HURUMA NA MSAMAHA NI KUBWA KULIKO DHAMBI ZETU. TUMWIGE MUNGU KATIKA KUWASAMEHE WENGINE
Maandiko Matakatifu yanaongea sana juu ya kutostahili kwetu kuhurumiwa na upendo usio na masharti wa Mungu. Kwamba tumetenda dhambi, hakutuondolei, wala kumfanya Mungu aache kutupenda. Huruma na msamaha wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko dhambi tunazotenda.
Kimsingi Mungu anatufahamu kwa majina na sio kwa dhambi tulizotenda. Na hata kama tunaasi na kukataa kumpenda Mungu, Yeye anaendelea kutupenda. Haachi kutupenda kwani alituumba wa sura na mfano wake, na alifanya hivyo kwa makusudi kamili.
Yeye ni kama Baba mwenye Huruma anayesimuliwa katika Injili ya Luka sura ile ya 15, ambaye ana shauku, akimsubiri mwanae aliyefuja upendo wake arudi nyumbani.
Yeye yuko tayari kufanya sherehe kubwa na kutuvika tena utukufu ule ambao tumeupoteza kutokana na ujinga wetu wa kufikiri kwamba nje ya nyumbani kuna raha, kumbe karaha na udhia.
Dhambi zetu, kimsingi ni kukataa kupendwa na Mungu. Hata hivyo hata kama tunakataa kumpenda Mungu, Yeye haachi kutupenda sisi Maandiko yanatuhibitishia “Lakini Bwana aliyekuhuluku, ee Yakobo, Yeye aliyekuumba, ee Israel, asema hivi: Usiogope kwa sababu nimekukomboa, nimekuita kwa Jina lako wewe u wangu.
Upitapo katika maji mengi nitakuwa nawe, na katika mito haitakugharikisha, uendapo katika moto hutateketea, wala mwali wa moto hautakuunguza (Is 43:1-4; 1Kor 3:15); “Bali Mungu aonesha pendo lake, Yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa bado kwenye dhambi.” (rej. Rom 5:8).
Msamaha wa Mungu hauondolewi kutokana na uovu wetu kwa Mungu.
Kwa kutenda dhambi, tunajitenga na upendo wa Mungu, lakini Mungu hajitengi nasi ila anakuja karibu zaidi nasi. “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha, mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, naye pamoja nami, (rej Uf 3:20).
Mtume Paulo anasema: “Dhambi ilipozidi, Neema iliongezeka. (rej. Rum 5:20). Maneno haya yanalenga kutuambia kwamba hakuna mipaka katika upendo wa Mungu wala hakuna kizuizi kinachomfanya Mungu asitishe kutupenda na kutuhurumia.
Frt. Flavian Lutakangwa
No comments:
Post a Comment