MIITO YA NDOA, UPADRE NA UTAWA KATIKA ZAMA ZA MFADHAIKO
Kadiri tunavyoona sasa, ni kwamba kwa baadhi ya majimbo na Mashirika idadi ya wale wanaoingia seminari na nyumba za malezi inapungua kila kukicha katika baadhi ya maeneo ya dunia.
Kadhalika, idadi ya wale *wanaothubutu kuingia na kubaki kwenye taasisi ya ndoa _takatifu_ inazidi kudhoofu.
Katika hali kama hii, swali la msingi linaibuka: nini kinatokea hapa? Wengi wetu tuna maelekeo ya kulaumu wengine au kuelekeza lawama kule ambako siko.
Ni wakati muafaka kujichunguza na kufanya tathmini ya kina kuona na kubaini ukweli wa kile kinachoendelea, hata kama hatima ya tathmini yetu itatuumiza na kutuchefua kwa jinsi ambavyo sisi wenyewe tumehusika au kusababisha kupungua kwa mwitiko wa miito katika familia, mashirika yetu au majimbo yetu.
Huenda sehemu kubwa ikawa ni kukosekana kwa ushuhuda wa maisha kwa wale ambao wameshaingia kwenye maisha yale.
Ni changamoto kwa wazazi, watawa na mapadre kuona kama namna yao ya kuishi inachochea wengine kuvutwa au inawasukumizia pembezoni!
Katika lugha ya kiteolojia, wito ni zawadi ya Kristo kwa mwanadamu, zawadi iliyotolewa kwa Kanisa na ulimwengu, katika nyakati na fursa maalumu, kwa makusudi kamili ya kuendeleza kazi ya uumbaji au/na ukombozi wa watu wote.
Kristo ndiye anayetuita katika maisha ya ndoa, ukasisi na utawa akitupatia neema inayohitajika ili kuutambua wito ule, kuupokea mwaliko huo, kudumu kiaminifu katika maisha hayo mapya, tukimrudishia Mungu sifa na utukufu, kwa uhakika wa kupokea taji ya uzima wa milele kwa kadiri ya ukarimu wa Mungu mwenyewe.
Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538
No comments:
Post a Comment