuki, husuda na shauku ya kulipiza kisasi muda mrefu kutokana na kushindwa kusamehe na kuanza mchakato wa msamaha. Imewagarimu sana.
Msamaha ni majitoleo ya upendeleo yanayotolewa kwa yule aliyetukosea na fursa ya kuanza maisha upya tena. Ni kutoa nafasi ya pili, na kuruhusu mabadiliko.
Ni kutambua kuwa hakuna aliye mkamilifu, ni kuingia kwenye viatu vya yule aliyetukosea na kutambua kuwa hata sisi tungeliweza kukosea pia. Kila mmoja anafanya makosa, ni vema tukapeana nafasi ya pili kurekebisha mambo.
Ni kujifunza kujenga mahusiano bora yenye afya ya kimwili, kisaikolojia na kijamii. Kumsamehe mwingine kunadai utashi, utayari, kujisadakisha kwa mwingine na nguvu ya kuishawishi akili na moyo vikubali. Tunaposamehe tunaelewa kwamba hatuitaji hasira yetu na chuki kujikinga wenyewe (Si NGAO).
Hatuhitaji kuhifadhi hasira, chuki na husuda kana kwamba ni mtaji. Ndugu zangu, maang’amuzi ya maisha kwa wenye kutafakari kwa kina katika uhalisia wa mambo tunabaini kwamba, gharama itumikayo kulipiza kisasi ni kubwa kuliko garama ya kusamehe.
Mwaminini Mungu ambaye ni hakimu wa haki. Kusamehe ni njia hakika ya kupokea msamaha wa Mungu wakati ufaao.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
No comments:
Post a Comment