Tuesday, February 4, 2020

TAFAKARI DOMINIKA 5 PASAKA C

*TAFAKARI YA DOMINIKA YA 5 YA PASAKA, MWAKA C*

*Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Parokia ya Buhingo, Jimbo Kuu la Mwanza*

*0753 266 330*

*SOMO LA KWANZA: Mdo. 14:21b-27*

Katika somo la kwanza tunamwona Paulo na mshirika wake Barnaba wanaendelea kuhubiri habari za Yesu katika miji na vijiji. Kwa upande mmoja mahubiri yao yanazaa matunda kwani Wayahudi na Wayunani/Wagiriki wengi wanaipokea imani waliyohubiriwa na kuongoka. Kwa upande mwingine Wayahudi wasioamini (Wayahudi wakereketwa wa dini ya Kiyahudi) wanaona wivu na hivyo wanataka kuwaua Paulo na Barnaba ili habari njema ya Kristo isiendelee kusikika. Hata hivyo, mitume hawa hawakati tamaa. Kutokana na mateso wanayoyapata wao wenyewe, wanawafundisha wengine kuwa njia ya kuingia mbinguni si rahisi: _*“imetupasa kuingia mbinguni kwa njia ya njia dhiki nyingi”.*_ Wanatambua kuwa kuishi Imani yao na kumtangaza Kristo si lelemama, bali ni wajibu unaowadai kupitia dhiki/mateso: _*kudharauliwa, kupigwa, kupingwa, kutukanwa, kufungwa gerezani na hata kuuawa kwa ajili ya Kristo.*_ Na ni kwa njia ya mateso /dhiki ndiyo wataweza kuingia mbinguni. Hoja ya Paulo na Barnaba ni hii: *hatuwezi kuingia mbinguni bila kuteseka hapa duniani na hatuwezi kuishuhudia imani bila kukumbana na changamoto, mateso, dhuluma, kejeli na hata kuuawa.* Hata katika ulimwengu wa sasa wapo Wakristo wanapitia dhiki kubwa wanapotangaza na kuishi imani yao kwa Kristo. Mfano mzuri ni Wakristo wa Sri lanka, Nigeria, Burkinafaso na kwingineko ambao wanatishwa na hata kuvamiwa wakiwa makanisani na kisha kurejuhiwa au kuuawa. Dhiki/mateso haya wanayopitia siyo hasara bali ni njia/nyenzo inayowasaidia kuingia mbinguni. Kila mmoja wetu anazo dhiki zake: mateso/changamoto zinazotokana na ukristo wetu, changamoto za ndoa na familia, misiba ya kupotewa wapendwa wetu tuliowategemea katika maisha, majanga ya asili, magonjwa yasiyopona, mahangahiko ya uzee, usaliti katika mahusiano, na mengineyo. Haya hayakwepeki katika maisha. Tukiyabeba kwa jicho la imani yatatusaidia kuingia mbinguni. Je, mimi na wewe tunapokumbata na dhiki/mateso/changamoto zinazotokana na imani yetu kwa Kristo tunazitazama kwa jicho gani? Je, tunazipokea na kuziona kama njia/ngazi ya kwenda mbinguni? Mt. Rosa wa Lima anasema, _*“ngazi pekee itakayotuwezesha kufika mbinguni ni msalaba.”*_ Anaposema msalaba anamaanisha mateso, magonjwa, changamoto za maisha na imani, kejeli, kudharauliwa, misiba ya maisha, ugumu wa maisha na mengineyo. *Bila msalaba hakuna mbingu.* Dhiki zetu zisiwe sababu ya sisi kuogopa kumtangaza Kristo, kukata tamaa ya maisha au kuikana imani yetu. Mitume hawakuiacha imani kwa sababu ya dhiki/mateso waliyopitia. Kama Mitume walivyowaonya watu wa Listra, Ikonio na Antiokia wakae katika Imani, nasi pia tunapaswa kuwa imara na kukaa katika Imani licha ya dhiki/changamoto/mateso yanayotukabili.

*SOMO LA PILI: Ufu. 21:1-5a*

Somo letu la pili linatoka kwenye kitabu cha Ufunuo. Kitabu cha ufunuo kiliandikwa mwanzoni kabisa mwa ukristo ili kuwatia moyo wa ujasiri Wakristo ambao walidhulumiwa (kuteswa, kufungwa gerezani na kuuawa) kwa sababu ya imani yao kwa Kristo. Kutokana na madhulumu hayo, baadhi ya Wakristo walianza kuikana imani yao ili wasiteswe au kuuawa. Hivyo, kitabu cha ufunuo kinalenga kuwatia moyo Wakristo kuishuhudia imani yao kwa Kristo na hata ikibidi kuuawa kwa kuwa kuna maisha ya uzima wa milele katika ulimwenguni ujao (Yerusalemu mpya). Hili ndiyo lengo la somo letu la pili la leo.

Yohane, katika maono, anaona *“mbingu mpya, nchi mpya na Yerusalemu mpya.”* Maono ya “mbingu mpya na nchi mpya” ayapatayo Yohane ni utimilifu wa ahadi ya Mungu aliyoitamka kwa kinywa cha nabii Isaya (rejea Isaya 65:17). Hii ina maana kuwa uumbaji wote utafanywa upya. Katika maono haya Yohane anaona pia *“Yerusalemu mpya”.* Mji wa Yerusalemu, kwa Wayahudi, ulikuwa ni mji mtakatifu ambamo ndani yake kulikuwa na hekalu la Yerusalemu, hekalu ambalo ni makao ya Mungu. Hivyo, mji wa Yerusalemu ulikuwa ni kitovu cha imani na maisha ya kidini ya Wayahudi. Hata hivyo katika maono Yohane anaona “Yerusalemu mpya” inayoshuka kutoka mbinguni (siyo Yerusalemu asilia iliyopo Israeli). Je hii “Yerusalemu mpya” inawakilisha nini? _*Kwanza, “Yerusalemu mpya” inawakilisha Kanisa.*_ Kama Yerusalemu mpya inavyoshuka toka mbinguni, kadhalika kanisa asili yake ni mbinguni (lilianzishwa na Yesu Kristo aliyeshuka toka mbinguni). Ni katika kanisa ambapo Mungu anafanya maskani yake pamoja na watu wake. Ni katika kanisa ambapo tunafanywa kuwa watu/taifa la Mungu: “nao watakuwa watu wake”. Hivyo, tunapaswa kulitumia Kanisa kwa ajili ya kupata wokovu. _*Pili, “Yerusalemu mpya” inawakilisha mbinguni, makao matakatifu na kamilifu ya Mungu na miliki yake.*_ Yohane anaeleza mandhari ya hiyo “Yerusalemu mpya”: hakuna mauti, hakuna maombolezo wala vilio na wala hakuna maumivu. Je, maono haya ya Yohane juu ya “Yerusalemu mpya” yalikuwa na lengo gani? Lengo ni kuwafunulia Wakristo wanaokabiliana na madhulumu kuwa maisha hayakomei hapa duniani bali kuna maisha baada ya kifo huko mbinguni (yaani Yerusalemu mpya). Hivyo, hakuna sababu ya wao kuikana imani yao ili waendelee kuishi duniani ilihali ulimwengu huu na maovu yake vitatoweka. Wakristo hawapaswi kuogopa mateso au kuuawa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo. Wakiwa tayari kuishuhudia imani yao, licha ya madhulumu, wataingia mbinguni (yaani Yerusalemu mpya) na kuishi pamoja na Mungu maana Mungu Mwenyewe *“atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake”.* Katika hiyo Yerusalemu mpya (mbinguni) hakutakuwa tena na maombolezo na vilio, maumivu wala mauti kama yale nayowapata katika ulimwengu wa sasa (yaani hapa duniani) kwa sababu ya imani yao.

Ujumbe mkubwa wa somo letu la leo ni huu: _*kuishi imani yetu kwa uthabiti na ushuhuda wa kweli, hasa nyakati za mateso na misukosuko, ndiko kutatuwezesha kuingia mbinguni “Yerusalemu mpya” na kuishi na Mungu.*_ Swali la msingi ni hili: Je, mimi na wewe tuwapo katika mateso, misukosuko na misiba ya maisha tunabaki waaminifu katika imani? Je, tunatambua kuwa ulimwengu huu utapita na hivyo hakuna haja ya kujiambatanisha nao? Tafakari, chukua hatua.

*SOMO LA INJILI: Yn. 13:31-33a, 34-35*

Somo letu la Injili linatupatia ujumbe kuwa *“yatupasa kupendana kama Kristo alivyotupenda sisi”.* Ingawa bado tunasheherekea ufufuko wa Bwana (Pasaka), injili yetu ya leo imeturejesha kwenye Karamu ya Mwisho ya Yesu na wanafunzi wake. Alapo karamu na wanafunzi wake Yesu anajua wazi kuwa saa ya kuondoka hapa duniani (saa ya kifo) imekaribia. Kwa kawaida watu wanapokaribia kufa hutoa wosia kwa wale wanaobaki. Ndivyo Yesu anavyofanya leo katika Karamu ya Mwisho. Yesu anatoa wosia kwa wanafunzi wake: _*“Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.”*_ Kwa Kigiriki (ambayo ni lugha asilia ya Agano Jipya) yapo maneno mengi yanayotumika kuelezea aina za upendo kama vile *“philos”* (upendo wa kawaida wa kirafiki au kidugu) na *“eros”* (upendo wa hisia unaovutwa na sifa alizonazo mtu- sensual/physical love). Hata hivyo, katika wosia huu neno la Kigiriki linalotumika kumaanisha upendo ni *“Agape”* (yaani upendo wa kimungu- ngazi ya juu kabisa ya upendo): _*mpendane kwa upendo wa Agape kama mimi nilivyowapenda ninyi kwa upendo huo wa Agape- upendo wa Kimungu, upendo wa hali ya juu kabisa.*_  Katika wosia huu Yesu anasema kuwa hiyo ndiyo *“Amri mpya.”* Kwa kawaida huwezi kuwa na amri mpya kama hakuna "amri ya zamani." Je, *"Amri ya zamani"* ihusuyo upendo ni ipi? Ni hii: _*“Mpende jirani yako kama nafsi yako” (rejea Law. 19:18).*_ Sasa “Amri mpya” haisemi umpende mwenzako/jirani kama nafsi yako bali tupendane kama Kristo alivyotupenda sisi. *Kristo hakutupenda sisi kama nafsi yake bali alitupenda sisi zaidi ya kuipenda nafsi yake mwenyewe na ndiyo maana akawa tayari kuiangamiza nafsi/roho yake kwa ajili yetu:* “alitupenda upeo” (Yn. 13:1) na tena Yeye mwenyewe anasema, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn. 15:13). Katika Amri hii mpya kipimo cha upendo sio tena *“kupendana kama tunavyopenda nafsi zetu”* bali *“kupendana kwa upendo wa Kristo.”* Yesu anataka tupendane kwa upendo aliotuonesha sisi. Je, upendo wa Kristo ukoje? _*Ni upendo upeo, ni upendo wa kutoa uhai kwa ajili ya wengine, ni upendo wa kujitoa sadaka, ni upendo usiotazama mapungufu ya mtu, ni upendo usio na ubinafsi wala unafiki, ni upendo wa kuumia kwa sababu ya mwingine, ni upendo wa kujinyima ili mwingine afaidike.*_ Huu ndiyo upendo wa Agape ambao Kristo anatuasa tuwe nao. Upendo wa Agape umeelezwa kwa undani zaidi katika 1Kor. 13:1-13. Tukiwa na upendo wa Kristo watu wote watatambua kuwa sisi ni wanafunzi wa Yesu.

Katika Injili yetu ya leo kuna fundisho kubwa moja tu: *tunapaswa kupendana kama Kristo alivyotupenda sisi.* Wengi wetu tu wepesi kutamka neno “upendo” au “nakupenda” bila kujua maana na uzito wa neno hilo. Nimehangaika sana kutafuta maana ya neno “upendo”. Kamusi ya Ukristo iliyoandikwa na Jordan Nyenyembe imenipa mwanga. Kwa kadiri ya kamusi hiyo *“upendo ni hali ya kumpokea Mungu, binadamu wengine, viumbe na mazingira yote kwa moyo na kwa dhati kabisa.”* Je, tunapokeana sisi kwa sisi kwa moyo na kwa dhati kabisa? Je, upo tayari kumpokea (kumpenda) na kumvumilia mwezi wako wa ndoa licha ya mapungufu yake? Je, upo tayari kutoa uhai wako kwa ajili ya kuokoa uhai wa mwingine? Je, upo tayari kujinyima baadhi ya vitu kwa ajili ya kumsaidia/kumnufaisha mwingine? Je, upo tayari kumsaidia/kumpenda mwingine hata kama hunufaiki na kitu chochote kutoka kwake? Je, upo tayari kuumia/kuteseka kwa ajili ya mtu mwingine? Je, unaguswa na mahangaiko/mateso ya mtu mwingine? Kama upo tayari kufanya haya yote basi wewe una upendo wa Agape.

Wengi wetu tunapendana kwa sababu ya fedha, kwa sababu tunatoka kabila/mkoa mmoja, kwa sababu ya kukidhi tamaa zetu za mwili, kwa sababu ya hulka fulani zinazofanana, kwa sababu ya elimu, kwa sababu ya utajiri wetu au kwa sababu ya hadhi zetu katika jamii. Matokeo ya kupendana kwa misingi ya vitu fulani fulani ni kuwa upendo wetu hauwezi kudumu. Ni katika ndoa ngapi upendo umetoweka kwa sababu mume/mke amefilisika, hana pesa tena? Ni mara ngapi tumependana nyakati za furaha lakini tumeachana nyakati za shida? Ni wangapi waliwatamkia wachumba zao neno *“nakupenda sana”* lakini baada ya kufunga ndoa wanawatamkia neno *“nakuchukia sana”*? Ni wangapi wanajifanya wanapendana kabla ya kutimiziana haja zao za mwili lakini upendo/mapenzi yao yanakufa baada ya kutimiziana tamaa za mwili? Ni wangapi tuliwapenda walipokuwa na afya njema lakini walipougua tuliwatelekeza? Je, huo ndiyo upendo? Tupendane kwa moyo na kwa dhati kabisa tukikumbuka kuwa *upendo ni ukamilifu wa sheria* na ya kwamba upendo wa kweli hauna kikomo.

_*Dominika Njema*_

No comments: