ILI MSAMAHA UFANYIKE SHAMBULIA TATIZO NA SI WATU
Tukisoma katika kitabu cha Mithali 15:1 “Jawabu la upole hugeuza hasira, bali neno liumizalo huchochea gadhabu.” Tena tunasoma: Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara, utamu wa maneno huongeza elimu (rej. Mith 16: 21). Kulaumu hakusaidii.
Kuwafananisha maadui zetu na uovu ni kukataa ukweli kwamba wao wana sehemu ya Mungu ndani yao: Wameumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu.
Kwamba wao pia ni Hekalu la Roho Mtakatifu, tena kwamba wamekombolewa na damu ya Kristo. Huku ni kumdhalilisha Mungu aliyeumba kwa ufundi mkubwa sana.
Tutamadunishe maisha ya Upendo: Maisha yasiyo na upendo ni chanzo cha mateso na mahangaiko yasiyo na idadi kati ya wanadamu ikiwa ni pamoja na kutokusamehe.
Tiba pekee ya kubandukana na magonjwa ya ajabu ajabu na kuzeeka hovyo kabla ya wakati wetu ni kujenga utamaduni wa kusamehe.
Hali hii inatualika kuishi maisha ya upendo. Upendo ni mpango nafsi na kujitosheleza nafsi.
Moyo wa upendo pekee unaweza kushinda hali ya kutosamehe, kutuwezesha kusamehe na kuwianisha maisha.
Maisha ya upendo hutuwezesha sisi kuwa na joto, kuhusiana, kutuungasha, na daima kujitahidi kuwianisha na kustawisha maisha yetu na ya wengine.
Kwa hiyo, upendo unaumba maisha, lakini pia huunganisha watu katika gundi inayowaweka wanandoa, familia, marafiki na jumuiya pamoja.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea
No comments:
Post a Comment