MSAMAHA NI MAPATANO NA MARIDHIANO
Kupatana ni watu wawili kuja pamoja wakiaminiana tena. Hili linadai ushirikiano wa pande zote.
Mchakato huo unatudai kumfikiria mkosaji kama mtu mzima badala ya kumwona kama mdhambi, mtesaji, mkosaji, fedhuli, na mabango mengine ambayo tunaweza kuyatumia. Tutambue kuwa sisi ni zaidi ya vitendo vyetu.
Sisi ni watu dhaifu ambao tuna matarajio mengi maishani ya kufanya vizuri zaidi kila zinapoibuka fursa mbalimbali kimaisha, na moja ya fursa ni pale ambapo tumemkosea mtu kisha tukaweza kusuluhishana na kuhesabu hiyo kama hatua ya makuzi. Sisi ni wana wa Mungu.
Baada ya fikra chanya, tunapaswa kuwa na hisia za kusamehe (emotional forgiveness), kujiruhusu wenyewe tusukumwe kumhurumia na kumpenda huyu mwana wa Mungu aliyepotoka na kuniumiza. Hapa ni pagumu na inaweza kuchukua muda.
Neema ya Mungu na nguvu ya sala inafanya kazi katika hili na wanasayansi wanabaki midomo wazi katika hili.
Hapa tunapaswa kujua kuwa, kusamehe kuna madai ya sadaka: Kuvumilia maumivu yatokanayo na majeraha ya maumizo tuliyotendewa. Anayesamehe hawezi kurudi nyuma kufuta majeraha aliyotendewa. Makovu yale yanabaki.
Anachofanya sasa ni kuthubutu kwa ujasiri mkubwa kupokea hali ile, na kurejesha mema kwa aliyemtendea kwa ujeuri. Ni kuchukua mwilini mwetu mateso ya Kristo kwa ajili ya wanadamu.
Na kwa sababu hiyo, tunaadhibu uovu kwa wema, na huo ndio ushindi unaotupeleka katika Pasaka Mpya ya maisha yetu ya kikristo.
Kristo aliyavumilia mateso yetu nasi tukasamehewa. Na ni katika kuyavumilia mateso waliyotutendea wenzetu nao wanasamehewa.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
No comments:
Post a Comment