CHANGAMOTO ZINAZOITIBUA AFYA YETU
Katika maisha ya kawaida, kuna changamoto nyingi. Kuna nyakati za kukubalika na mara nyingine kutokukubalika, kukataliwa na kupokelewa! Kuna kupata na kupoteza.
Kuna nyakati za furaha na masikitiko, kupanda na kushuka na maang’amuzi yanayofanana na hayo. Hali hizi hutupatia uzito moyoni na akilini.
Maumizo yanaweza kuwa ni chanzo cha hasira, chuki, kujisikia mkosaji, kujilaani, kuwa na mashaka na wasiwasi, msongo na mfadhaiko. Ili kuwa na afya njema inafaa kufahamu namna ya kukabiliana na hali kama hizo.
Ikiwa mmoja amekutendea kwa namna ambayo si njema – kuumizwa, mrejesho haupaswi kuwa ubaridi, vita na vurugu. Huko ni kuweka chumvi kwenye kidonda kibichi.
HASIRA NI NINI?
Hisia kali ndani ya nafsi zetu zinaweza kuwa ni chanzo ya majeraha makubwa kwa akili na miili yetu. Hasira, chuki na huzuni huweza kung’oa uzuri wa mahusiano baina yetu.
Hasira imekuwa ni chanzo cha malalamishi kwa kushindwa kwetu kusonga mbele na majanga yanayotufika, licha ya kwamba anayedhaniwa ni msababishi, huenda hana hata habari ya kile kinachoendelea ndani yetu. Tunapokuwa na hasira na huzuni kali, tunavunjika moyo mapema na kukata tamaa mara.
Wengi wetu tunakuwa ‘faru waliojeruhiwa’ ambao tunawashambulia wote walio mbele yetu hata kama sio wakosaji kwani mara nyingi tunajiona kwamba hatuko salama (insecurity).
Wengi tunajitenga sio tu nafsi zetu, ila pia na majirani, mazingira, hatimaye na Mungu kwani katika hao kuna giza nene.
Hasira ni adui mkubwa wa amani na usalama wetu, lakini pia ni ukuta mkubwa wa kuweza kusamehe. Ukiwa na hasira kali huwezi kuruka kihunzi hicho
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea...
No comments:
Post a Comment