Tuesday, February 4, 2020

DOMINIKA 4 KWARESMA C

DOMINIKA 4 YA KWARESMA NI  YA LAETARE YAANI FULL KUFURAHI.

somo la kwanza: Yoshua 5:9a, 10-12
Somo la pili: 2kor 5:17-21
Injili: Luka 15:1-3,11-32.

Jamani popote mlipo Tumsifu Yesu Kristooooooooo, Leo tumefika nusu ya kipindi cha kwaresima tunatakiwa kujitadhmini tuone tumeitumiaje nusu ya kwanza ya KWARESIMA .

Kama tumeitumia vizuri sifa na utukufu zimrudie Bwana wa mbingu na nchi. Ila kama tumeitumia vibaya bado tuna nusu nyingine basi tuitumie vizuri. Jumapili ya leo inaitwa LAETARE kwa kilatini,  maanake Furahi. Bila shaka ni DOMINIKA YA furaha kwa sababu tuna matumaini ya kuuona utukufu wa ufufuko.

Tuendelee basi kuitafakari safari yetu ya kwaresma, ila kwa vyovyote vile tusikubali kumaliza vibaya. Leo katika somo la kwanza, waisraeli wanamaliza safari yao ya miaka arobaine.

Ila kumbuka walioimaliza safari hii  ni wale tu waliovumilia changamoto za nyikani. Wengi wao hawakufikia lengo lao kwa sababu walirudi nyuma, walilalamika na wengine kukata tamaa.

Ndio safari ilikuwa ndefu na yenye changamoto ila waliovumilia  jua, kiu, uchovu na na changamoto nyingine nyingi ndio waliouona mwisho wa safari yao. Hakuna marefu yasiyo na mwisho, yawezekana hata wewe upo kwenye safari ya mateso, magonjwa, manyanyaso, nk. 

Usikate tamaa utakuja tu kuuona mwisho mzuri wa safari yako. Hayo mateso yana mwisho, hayo maumivu yana mwisho, huo uonevu una mwisho, hayo mahangaiko yana kikomo ila watakaovumilia watauona mwisho wa safari zao. Kama waisraeli tunashindwa sana kuvumilia na hivyo kushindwa kuuona mwisho wa safari yetu au tunashindwa kufikia malengo yetu.

Leo waisraeli wanafanya karamu ya kukumbuka walivyotoka utumwani. Ni vizuri kukumbuka, Mara nyingi tunasahau sana tuliko toka. Baada ya mafanikio huwa tunasahau sana, unakumbuka wazazi walikokutoa wewe? unakumbuka mlikotoka na mwenzako wa ndoa?

Wengi wetu tunasahau sana. Kijana tunayemsoma katika Injili alisahau baba yake alikomtoa na pia alisahau kuwa ya Dunia yana mwisho wake.

Dunia haileti furaha mara nyingi inaleta majuto na masikitiko. Kwanza kabisa huyu kijana alikuwa ni mkorofi, alikuwa hana mamlaka ya kuomba mali kabla ya kifo cha baba yake, kufanya hivyo ni sawa sawa na kumuua baba yake, tena alitakiwa apewe theluthi tu ya mali kwani alikuwa kijana wa mwisho. Kwa sababu ya ukorofi wake huu na kulingana na Desturi za waisraeli alitakiwa apigwe mawe afe,  ila baba yake hakuruhusu.

Kumbe huruma ya baba inaanza kuonekana mwanzoni kabisa. Ila nilikuwa najiuliza hivi; huyu kijana alikosa nini kwa baba yake mpaka aende kuishi mbali ivo? Nafikiri sio pesa au mali. Kumbuka baba yake alikuwa tajiri mkubwa, angeomba pesa angepewa tu za kutosha.

Kumbe hakukosa pesa wala mali, ila huyu kijana alikosa furaha ndani ya Familia yake. Akafikiri ataipata nje ya Familia yake, kumbe furaha ya kweli aliiacha ndani ya Familia yake. Mara ngapi ndugu umefikiri ndoa yako haina furaha na ukaitafuta nje, 

Mara ngapi umefikiri ukatoliki hauna maana ukaanza kutangatanga na kuhangaika na manabii wa uongo na waganga wa kienyeji. 

Mara ngapi jumuiya zetu tunaziona hazifai na kuona za wengine ndio bora. Ndugu yangu sasa rudi nyumbani kumenogaaaaaaa. Huyu kijana aliondoka kwa mbwembwe nyingi akaenda mbali na baba.

Kukaa mbali na nyumbani ni sawasawa na kupotea kabisa, ndio maana mwishoni baba anasema alikuwa amepotea. Kukaa mbali na Mungu au mbali na sakramenti za kanisa ni kupotea. Wewe unayenifuatilia una sakramenti?  Kanisani unaenda? Jumuiyani je? Uko karibu na Mungu? Wangapi humu tumepotea?

Huyu kijana alikaa mbali na baba na kwenda kufurahi na marafiki lakini ilifika wakati akafulia kweli. Pesa ilipomuishia aliamua Kula na nguruwe.

Yaani alishuka kiwango akafanana na nguruwe, hadhi yake inashuka hasa, aliyekula nyama choma na bia, michemsho, sasa anakula pumba na nguruwe, anakula sahani moja na nguruwe, Mara ngapi aliwatimua wahudumu kisa hawajasafisha glasi ya bia vizuri, Mara ngapi aligomba chakula hakijapikwa vizuri sasa anakula sahani moja na nguruwe. Ndivyo dhambi inavyotushushaga hadhi. Kwa muisraeli kulisha nguruwe ni kosa kubwa sana.

Anakubali kuwa mtoto wa nguruwe kwani anakula na nguruwe. Nguruwe kwa waisraeli ni shetani, kumbe anabadilika na kuwa mtoto wa shetani. Huyu kijana anakuwa mtumwa sasa, maanake anarudi tena misri.

Mara ngapi mimi na wewe tunarudi misri kwa kutenda dhambi. Toka misri, ondoka kwenye mabanda ya nguruwe, yaani mabanda ya dhambi.

Niliposoma huu mstari nimepatwa na hasira kali sana. Alipokuwa na pesa alikuwa na marafiki wengi, sijui alikula na wangapi, sijui alikunywa na wangapi, sijui alilala na wangapi ila hela ilipokatika tu, alijikuta mwenyewe.

Marafiki waliomzunguka na kumsifia wako wapi sasa, waliomfuta jasho wako wapi, mabinti wazuri wako wapi? Maskini yupo kwenye Banda la nguruwe peke yake.

Marafiki hawakumsindikiza kwenye Banda la nguruwe. Ndugu yangu asilimia kubwa ya marafiki ni matapeli, kuna watu watakusifia wakati unacho ila ukiishiwa huwaoni tena wanakuacha upambane na hali yako. Hako kanyumba ndogo unafikiri kanakupenda sana baba yangu ni uongo.

Siku inakuja utakapoishiwa pesa na nguvu hutakuwa na dhamani tena. Rudi Nyumbani dear kumenogaaaaa. Atakayekujali katika umaskini wako ni mkeo rudi kwake, ni mumeo tu rudi kwake. Hako kamchepuko katakuacha tu peke yako kwenye Banda la nguruwe.

Mabinti wangapi wamepewa mimba na kuachwa wapambane na hali zao. Angalia kijana nakwambia mapema kabla hujaachwa kwenye banda la nguruwe peke yako.

Kuna watu katika maisha yako watakuja tu kukutumia tu ukishaisha ladha wanakutupa. Vijana muwe makini, usikubali kutumika na kutupwa kwa gharama yoyote Ile kataa kabisa.

Wewe ni wa dhamani umenunuliwa kwa gharama. Ila nimeyafurahia maamuzi ya kijana huyu, alichukua maamuzi magumu kweli aliposema nitaondoka, nitanyanyuka, nitatoka kwenye mabanda haya nitaenda kwa baba.

KWARESIMA ni kipindi cha kuyaacha mabanda ya dhambi na kurudi kwa baba. Kumbuka alivyoondoka kwa kiburi na mbwembwe, labda pia alimtukana baba hatujui, sasa anataka kurudi. Hakika ni maamuzi magumu na ya ujasiri.

Wakati mwingine tuchukue maamuzi magumu ya kutubu dhambi, maamuzi magumu ya kuacha michepuko, ndio ananipenda, ndio nimemnunulia gari na viwanja ila inatosha narudi nyumbani. Haya ni maamuzi magumu na ya ujasiri.

Toba ya kweli huanza moyoni, kabla ya kwenda kwa baba alitubu sana moyoni. Akasema yuko tayari kuwa mtumwa kuliko kuwa mwana. Ila nafikiri alichukua uamuzi mzuri wa kutaka kuitwa mtumwa.

Mtumwa hakatai anachoambiwa na bwana wake, yuko tayari kufanya chochote. Kumbe kule  kutaka kuitwa mtumwa, huyu kijana yuko tayari kutii sasa, yuko tayari kuyafanya mapenzi ya baba yake. Afadhali kuwa mtumwa. Sisi ni watumishi.

Jamani mapadre wenzangu sisi ni watumishi sio mabosi. Ole wako paroko wangu, ole wako msaidizi kama tunajiona mabosi. Tuna bosi mmoja tu aliye juu sana. Upanga wangu Leo unakata kote kote simuachi mdhambi yeyote salama.

Nirudi tena kwa kijana wangu, aliporudi nyumbani, mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni baba yake. Maanake baba alikuwa akimsubiri sana mwanae,  bado baba alikuwa na haja nae. 

Alipishana njiani na watu wengi sana na yawezekana hawakumtambua kwa sababu alikuwa mchafu, amevaa matambara na hawakutegemea mtu aliyetoka nyumbani kwa mbwembwe nyingi arudi kama mtumwa. Binadamu huangalia kwa nje ila baba aliangalia moyo akaona toba ya kweli.

Ndugu yangu baba anakusubiri urudi kutoka kwenye Banda la dhambi. Embu angalia hata kabla kijana hajamaliza kutubu baba yake anaagiza nguo nzuri ili kumvalisha.

Kumbe alikuwa uchi na baba alitaka kuuficha uchi wake. Tunapotubu baba anatufichia uchi wetu anatuvalisha nguo ya utakatifu. Anamvalisha Pete pia, yaani  kumpa mamlaka, pete ilikuwa ishara ya mamlaka. Yeye ni mtoto wa Baba, ana mamlaka.

Sisi pia kama ni wana wa Mungu kweli tuna mamlaka. Mamlaka juu ya shetani na maovu yake. Baba pia alimvalisha vitatu, maanake kumpandishia hadhi yake. Tunapotubu baba anatupandisha juu. Tunakuwa watu wenye mamlaka na hadhi.

Baada ya hayo akamfanyia sherehe kubwa. Kila siku Mungu hutufanyia karamu ya Ekaristi, ila kuila karamu hii kwanza tunatakiwa tutubu. Kumbuka Baba hakuanza na karamu, kwanza kijana alitubu, akasamehewa ndio karamu ikafuata.

Tubu kwanza kabla ya kupokea Yesu wa Ekaristi. Ila cha kushangaza ni kwamba Yule kaka mkubwa hakutambua karamu hiyo. Alimkataa mdogo wake na kumuita Malaya. Hakuona mdogo wake, aliona Malaya. Mara ngapi hata sisi katika familia na katika jamii pia hatuwatambui wadogo zetu na kaka zetu.

Kwa sababu alinikosea mahusiano yanakatika. Embu sikiliza alivyo sema kaka mkubwa, "tazama nimekutumikia miaka mangapi" maanake yeye katika familia yake alijiona kuwa ni mtumwa.

Mara ngapi wewe mwanandoa anajiona mtumwa? Badala ya kujiona mke, mama, mume na baba anajiona mtumwa kwenye ndoa yako. Jamani poleee.

Mara ngapi najiona padre mtumwa, mtawa mtumwa katika kanisa au shirika langu. Huyu kaka alikuwa mchapa kazi sawa, alikuwa mtiifu sawa, hakuvunja sheria sawa ila alikuwa hana utu. Hakuona mdogo wake aliona Malaya. Hakika hii ni roho mbaya.

Wangapi tunaenda kanisani sawa, zaka tunatoa sawa, sadaka hata ya pili sawa, mavuno safi ila bado tuna roho mbaya, hatuwapendi wenzetu, jamani hii haikuletei baraka, ndugu katubu haraka.

Tatizo hapa ni kujiona mwema na kushindwa kutambua maovu yetu. Nampenda sana yule mdogo, hakumsingizia mtu yeyote alisema nitamwambia Baba nimekosa mimi.

Si  mwingine ni mimi hapa na kwa sababu ya kuona dhambi zake akasamehewa. Tatizo la mkubwa anajiona mtakatifu sana kumbe hata lilikuwa jukumu lake kama kaka kumshauri mdogo wake, hakufanya ivyo.

Dogo anaondoka anamuangalia tu kuliko kumshauri. Hatimaye alibaki nje. Hata baba alipomwita aliendelea kukaa tu nje. Baba yake hakuweza kumkumbatia,kumbusu na kumvalisha nguo kwa sababu alibaki nje. Wanaobaki nje ni wapumbavu.

Rejea mt.25 wanawali watano wapumbavu walibaki nje.  KWARESIMA hii Baba anataka uingie ndani, usikae nje, usiwe mpumbavu. Ndio maana Paulo anatusihi tukae ndani ya kristo ambaye ni mpatanishi wetu na mtetezi wetu.

Nawatakia DOMINIKA njema ya kutoka kwenye Banda la dhambi.

Ni ndugu Niliye mdogo sana kuliko wote

No comments: