Tuesday, February 4, 2020

MSAMAHA NA MATESO YA YESU

MSAMAHA UNAWEZESHWA NA TAFAKARI JUU YA MATESO YA KRISTO

Tafakari juu ya mateso ya Yesu na ya wanadamu wote hutusaidia sisi kusamehe. Yesu hakuwa na kosa lolote. Alifanya tu matendo mema, lakini alichukiwa, kusingiziwa, kushutumiwa, kudhalilishwa na kuteswa na kusulubiwa msalabani kama mhalifu.

Lakini wakati akiwa ameangikwa msalabani aliwaaombea maadui wake kwa Baba Mungu: “Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.”

Katika hali ya kufanana vile, tunawafahamu watu walioteseka pasipo kosa, Lakini waliwasamehe watesi wao na wakaendelea kuishi maisha ya amani na utulivu [Nelson Mandela Baba wa Taifa la Afrika Kusini ni mfano mmoja wapo].

Tunapotafakari juu ya watu hawa tunapata mwanga zaidi kwa nini inatupasa kusamehe.

WAOMBEENI MAADUI ZENU: ongea na Mungu katika SALA kabla ya kuongea na mtu: Sala hutuandaa, kimwili, kiakili, kiroho katika kujiweka mbele ya Mungu ambaye ni mwingi wa huruma.

Ni katika mazingira ya sala, tunajikuta katika hali ya utulivu na moyo wa kusikiliza, kuelewa na kusamehe.

Mungu wa rehema, katika sala hutujalia Roho wake, anayetuwezesha kuwa kama Mwanae Yesu Kristo, aliyesamehe kutoka msalabani. msamaha ni tunda la sala inayorutubisha maisha, kutuleta pamoja, kutukamilisha na kutupatia uhuru wa ndani kabisa.

Ni muhimu sana kwamba ili zoezi la msamaha liende vizuri na liweze kufanyika, ongea na Mungu kabla ya kusema na mtu. Acha kukurupuka na kufuata vionjo. Jadili tatizo lako na Mungu.

Kama utaomba kwa ajili ya mgogoro huo kabla ya kusengenya na rafiki, mara nyingi utagundua kuwa Mungu atabadili moyo wako na atambadili yule mwingine bila msaada wako. Mahusiano yako yangekuwa bora ikiwa kila mara tunaanza na Mungu kwanza. 

Fr. Innocent Bahati OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)
+255 755552538// +255783942208
Itaendelea

No comments: