DOMINIKA YA 6 PASAKA MWAKA C
TUSIWE NA MISIMAMO USIYO NA MSINGI.
Somo la kwanza Mdo 15:1-2,22-29
Somo la pili ufu 21:10-14,22-23
Injili Yn 14:23-29
Tumsifu Yesu Kristo,
Katika somo la kwanza tunaona kanisa la kwanza liko katika mgogoro mkubwa. Sasa kuna wakristo wa aina mbili. Waliotahiliwa na wasiotahiliwa.
Somo linaeleza kuwa kuna watu ambao wametoka uyahudi na wanashikilia msimamo kwamba wapagani wanaotaka kuwa wakristo lazima watahiliwe kwanza ili wapate kuokoka. Hili jambo linaleta mgogoro mkubwa katika kanisa la kwanza. Je, ni sahihi kuwa na msimamo kama huu? Wapendwa kuna misimamo mingine sio lazima kuing'ang'ania.
Wayahudi walionyesha msimamo wao ambao kwanza kabisa sio wa msingi. Msimamo kama huu hauwezi kusogeza kanisa mbele ila kurudisha nyuma. Misimamo mingine inaweza kuleta migogoro katika Jumuiya, Familia au ndoa.
Wakati mwingine tunashindwa kusonga mbele kwa sababu ya misimamo ambayo haina msingi.kwa nini ndoa zinavunjika, ni kwa sababu labda Mume anamsimamo wake, Mke anamsimamo wake, wakwe wanamsimamo wao na hatimaye mgogoro mkubwa katika maisha ya Familia na ndoa. Embu jiulize ewe mke, mume, mkristo huo msimamo wako kweli ni wa msingi?
Kwamba ukioa lazima utambike, ukizaa lazima umtoe mwanao wa kwanza kwa mizimu, sijui kwetu tunafanya hivi, kwetu tunalala tukiangalia juu yani ndoa ina masharti mpaka basi. Kuna misimamo tunayotakiwa kuiacha ili tusonge mbele, ili Familia isonge mbele, ili Ndoa iwe na amani. Tukae tutafakari na kutupilia mbali misimamo ambayo haina msingi katika maisha. Wayahudi wangetupilia mbali msimamo wao wa kutahiliwa hakungekuwa na mgogoro.
Sasa, mgogoro ulipozidi, ndugu waliamua kuomba ushauri kwa Mitume, na ndipo walipowatuma Paulo na Barnaba, Yuda na sila kwa Mitume. Kumbuka Leo hii wanaoshika nafasi ya Mitume ni maaskofu.
Ndio maana hata Leo tunapokuwa na matatizo ya kiimani baraza la maaskofu huja pamoja na kuandika waraka wa kutuelekeza, kutukosoa au kutuonya kama walivyofanya Mitume.
Ndio maana kanisa ni takatifu, katoliki na la Mitume. Hii haina mjadala hata kidogo. Waliosuruhisha ni mitume, wakawaambia kuhusu kutahiliwa na kutotahiliwa si hoja. Ila wajiepushe na mambo makuu manne; chakula kilichotambikiwa vinyago, wasinywe Damu, wasile nyama iliyosongolewa na wajiepushe na uasherati. Hayo manne ndio ya msingi.
Ndugu zangu kama tungeweza kushika haya ya msingi, kama kwenye ndoa ungeweza kuepuka uasherati, kama kwenye Jumuiya zetu tungeacha kuwa na miungu mingine kama waganga wa kienyeji na ushirikina, wapendwa ingempendeza mungu. Mitume waliwaambia mkiachana na mambo hayo manne ni vema. Na mimi na sema tukizingatia mambo ya msingi katika imani yetu ni vema na ni baraka.
Bila shaka hawa mitume waliongozwa na Roho Mtakatifu kwa sababu Yesu alikuwa amewaahidi Roho huyo. Katika somo la injili Kristo anasema atakapokuja huyo Roho, atawakumbusha yote niliyowafundisha. Kumbe kazi ya Roho Mtakatifu ni kutukumbusha.
Tumwombe Mungu Leo atupe Roho Mtakatifu ili tuweze kukumbuka yote aliyotutendea Mungu. Mara nyingi huwa tunasahau sana alikotutoa Mungu. Mara nyingi huwa tunasahau aliyotutendea Mungu, tunahitaji Roho Mtakatifu atukumbushe. Lakini pia katika maisha ya Ndoa watu wanasahau sana walikotoka, kumbukeni kabla hamjaoana mlivyopendana, mlivyotembea pamoja huku mumeshikana mikono.
Leo hii mnaishije, mbona siku hizi na kama jeshini?ahadi kibao kabla ya Ndoa kwamba mtakuwa waaminifu nk je huo uaminifu Leo hii upo? Ndio maana nasema tunamuhitaji Roho atukumbushe yote. Hata sisi Watawa tunahitaji Roho wa Mungu atukumbushe kufanya utume wetu kwa uaminifu na kwa bidii kubwa. Kwa hiyo sisi sote tunahitaji Roho mtakatifu atukumbushe wajibu wetu kama mapadre, watawa, awakumbushe wajibu wenu wanandoa na cha muhimu kabisa atukumbushe ahadi tulizoweka.
Katika Somo la Injili, Yesu anawaaga Mitume wake na kuwapa wosia wa kumpenda Baba. Anasema ya kuwa tukimpenda Baba naye Baba atatupenda na watafanya makao kwetu. Yesu anataka kutuingiza katika Familia ya utatu mtakatifu. Kibali cha kuingia ni upendo ni kumpenda Mungu. Mwisho kabisa Yesu anatuachia amani. Anavyotupa amani ni tofauti na wanavyotoa watu wa ulimwengu huu. Ulimwengu hutoa amani kwa kupigana, bunduki, silaha nk. Hata Familia nyingi na ndoa nyingi hutafuta amani kwa kupigana. Wapendwa, ugomvi haujawahi kuleta amani. Yesu anataka mioyo yetu iwe na amani. Ila tutofautishe kutulia na kuwa na amani. Nchi, Familia au Ndoa inaweza kuwa imetulia tu lakini haina amani.
Watu wengi wametulia tu ila ndani ni maumivu, vinyongo, uchungu na chuki. Sio kila anayecheka ana amani, wengi hawalali, wengi hawana hamu ya Kula, wengi ndani wamejaa sumu. Yesu ana haja na mioyo yetu atupe amani ya ndani.
Kuna watu wana nyumba, gari, wake, waume, watoto, kazi ila hawana amani ili mjue amani haipatikani kwa mali Ila kwa Yesu tu. Yesu anataka afanye makao kwetu tumruhusu ili amani ipate kutawala.
Katika somo la pili Yohane anaona Yerusalemu mji mtakatifu una milango kumi na miwili uliyoandikwa Majina kumi na mawili ya makabila kumi na mawili ya waisraeli. Hii milango iko kila kona; kaskazini, kusini, magharibi na mashariki ili sisi sote tupate kuingia Katika mji huu. Mji wa Yerusalemu ni mzuri, watu wake hawaitaji taa kwa sababu wanaongozwa na nuru ya Mungu. Daima tuongozwe na nuru hii katika Maisha yetu ya Ndoa, Jumuiya, Familia, utawa na upadre.
Nawatakieni DOMINIKA njema ya kuongozwa na nuru ya Mungu.
No comments:
Post a Comment