MSAMAHA NI KUJIWEKA HURU
Msamaha ni njia hakika ya kupata Uhuru kwa ajili yetu sisi wenyewe na maadui zetu.
Kutokusamehe ni kujihukumu kifungo gerezani, kuhusu hali yetu ya zamani na migogoro ya zamani, na kutoruhusu maisha mapya yenye dira na mwelekeo.
Kutokusamehe ni kujiachilia na kutangaza kushindwa kujitawala, hivyo kuwaruhusu wengine watutawale. Upya wa maisha unahujumiwa na kumezwa na maisha ya kale na hivyo mtu hakui na kufurahia maisha kama mtu mzima.
Tunaposongwa na mawazo ya chuki, hasira na kutaka kulipa kisasi, tunajisikia kujibebesha furushi mkubwa ndani ya mioyo yetu na hali hii inatunyima uhuru na uwajibikaji wetu wa kawaida.
Tunashindwa kutulia, kwa kuwa yule aliyetuudhi anatawala akili zetu na hivyo anakuwa na nguvu juu yetu.
Tunajiweka wenyewe huru, pale tu, tutakapowasamehe. Na baada ya kusamehe, wanaotuudhi hawana tena madaraka na mamlaka juu yetu. Hawatawali tena hisia na fikira zetu.
Kwa msamaha tunatua furushi kubwa la utumwa, mawazo ya kisasi na kujitawala sisi wenyewe.
Msamaha unatuweka sisi huru kiakili, kifikra, katika mahusiano, na ugumu wa moyo. Msamaha unatutoa kutoka zama za huzuni kuelekea siku za matumaini, furaha na usitawi. Kwa msamaha tunajiweka huru na kuendelea mbele kimaisha.
Nguvu tuliyoitumia kupambana na majeraha ya zamani sasa inatumika kujenga usitawi wa maisha ya baadaye katika ukamilifu wake.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Jipatie nakala ya kitabu cha UPONYAJI WA MAJERAHA YA NAFSI KUPITIA MSAMAHA
No comments:
Post a Comment