FURAHIA MAISHA HAIJALISHI UNAJIKUTA KATIKA HALI GANI
USIKUBALI KUTUMIKISHWA NA HASIRA AU CHUKI, SAMEHE NA FURAHIA MAISHA
Unaweza kuwa na hitilafu, madhaifu au dosari, huenda una wasiwasi au dukuduku, pengine mwingi wa hasira kila wakati.
Hata hivyo usisahau kwamba wewe ni wa pekee, maisha yako ni ya maana kuliko mradi mwingine wowote uliowahi kuwapo, uliopo na utakao kuwapo hapa duniani.
Kutokana na unyeti wa kile ulicho, ni wewe tu mwenye uwezo na mamlaka ya kuamua hatima ya maisha yako ukipenda.
Tambua kwamba, wapo wengi wanaokupenda, wanaokuthamini, kukujali tena kufurahia uwepo wako. Kumbuka kwamba maisha ya furaha sio kuwa na
· Anga lisilo na tufani au· Bahari isiyo na dhoruba,· Barabara isiyo na kona, matuta au ajali,· Kazi isiyochosha na kukatisha tamaa,· Mahusiano yasiyoridhisha na maudhi.
Kuwa na maisha ya furaha ni kutafuta nguvu katika uwezo wa kusamehe na kuachilia, kuwa na matumaini katika mapambano, kujiona salama wakati wa hofu na mashaka, kujisikia kupendwa hata katika hali ya kutoelewana na kupatana na wengine.
Kuwa na furaha ya kweli sio tu kufurahia tabasamu, lakini pia kutafakari juu ya huzuni, maumivu na mateso.
· Sio tu katika kusherehekea kufaulu, bali pia kujifunza kutokana na kushindwa kwetu.
· Sio tu kufurahia unaposhangiliwa ukipigiwa makofi, lakini zaidi mno kufurahia kutojulikana na kutambuliwa hata kati ya watu.
Furaha ya kweli sio mwisho wa safari ila ni mafanikio kwa wale ambao wanaweza kusafiri kuingia katika nafsi zao.
· Kufurahia maisha ni kuachana na dhana ya kujiona kwamba wewe ni mhanga wa kushindwa, bali kuwa tayari kuandika historia na hatma ya kile unachopenda kuwa kwa maisha yako siku za mbeleni.
·Ni kule kuweza kutembea na kuvuka jangwa la majaribu, vishawishi, magumu na changamoto nyingine za kimaisha na kuweza kubaini oasis (mahali pa kujiburudisha) ya faraja na kitulizo nafsini mwetu.
· Ni kumshukuru Mungu kila kukicha asubuhi, unapobaini kwamba uwepo wetu kila siku ni mwendelezo wa miujiza ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuifunua kwetu.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538
Itaendelea
No comments:
Post a Comment