Tuesday, February 4, 2020

HOMILIA IJUMAA KUU C

IJUMAA KUU: HOMILIA
somo la kwanza: Isaia 52:13-53:12
Somo la pili: Her 4:14-16;7-9
Injili: Yn 18:1-19,42

HATUABUDU SANAMU TUNAABUDU WOKOVU WETU.

Wapendwa wa Mungu Tumsifu Yesu Kristo,
Leo ni siku ya Ijumaa kuu, ila najiuliza ni kitu gani kikuu au kikubwa siku hii ya mateso? Kwa kingereza siku hii inaitwa Good Friday, but what is so good on this day of passion? kumbe leo ni siku muhimu sana kwa sababu Leo Yesu anatimiza lengo lake la kuja ulimwenguni.

Ukweli ni kwamba Leo tunakumbuka wokovu wetu, Leo Yesu anakufa kwa ajili yetu na hii ndio habari njema, hii ndio ijumaa kuu. Ni kuu kwa sababu Yesu anamwaga Damu ili tuokolewe.

Baada ya kutafakari sana juu ya fumbo hili la msalaba, nimegundua kuwa, njia yetu ni njia ya msalaba. Njia ya msalaba ina vituo vingi.  Kabla ya kufikia ufufuko Yesu alipitia vituo vingi ya msalaba. Kumbe hata sisi tutapita katika vituo vingi ili kufikia malengo yetu.

Ili kufikia malengo yetu ya kuwa na Kristo, hatuwezi kukwepa vituo vya msalaba. Kuna kuanguka, kunakumwaga jasho, kuna kubeba msalaba, kuna kupigwa mijeledi nk ila baada ya vituo hivi, kuna utukufu, kuna furaha na ushindi.

Siku ya Leo imegawanyika katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni neno la Mungu, sehemu ya pili ni kuabudu Msalaba Mtakatifu na mwisho Ekaristi takatifu. Ninauhakika sehemu ya Neno la Mungu na Ekaristi haina utata. Ila utata ni kwamba, kwa nini tuabudu msalaba.

Hata kwa wakatoliki wengi hapa pamekuwa na utata Mara nyingi. Naomba nirudi katika kitabu cha kutoka 20:4. Ni kweli Mungu aliwakataza waisraeli kuchonga sanamu, kwa sababu Mungu alijua udhaifu wao kwani huko misri waliabudu sanamu sana.

Mungu aliwakataza wasiendelee na mambo ya misri. Lakini baada ya waisraeli kumjua Mungu vema, sasa Mungu yuyo huyo anawaruhusu kutengeneza sanamu rej kutoka 25:18-22. Tena anaruhusu sanamu zitumike katika madhabahu na pia katika kiti chake cha rehema. Mungu hachukii sanamu bali anachukia sanamu zinazo abudiwa.

Pia Mungu aliruhusu sanamu zitengenezwe katika patakatifu pa patakatifu rej. 2 nyakati 3:10. Kwa hiyo kanisa katoliki haliabudu sanamu nakataa kabisa na mimi ni mmoja wa wakatoliki, sijawahi kuabudu sanamu. Ila tunaheshimu ujumbe uliobebwa katika sanamu hizo.

Musa alipoambiwa atengeneze nyoka ya shaba rej. Hesabu 21:8 baadae suleimani anasema, waliotazama alama hiyo, yaani nyoka ya shaba walipona, ila kilichowaponya sio nyoka ya shaba bali ni Mungu aliye mkombozi wa watu wote rej. Hekima 16:7. Kwa hiyo ndugu zangu tunachoabudu leo ni wokovu wetu wala si sanamu. Tunapoangalia msalaba, kuugusa au kuubusu tunabusu Yesu aliyekufa, tunabusu wokovu wetu.

Kumbukeni  leo hakuna padre anayeadhimisha misa. Nimewahi kusikia watu wengi wakisema ibada ya Ijumaa kuu ni misa. Jamani ijumaa kuu hakuna misa. Ila Yesu anaadhimisha misa mwenyewe msalabani.

Altare yetu Leo ni msalaba, mkate na Divai ni Yesu mwenyewe na kuhani au padre ni Yesu mwenyewe. Aliyoyafundisha Kristo Jana kwa maneno, Leo anayafanya kwa matendo. Kwa hiyo msalabani kristo anajitoa sadaka kwa ajili yetu sisi wakosefu. Kwa hiyo msalaba unabaki kuwa ishara ya wokovu wetu na ni lazima kuuheshimu.

Kama tunaheshimu vitu tulivyo navyo kama vile: Nyumba, gari, mashamba nk. Kwa nini tusiheshimu msalaba uliotuletea wokovu? Ila tunachoabudu siku hii ya leo ni Yesu ambaye ni wokovu wetu. Ndio maana leo tunapopiga magoti mbele ya msalaba tunasema, tunakuabudu ee Yesu na tunakutukuza.

Sasa hapo anayeabudiwa ni Yesu au ni sanamu jamani? Lakini hata wakati wa kuonyesha msalaba Padre au shemasi anasema; huu ndio mti wa msalaba ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake.

Kwa hiyo tunapopiga magoti mbele ya msalaba, tunapoubusu twende zaidi, tutumie macho ya roho sana kuliko ya nyama. Kwenye msalaba tuone wokovu wetu, tuone ushindi wetu. Ila tukitumia macho ya mwili tunaona sanamu au vipande vya mbao.

Sasa nirudi kwenye historia ya mateso, Katika historia ya mateso, wahusika ni wengi ila naomba Leo ni mguse petro na Yuda. Yuda bado hajabadilisha mawazo yake ya kushirikiana na wauaji. Lakini tusimwangalie Yuda leo, tujiangalie sisi wenyewe, kwaresima inapoisha ivo, je, mawazo yetu ni yale yale au tumebadilika. Ukihamishia nyani kwenye msitu mpya wanabaki kuwa wale wale.

Si ajabu tunaingia katika kipindi cha pasaka lakini mawazo ni yale yale. Dhambi ni zile zile, nyani ni wale wale msitu tu ndo umebadilika. Kumbe akina Yuda tupo wengi ambao hatuko tayari kubadilika. Anampiga Yesu busu ya kinafiki. Yuda kwa nje ni mwema sana, safi ila ndani ni hatari, amebeba sumu kali.

Ndivyo tulivyo wakati mwingine, wema sana kwa nje, kwa nje tunacheka na marafiki ila wengi ndani wanakuwa na roho kama ya Yuda. Hatari sana. Wakati mwingine afadhali kuishi na maadui, ukajua unaishi na maadui kuliko kuishi na marafiki wanafiki kama Yuda.

Tuombeane kwa sababu roho kama hii ya Yuda ikiingia kwenye Familia au Jumuiya ni hatari. Roho ya usaliti ikiingia kwenye ndoa, hiyo ndoa hamna tena. Nilikuwa pia nawalinganisha petro na Yuda,  kosa la petro lilikuwa ni kubwa sana. Alimkana Yesu Mara tatu, ni Mara ngapi petro alienda na Yesu katika ziara zake? Petro alishawahi kumkiri Yesu kuwa Kristo mwana wa Mungu. Petro alikuwa na uelewa mkubwa wa Yesu kuliko Yuda.

Yuda alikuwa haambatani na Yesu Mara nyingi kama Petro. Maanake petro alimjua Yesu kwa asilimia kubwa kuliko Yuda, ila Leo anamkana rafiki yake live. Wapendwa inauma, hii ya Petro inauma, kumkana rafiki hadharani tena Mara tatu.

Wewe fikiria kukanwa na rafiki hadharani, rafiki uliekuwa nae muda mrefu, umekunywa na kula nae mara nyingi, leo mbele za watu anasema hakujui kabisa. Yaani inauma. Lakini hata kama alimkana Yesu, Petro ni tofauti sana na Yuda kwa sababu alizichukia dhambi zake na akalia sana kwa ajili ya dhambi hizo. Petro anapatana na Kristo mapema kabla hajakata roho. Yuda hakufanya ivo na hii ndio tofauti kati ya Petro na Yuda.

Sasa nikirudi kwa Yesu, yeye  akiwa pale msalabani anasema ana kiu, ila sio kiu ya bia au juisi au maji. Ilikuwa kiu ya kutukomboa sisi. Ana kiu hata sasa, ana kiu ya kubadilisha mioyo yetu, ana kiu na maisha yetu, ana kiu ya kutusamehe. Tunatakiwa tuipooze kiu ya Yesu kwa kutubu na kuanza upya.

Wengi wetu tunakiongeza kiu cha Yesu kwa kutenda dhambi. Tunapotenda wema tunapooza kiu ya Yesu na kumfanya aseme; yamekwisha.  Tunapoungama vizuri, Yesu anasema, yamekwisha, tunaposemeheana anasema yamekwisha.

Wapendwa tukumbuke Yesu anakufa kifo cha aibu sana kwa ajili Yetu. Waliotundikwa msalabani walikuwa ni wahalifu. Makosa yao yaliandikwa juu ya msalaba ili kila mmoja hata wapita njia wayaone makosa yao.

Ila badala ya kuandika makosa ya Yesu juu ya msalaba wake, waliandika Kristu Mnazareti mfalme wa wayahudi. Ila wayahudi walimkataa, wakasema si mfalme wetu, hata sisi tunapoendelea kutenda dhambi na kuzishabikia, tunamkataa Yesu. Basi Leo iwe ni siku ya kupooza kiu ya Kristu kwa kutubu.

Ijumaa kuu njema ya kupooza kiu ya Yesu.

Ni mimi Kaka Niliye mdogo kuliko wote

No comments: