Tuesday, February 4, 2020

KUNA UHITAJI WA KUJISAMEHE SISI WENYEWE

KUNA HITAJI LA KUJISAMEHE SISI WENYEWE PIA

Ili kuwa maisha ya furaha, kama tunavyohitajika kuwasamehe waliotuudhi, tunalazimika pia kujisamehe sisi wenyewe.

Tunajikosea na kujiumiza sisi wenyewe mara kadhaa tunajilaumu wenyewe, tunajilaani wenyewe, tunajiona wakosaji na kujichukia tunaposhindwa kufikia malengo yetu au tunaposhindwa kupambana na madhaifu na vilema vyetu.

Wengi wetu kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskarioti, si ajabu tukashindwa kujisamehe sisi wenyewe, tukaishia kujinyonga.

Ni sheria kwamba sisi pia tunapaswa kuishi maisha halisi ya kibinadamu kuhusiana na hali yetu ya ndani, madhaifu, mipaka yetu na kuboresha yale tunayoweza, kujikubali, kujipenda na kujisamehe.

TUMESAMEHEWA: Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Tunaalikwa kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo, katika maisha na mafundisho yake.

Yesu mwenyewe anasema, “unapokuja kutolea sadaka yako, na huku unagundua kuwa ndugu yako ana neno nawe, iache sadaka yako mbele ya madhabahu ukapatane naye kwanza.” (rej Mt 5:23-25). Katika aya hizo unaweza kujifunza kwamba sala ya kweli ni sala ya Msamaha.

Yesu mwenyewe alitufundisha ile sala kuu ya “BABA YETU,” akitukumbusha kwamba Mwenyezi Mungu ni Baba yetu. Sisi ni sehemu ya familia yake.

Ni katika ukweli huo kwamba kila mmoja tunayekutana naye katika maisha haya, haijalishi historia, hulka na tabia, taifa, rangi na imani, sote ni familia ya Mungu. Hawa wote ni ndugu tunaopaswa kuwapenda, kuwajali, kuwahurumia na kuwasamehe inapobidi.

Tukumbuke kwamba, kutokana na majeraha ya dhambi ya asili na dhambi tulizotenda kwa hiari yetu wenyewe, kiburi na majivuno, huweza kutuzalia hali ya kutosameheana na kujaliana. Huenda ikawa pia vigumu kutafakari wema, ukarimu, rehema na huruma ya tuliyopokea kutoka kwa Mungu mwenyewe.

Tukumbuke tena kwamba, kule kushindwa kusaheme au kupokea msamaha kumekuwa ni chanzo cha ubinafsi uliokubuhu, unaodhoofisha na kudumaza mapendo ya kweli, heshima na hadhi ya mwanadamu, na utulivu katika familia na jumuiya.

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea.....

No comments: